Muonekano wa hatua ya
ujenzi wa barabara ya Mtwara-Mnivata KM 50 kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa
barabara hiyo umefikia zaidi ya asilimia 50 na utagharamu zaidi ya shilingi
bilioni 89.
|
KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeupongeza Wakala wa Barabara Tanzania
(TANROADS), kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa na barabara
ya kuunganisha mkoa kwa mkoa kupitia mtandao wa barabara nchini.
Akizungumza mara baada
ya kupokea taarifa ya utekelezaji ya Wakala huo ilyowasilishwa kwa Wajumbe wa Kamati
jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso, amesema kuwa
kupitia utaratibu huo hata barabara zilizosahaulika nchini zinaweza kunufaika kwa
kuwa na maendeleo ya kiuchumi kutokana na uwepo wa miradi hiyo.
"Naipongeza Serikali
kupitia TANROADS kwa kufikiria kuunganisha mikoa kupitia barabara hususan
katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mikoa hii ilionekana kama
imesahaulika lakini sasa inaonekana kupata maendeleo kutokana na uwepo wa
miradi ya barabara ambayo inatekelezwa", amesema Mhe. Kakoso.
Aidha, Ameutaka Wakala
huo kuendelea kuziangalia na kuzipa kipaumbele barabara za kimkakati ambazo
zina maslahi mapana katika maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Ametaja miradi hiyo
kama barabara ya Mtwara- Mnivata, Katavi- Kigoma na Kasulu - Kagera ambayo kwa
pamoja ikikamilika itaunganisha mikoa hiyo na mikoa jirani na hatimaye kufungua
fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Mwenyekiti Kakoso,
ameusisitiza Wakala huo kuendelea na uboreshaji wa viwanja vya ndege hususan katika ujenzi wa majengo ya abiria
ambayo yanaendana na wingi wa abiria pamoja na kujenga uzio katika viwanja vya ndege
ambavyo havina uzio lengo likiwa ni kuweka usalama katika viwanja hivyo.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias
Kwandikwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ujenzi na ukarabati wa
barabara, madaraja na mizani.
Amefafanua kuwa hadi
kufikia Juni, 2019 Wakala umefanikiwa
kujenga kituo cha mizani cha Kurasini ambacho kimejengwa kwa ajili ya kuhakiki uzito
wa magari yanayotoka bandarini na kuweka CCTV Kamera katika mzani huo.
Kwandikwa, ameongeza
kuwa Wakala umeendelea na kazi za ujenzi na ukarabati
wa miradi mbalimbali ya viwanja vya ndege ambapo hatua za utekelezaji
zilizofikiwa kwa baadhi ya miradi
zinaridhisha.
Amesema kuwa hadi
kufikia Juni, 2019 ujenzi wa Jengo la abiria katika Kiwanja cha ndege wa Songwe
umefika asilimia 77 na ukarabati na ujenzi wa Jengo la kuongozea ndege na
mizigo katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza umefika asilimia 93.
"Sisi kama
Serikali tutaendelea kuboresha viwanja vingine vya ndege, tunajua wananchi
wanahitaji maendeleo kupitia sekta ya anga, hivyo hatuna budi kuboresha viwanja
hivi, amesisitiza Kwandikwa.
Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Miundombinu imepokea taarifa ya TANROADS ambayo imeainisha majukumu ya
Wakala huo kwa mwaka wa Fedha 2018/19 na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa barabara kuu, barabara za mikoa,
madaraja na viwanja vya ndege.
No comments:
Post a Comment