WAZIRI MHAGAMA: SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA DINI KUJENGA USTAWI WA TAIFA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 26 July 2019

WAZIRI MHAGAMA: SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA DINI KUJENGA USTAWI WA TAIFA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb), akieleza umuhimu wa Taasisi za dini katika kujenga ustawi wa Taifa, wakati wa Kongamano la Maombi ya Wanawake Waombolezao, tarehe 25 Julai, 2019, jijini Dar es salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akimkabidhi sadaka Mratibu wa  Kongamano la Maombi ya Wanawake Waombolezao Mchungaji  Deborah Malassy, wakati wa Kongamano hilo, tarehe 25 Julai, 2019,  jijini Dar es salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akifanyiwa maombi maalumu na waratibu wa Kongamano la Maombi ya Wanawake Waombolezao, wakati wa Kongamano hilo, tarehe 25 Julai, 2019,  jijini Dar es salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb) (katikati), akicheza moja ya nyimbo za kwaya,  wakati wa Kongamano la Maombi ya Wanawake Waombolezao, tarehe 25 Julai, 2019,  jijini Dar es salaam.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb), ameeleza kuwa serikali inatambua juhudi za taasisi za dini hapa nchini ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na utulivu, hivyo itaendelea kushirikiana na taasisi hizo katika kuunga juhudi za serkali za kujenga amani, umoja, upendo na mshikamano  na hatimaye  kuleta ustawi wa Taifa.  

“Napenda kuwahakikishia ushirikiano wa serikali katika kutekeleza majukumu yenu ya kiroho na ya huduma za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya watanzania. Pale mtakapoona mchango wa serikali unahitajika msisite kuwasiliana nasi. Na iwapo mtaona kuna upungufu wowote semeni kwa viongozi wa wilaya, mkoa na wa kitaifa. Sisi ni wasikivu. Tuite tutawaitikia, tutatenda kwa lile ambalo lipo ndani ya uwezo wetu” amesisitiza Mhe. Mhagama.

Akiongea kwa niaba ya Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, katika Kongamano la maombi ya wanawake waombolezao, jijini Dar es salaam, tarehe 25 Julai, 2019, Mhe. Waziri Mhagama amefafanua kuwa waratibu wa Kongamano hilo wanapongezwa na viongozi wote serikalini,  akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwakuwa linachagiza maendeleo katika Taifa hili na ustawi wa watu wake.

“Viongozi wetu kwa pamoja ni shupavu, wanaoaminiwa na kutumainiwa na wananchi hasa wanyonge. Viongozi wanachukia na kupinga rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwa vitendo na Rais anayejipambanua kwa kufanya maamuzi magumu ya kulinda rasilimali za Taifa. Lakini haya yote yamewezekana kwa kuwa wamejikabidhi katika mikono ya Mungu na nyie mmekuwa mkiwaombea” amesema Mhe. Mhagama.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mhagama amewataka Wanawawake waombolezao waendelee kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambazo anaendelea kuzifanya tangu aliposhika hatamu ya uongozi,  kwa kuthubutu kutenda  na kuiletea nchi mafanikio makubwa.

“Kwa uchache kazi kubwa ambazo amezitekeleza Mhe. Rais, ni pamoja na kutoa elimu ya msingi bila malipo ambapo ameweza kuwagusa hata walewasiojiweza, kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi na kujenga Hospitali na Vituo vya Afya vingi  ili watanzania wengi wapate huduma za Afya kwa karibu. Pia umeme kwa sasa umesambazwa vijijini kupitia mradi wa REA na sasa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Maji (Rufiji) umeanzishwa” amesisitiza Mhagama.

Awali wakiongea  katika Kongamano hilo, waratibu wa Kongamano hilo, Mchungaji Deborah Malassy na Askofu Dkt. Godfrey Malassy wamebainisha kuwa wameamua kuendesha Kongamano hilo kwa kuwa wanatambua kuwa viongozi wa dini kama walivyo wa serikali wanao wajibu  maalamu wa kulilea Taifa. Aidha wameongeza kuwa ushirikiano ukiwa imara watafanikiwa kuendeleza amani, umoja na mshikamano uliopo hapa nchini.

“Tutaendelea kutekeleza wajibu pekee wa kujenga uhai wa Taifa letu na watu wake. Tunampongeza Mhe.Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake bora uliokidhi kiu na kilio cha watanzania kwani tumeona jitihada anazofanya pamoja  na kutiwa moyo na kazi zake anazozifanya  na viongozi wote wa serikali ya awamu ya tano. Kwa hamasa hii tunapata nguvu ya kuendelea na wajibu huu mkubwa tuliopewa na Mungu kwa ajili ya kuendelea kuliombea Taifa letu” amesema, Mchungaji Deborah.

Kongamano hilo la kumi la Kihistoria hapa nchini liliohusisha Wanawake Waombolezao Kitaifa kutoka mikoa yote Tanzania  na Zanzibar, pamoja na viongozi wa Taasisi mbalimbali, limebebwa  na maudhui ya  Mwaka wa Maachilio kwa Wanawake wote. Kongamano hilo ni sehemu ya Maombi ya kila mwisho wa mwaka wa tarehe 31 Disemba ya kuliombea Taifa hili yajulikanayo kama MKESHA MKUBWA KITAIFA DUA MAALUM, ambayo yamekuwa yakifanyika katika viwanja vya wazi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Zanzibar.

No comments:

Post a Comment