HALMASHAURI ZATAKIWA KUENDELEZA VIJANA KUPITIA KILIMO CHA KISASA CHA KITALU NYUMBA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 11 October 2019

HALMASHAURI ZATAKIWA KUENDELEZA VIJANA KUPITIA KILIMO CHA KISASA CHA KITALU NYUMBA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria kufungua maadhimisho ya 17 ya Wiki ya Vijana yanayofanyika Mkoani Lindi katika viwanja vya Mpilipili. (Wa pili kutoka kulia) ni  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, na Mwakilishi wa UNFPA Bi. Tausi Hassani. (Wa nne kutoka Kulia) ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi na  Waziri wa Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Ali Karume.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia wanachi waliyohudhuria katika Uzinduzi wa Mafunzo kwa vijana kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba uliofanyika katika Viwanja vya Nanenane, Mkoani Lindi Oktoba 10, 2019.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri kuwawezesha vijana mikopo ya asilimia 4% ya mapato ya ndani wanayotenga kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujenga Vitalu Nyumba (Green House) vyao binafsi.
Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 10, 2019 wakati wa Uzinduzi wa Mafunzo kwa Vijana ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba katika Viwanja vya Nanenane, Ngongo Mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amesema vijana ni rasilimali muhimu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo katika jamii, hivyo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliamua kuwajengea vijana mazingira wezeshi ikiwemo kupata fursa za mikopo na ujuzi unahitajika ili waweze kushiriki kikamilifu katika shunguli za kimaendeleo.
Alieleza kuwa, Serikali iliamua kuanzisha utaratibu wa kila halmashauri kutenga asilimia 10% ya mapato yake kwa lengo la kutoa mikopo isiyo na riba kwa vijana asilimia 4%, wanawake asilimia 4% na wenye ulemavu asilimia 2%.
“Halmashauri zote zihakikishe zinatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana ili waweze kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo shughuli za kilimo zitakazowasaidia kujiajiri na kujiingizia kipato,”
Alifafanua kuwa sekta ya kilimo ndiyo kimbilio la wananchi wengi na kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba vijana wengi watapata ajira katika sekta hiyo kwa kuwa ina faida kubwa sana ikiwemo kupata mazao mengi katika eneo dogo na kupata mazao bora yanayokidhi viwango katika soko la ndani nan je ya nchi.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi yake imeendelea kuratibu programu ya ukuzaji ujuzi nchini na imeanza kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba katika Mikoa yote na Halmashauri zote nchini.  
Aidha alitoa wito kwa vijana kuendelea kujitokeza kwa wingi katika kuchangamkia fursa za mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi kupata ujuzi stahiki utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira.
“Nimefarijika kuona vijana waliopata mafunzo haya katika awamu ya kwanza wamekuwa na uwezo wa kujenga vitalu nyumba kwa ajili ya watu wengine waliotambua umuhimu wa kilimo cha aina hiyo, fursa hiyo ni ishara tosha kuwa vijana wameimarika katika mafunzo hayo,”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizindua Maadhimisho ya 17 ya Wiki ya Vijana Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Mpilipili na amewasihi vijana kuwa wazalendo na kutambua mchango wa Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika kuleta maendeleo ya nchi yetu na bara la afrika kwa ujumla.
Kwa Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alieleza kuwa Serikali imetoa kutoa mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa kwa teknolojia ya kitalu nyumba katika halmshauri zote nchini ambapo katika awamu ya kwanza mradi huo umefika katika halmashauri 83 hadi sasa lengo ni kufikisha ujuzi huo kwa vijana zaidi ya 18,000.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Gogfrey Zambi alisema kuwa vijana katika mkoa huo wamehamasika na mradi huo kwa kuwa wametambua una manufaa kwao.
“Programu hii imekuja wakati sahihi na imesaidia vijana kwa kiasi kikubwa kwa kuzingatia mafanikio yatokanayo na kilimo hiki cha kisasa kinacholeta tija,” alisema Zambi
Pamoja na hayo, Mkuu wa Mkoa alielezea hali ya usalama katika mkoa huo kulekea kwenye Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru zinazotarajiwa kufanyika Mkoani humo.
Pia Kijana Mmoja wapo aliyenufaika na mafunzo hayo Bw. Azizi Njenje ameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewajengea uwezo wa kujiamini na kuwafanya kuwa chachu katika kushiriki kwenye shughuli za kilimo.

No comments:

Post a Comment