Makamu wa Mkuu wa Chuo
hicho Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu akiongea na waandishi wa habari (hawapo
pichani) jijini Mwanza kuhusu uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 kuelekea
miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) utakaofanyika
Julai, 2 mwaka huu jijini Mwanza ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin. Kulia ni Mratibu wa Kamati ya
Habari-Maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya miaka 20/25 ya chuo cha SAUT, Padre
Titus Ngapemba na Rais wa Serikali ya wanachuo Elian Rodrick (kushoto).
Na Eleuteri Mangi- SAUT
RAIS Mstaafu wa
Serikali ya Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa anatarajiwa
kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 kuelekea miaka 25 tangu
kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT).
Kwa mujibu wa Makamu wa
Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu amesema kuwa chuo
kimemualika Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kwa kutambua na
kuthamini mchango wake katika elimu ya juu ambapo uzinduzi wa maadhimisho hayo unatarajiwa
kufanyika chuoni hapo Julai, 2 mwaka huu jijini Mwanza.
Akiongea na waandishi
wa habari leo chuoni hapo makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof. Mahalu amesema
kuwa yapo mafanikio mengi ambayo chuo kinajivunia tangu kuanzishwa kwake mwaka
1998. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka udahili wa wanafunzi
kutoka wanafunzi 204 hadi wanafunzi 11400 kwa mwaka wa masomo 2018/2019 licha
ya kwamba katika mwaka wa masomo 2012/2013 udahili uliwahi kufikia wanafunzi
13121 kabla ya kuongezeka kwa matawi 13 ya chuo hicho.
“Katika mtaala wa chuo,
wanafunzi wanapata fursa ya kusoma masomo ya ujasiriamali na kujiajiri baada ya
kuhitimu masomo yao na hivyo kuondokana na dhana ya kungoja kuajiriwa. Chuo
kimeboresha kiwango cha elimu inayotolewa
kuhakikisha wahitimu wanahimili
soko la ushindani Afrika Mashariki na duniani
kote pia kutokana na elimu ya dini na maadili kwa wanafunzi
wote.” Amesema Balozi Prof. Mahalu.
Katika kuunga mkono
juhudi za Serikali, Balozi Prof. Mahalu amesema kuwa chuo kimefanikiwa
kuanzisha kituo cha kuzalisha na kuwawezesha wajasiriamali ambapo wanafunzi
wanaohitimu masomo yao wanapata fursa ya kuandika mawazo ya biashara na baada
ya mawazo yao kukubalika hupatiwa mafunzo maalumu juu ya mawazo hayo na kisha
wanapatiwa mtaji kati ya shilingi milioni 25 hadi 30 kwa ajili ya kuendeleza
shughuli zao za ujasiriamali.
Aidha, chuo hicho kimefanikiwa
kuongeza vitivo vingine vinne (4) kutoka kitivo kimoja ambacho kilikuwa cha
Sayansi ya Jamii na Mawasiliano kilichokuwa na shahada moja ya Mawasiliano ya
Umma na kuongezeka kwa Kitivo cha Biashara na Utawala, Kitivo cha Ualimu,
Kitivo cha Sheria na Kitivo cha Uhandisi.
Zaidi ya hayo Balozi
Prof. Mahalu amesema chuo cha SAUT kina mchango mkubwa katika kutoa wanataaluma
na wataalam katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wahadhiri, Wanahabari, Wanasheria,
Wasimamizi katika taasisi za Fedha na Wakaguzi wa Fedha, Walimu, Wahandisi,
Wafanyabiashara, Watunza amani katika majeshi ya Ulinzi na Usalama pamoja na
Wanasiasa. Miongoni mwa wahitimu hao ni Mhe. Dotto Biteko Waziri wa Madini, Msemaji
Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, Zawadi Machibya na Sammy Awami ambao ni watangazaji
wa BBC, pamoja na wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi ndani na nje ya nchi.
Chuo cha SAUT nje ya
taaluma pia kinatoa huduma kwa jamii ambapo kimefanikiwa kuanzisha mradi mkuwa
wa umeme wa kutumia nishati ya jua kwa kushirikiana na nchi ya Ujerumani ambapo
mradi huo unatekelezwa katika vijiji mbalimbali katika mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Kagera na Geita.
Naye Mratibu wa Kamati
ya Habari-Maandalizi ya kuelekea miaka 20/25 ya chuo cha SAUT Padre Titus
Ngapemba amesema kuwa Rais Mtaafu Benjamin Mkapa amekuwa mdau muhimu katika
sekta ya Elimu nchini katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Padre Ngapemba amesema
kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa amekuwa mdau muhimu katika sekta ya elimu
nchini na kwa namna ya pekee katika chuo cha SAUT, akiwa madarakani
alifanikisha ujenzi wa barabara ya kutoka jijini Mwanza kuingia chuoni hapo
ambapo ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ulianza mwaka 2002 na
kuzinduliwa mwaka 2004.”
“Mzee Mkapa anakumbukwa
sana kwa kuwa mwasisi wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa vyuo
vyote vya umma na binafsi. Uamuzi huu wa Mzee Mkapa wa kuwapatia mikopo
wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi umesaidia Watanzania wengi kusoma elimu ya juu.
Kwa hili utakumbukwa Mzee Mkapa” alisisitiza
Padre Ngapemba.
Padre Ngapemba
aliendelea kusema “Kwa mara ya kwanza mwaka 2005 Serikali ya Awamu ya Tatu
ilibadilisha Sera ya mikopo ya elimu ya juu na kuanza kutoa mikopo kwa vyuo
vikuu binafsi ikiwemo SAUT baada Makamu wa
Mkuu wa chuo wa wakati huo Padre Deogratius Rweyengeza kutoa ombi hilo wakati
wa mahafali ya kwanza mwaka 2001 tangu kipandishwe hadhi.”
Chuo Kikuu cha SAUT
kinamilikiwa na kusimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kimeanzishwa
kwa mujibu wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya vyuo vikuu
Tanzania (TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka
2005 ambapo awali kilikuwa kinajulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Nyegezi (NSTI) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na wamisionari wa kanisa
katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika wakiwa chini ya
Askofu Mkuu Joseph Blomjous wa Jimbo Kuu
la Mwanza.
|
No comments:
Post a Comment