DARAJA LA MAGARA KUKAMILIKA FEBRUARI MWAKANI, KWANDIKWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 11 October 2019

DARAJA LA MAGARA KUKAMILIKA FEBRUARI MWAKANI, KWANDIKWA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa (mwenye miwani) akitazama ramani ya barabara ya mchepuo ya Babati (Babati bypass), yenye urefu wa Km 36.8.

Mhandisi mshauri Mtani Silas Mtani (kulia), akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa mwelekeo wa barabara ya mchepuo ya Babati (Babati bypass), yenye urefu wa Km 36.8 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami mkoani Manyara barabara hiyo inayotarajia kupunguza msongamano wa magari ya masafa marefu kuingia mjini Babati ipo katika hatua ya usanifu wa kina.

Muonekano wa daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 ambalo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho mkoani Manyara, daraja hilo linaunganisha Wilaya za Babati na Mbulu.

Muonekano wa daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 ambalo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho mkoani Manyara, daraja hilo linaunganisha Wilaya za Babati na Mbulu.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa akisisitiza jambo kwa wahandisi wa Tanroads alipokagua ujenzi wa daraja la Magara na barabara unganishi za daraja hilo mkoani Manyara.

Mwanahabari Charles Masanyika wa mkoani Manyara akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa alipokagua ujenzi wa daraja la Magara na barabara unganishi daraja hilo linaunganisha wilayani za Babati na Mbulu.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa akisisitiza jambo kwa wahandisi wa Tanroads na mkandarasi China Railway Seventh Group (CRSG) anayejenga daraja la Magara na barabara unganishi za daraja hilo mkoani Manyara.

IMEELEZWA kuwa kukamilika kwa asilimia tisini kwa ujenzi wa daraja la Magara na barabara zake unganishi mkoani Manyara kutawezesha daraja hilo kukamilika na kupitika ifikapo Februari mwakani.

Daraja la Magara lenye urefu wa mita 84 na barabara zake unganishi zenye urefu wa Km 4 linaunganisha wilaya za Babati na Mbulu mkoani Manyara hivyo kukamilika kwake kutamaliza adha ya muda mrefu ya wananchi wa wilaya hizo.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa amesema kukamilika kwa daraja la Magara kunatoa fursa nyingine kwa Serikali kujipanga ili kuijenga barabara yote ya Mbuyu wa Mjerumani –Mbulu Km 63 na hivyo kuimarisha huduma za usafiri na utalii mkoani Manyara.

“Nimeridhishwa na kasi ya mkandarasi China Railway Seventh Group (CRSG) katika ujenzi huu hivyo niwaombe wananchi kuibua fursa za kiuchumi katika mkoa wa Manyara”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Amesema nia ya Serikali ni kuunganisha kwa barabara ya lami wilaya za mkoa wa Manyara, Arusha na Singida ili kuwa na muunganiko mzuri kati ya mikoa hiyo na ile ya kanda ya ziwa na hivyo kuhuisha huduma za utalii na biashara na hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara ya mchepuo ya Babati (Babati bypass), yenye urefu wa Km 36.8 na kusisitiza nia ya Serikali kujenga barabara hiyo kwa lami ili kupunguza msongamano wa magari ya masafa marefu mjini Babati.

Amemtaka Mhandisi mshauri wa barabara hiyo kuongeza kasi ya kazi ili barabara hiyo itakayouzunguka mji wa Babati ianze kujengwa.

“Serikali inatambua umuhimu wa mji wa Babati kama kiungo muhimu kwa mikoa ya kati na kaskazini hivyo barabara zake zitakuwa madhubuti katika kipindi kifupi kijacho”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS mkoani Manyara Eng. Frank Lwenge amesema mkoa umejipanga kuhakikisha thamani ya fedha katika miradi yote inazingatiwa na miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.

No comments:

Post a Comment