WAZIRI HASUNGA AWASILI NCHINI ISRAEL KWA ZIARA YA KIKAZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 1 September 2019

WAZIRI HASUNGA AWASILI NCHINI ISRAEL KWA ZIARA YA KIKAZI

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa pamoja na mwenyeji wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Israel Brigedia Jenerali Kahema Juni Mziray (Mwambata wa Jeshi) mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion katika mji wa Telaviv nchini Israel kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku sita, leo tarehe 1 Septemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa pamoja na mwenyeji wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Israel Brigedia Jenerali Kahema Juni Mziray (Mwambata wa Jeshi) mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion katika mji wa Telaviv nchini Israel kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku sita, leo tarehe 1 Septemba 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).

Na Mathias Canal, Telaviv-Israel

WAZIRI wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) Septemba Mosi 2019 majira ya jioni amewasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Ben Gurion katika mji wa Telaviv nchini Israel kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku sita.

Katika uwanja huo wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion, Mhe Hasunga amepokelewa na mwenyeji wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Israel Brigedia Jenerali Kahema Juni Mziray (Mwambata wa Jeshi) kwa niaba ya Balozi wa Tanzania nchini Israel, Mhe Job Daud Masima.

Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku sita waziri Hasunga atashiriki mahafali ya mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies yatakayofanyika mjini Jerusalem tarehe 2 Septemba 2019. Mahafali hayo yatajumuisha vijana 1600 kutoka mataifa zaidi ya 12 ambapo kati ya hao vijana 45 ni watanzania, na kutoa vyeti kwa vijana hao wa Tanzania 45 watakaohitimu.

Akizungumza mara baada ya kuwasili nchini Israel Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepewa jumla ya nafasi 100 kwa ajili ya kupeleka vijana wa kitanzania kujifunza kilimo cha kisasa nchini Israel.

Alisema kuwa kupatikana na kwa nafasi hizo 100 ni kutokana na ombi la Rais wa Tanzania Mhe Dk. John Pombe Magufuli kwa serikali ya Israel ili kuwawezesha vijana wengi wa kitanzania kujifunza mbinu na teknolojia za kilimo cha kisasa.

Kadhalika, Waziri Hasunga atakutana na kurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Agro Studies ambapo miongoni mwa mazungumzo muhimu itakuwa ni pamoja na kumuomba uwezekano wa kuongezewa nafasi zaidi ili vijana wengi wa kitanzania waende kujifunza mbinu mpya za kilimo nchini Israel.

Pia, Mhe Hasunga atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo nchini Israel kujadiliana nae maeneo mbalimbali na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Katika mkutano mwingine, Mhe Hasunga atakutana na kufanya mazungumzo na wadau wawekezaji wakubwa wa sekta ya kilimo nchini Israel ili kuwaeleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania. Katika ziara hiyo tarehe 4 Septemba 2019 Mhe Hasunga atashiriki mapokezi ya vijana 100 ambao wapo nchini Israel kwa ajili ya kuanza mafunzo yao.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Israel Brigedia Jenerali Kahema Juni Mziray (Mwambata wa Jeshi) akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe Job Daud Masima mara baada ya kumpokea mwenyeji wake amesema kuwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Israel uliorejea mwaka 1995 baada ya kuvunjika mwaka 1963 unazidi kuimarika hivyo kutoa fursa kwa watanzania kujifunza mbinu bora za kilimo nchini Israel.

Alisema kuwa Tanzania kupitia nafasi za kimasomo zinazotolewa na Israel, itazidi kunufaika kwani nchi ya Israel ni moja ya nchi zinazoongoza katika utafiti wa maendeleo ya Kilimo na Teknolojia (Agriculture Research and Development).

No comments:

Post a Comment