Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akisisitiza jambo katika
Mkutano wake na Wasanii wa Sanaa mbalimbali kujadili mabadiliko ya Tasnia hiyo
nchini, mkutano huo ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius
Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wanachama
wa Chama wa Washereheshaji (SAA) wakifuatilia Mkutano wa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, kuhusu mabadiliko
mbalimbali Tasnia hiyo nchini, ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wasanii mbalimbali wakifutilia Mkutano
wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na
Wasanii wa Sanaa zote nchini katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius
Nyerere Jijini Dar es Salaam. (Picha na Idara ya Habari-MAELEZO).
Na Dianarose Shirima, MAELEZO
WAZIRI wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amekutana na wadau wa Sanaa
mbalimbali nchini katika kujadili
maendeleo ya tasnia hiyo, zikiwepo haki
za wasanii na jinsi ya kuboresha tasnia ya Sanaa na muziki ili wasanii waweze
kufaidika kwa kile wanachokifanya.
Akizungumza
katika Mkutano huo Waziri Mwakyembe amesema kuwa Serikali ipo tayari kupokea mapendekezo
ya wasanii kuhusu kuunganisha nguvu katika vyombo vya wasanii ambavyo ni
COSOTA, Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) NA Bodi ya Filamu Tanzania ili waweze
kuhudumia wasanii kwa maendeleo ya kazi zao.
“Sisi
tunawaletea mawazo tu, si Sheria, si Mswada ni mawazo ambayo yatamilikiwa na
ninyi baada ya kuyapitisha”, na ninyi kama wadau wa Sanaa na muziki waliohudhuria kwenye
mkutano huu mntakia kutoa mawazo yenu ili Tasnia hii iweze kufikia katika muafaka
mzuri ambao utaboresha kazi za wasanii na kutetea maslahi ya kazi zao, Alisema
Dkt.Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe
alisema kuwa Tasnia ya Sanaa na Mziki imekuwepo muda mrefu na imekuwa kimbilio
kwa vijana wengi, lakini imekuwa ikitajirisha baadhi ya watu na wengine kuachwa
nyuma kimaendeleo, kwa hiyo mabadiliko katika Tasnia hiyo hayana budi kutokea
ili kuleta ufanisi zaidi.
Aliongeza kuwa
mabadiliko hayo hayalengi kuvunja au kuingilia Mamlaka ya vyombo hivyo, bali lengo
lake ni kusogeza huduma karibu kwa ajili ya kurahisisha kazi kwa wasanii na
wadau wote wa Sanaa nchini.
Aidha Dkt.Mwakyembe
alisema kuwa mabadiliko hayo yatafanya vyombo hivyo kuwa na lugha moja ili
kuepuka wasanii kukamatwa au kufungiwa pale wanapokuwa wanafanya kazi zao
kutokana na utofauti wa kanuni na Sheria zilizopo.
“Kipindi cha mabadiliko
kimefika, watanzania tusiogope kufikiri katika tasnia hii, kwa muda mrefu
imekuwa ikisaidia sana lakini haiwezi kuwafaidisha wachache na wengine wabaki
masikini, haiwezekani ni lazima tufikirie njia itakayo tusaidia wote”, alisema
Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake Rais wa
Shirikisho la Sanaa za Maonyesho Tanzania, William Frank Chitanda, alisema kuwa
Mabadiliko ya kuiunganisha Basata na Bodi ya Filamu ziungane na COSOTA ihamishiwe
Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka Wizara ya Viwanda na
Biashara.
No comments:
Post a Comment