| Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Bw. Filbert Mponzi akizungumza wakati wa futari iliyoandaliwa na NMB na kufanyika katika Hotel ya Mabinat Al Bahr Mbweni Zanzibar. |
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuimarisha ulinzi, usalama na mazingira mazuri ya kazi, kwa mabenki ili yaweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Mohamed Ramia wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu na wateja wa Benki ya NMB, katika futari maalum iliyoandaliwa na NMB iliyofanyika katika Hotel ya Mabinat Al Bahr Mbweni visiwani Zanzibar.
Alisema kitendo cha Benki ya NMB na benki nyingine kufungua matawi Zanzibar kwa kiasi kikubwa kimeongeza kasi ya ukuaji uchumi wa Zanzibar jambo ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaliunga mkono.
Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameipongeza Benki ya NMB kwa kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo serikali itaendelea kuiunga mkono kwani wananchi wengi wa Zanzibar wanaridhika na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
Aidha liupongeza uongozi wa benki kwa kuandaa futari hiyo ambayo imewaweka pamoja wateja na viongozi wao na kuwataka kuendelea kufanya hivyo kila mwaka, hasa ikizingatiwa kuwa jambo hilo ni jema kwa waamini wa Kiislamu kwenye mwezi mtukufu wa ramadhani.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Miundombinu na Usafirishaji, Mohamed Ahmada ameipongeza benki hiyo kwa juhudi zake kubwa inazozifanya za kutoa huduma bora kwa wateja wake, pamoja na kuwaweka pamoja wateja wao kwa kuwaandalia futari kila mwaka.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Filbert Mponzi akizungumza alibainisha benki hiyo hivi sasa ipo katika muendelezo wa kutoa huduma bora kwa wateja, ili kuhakikisha inapiga hatua kubwa kufikia malengo yake.
Alisema kuwa katika kufanikisha hilo hivi sasa inatoa huduma mbalimbali kupitia mitandao ikiwemo simu hadi kwa watu wanaoishi vijijini, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limerahisisha huduma kwa wateja wengi, ikiwemo ufungaji mashine za ATM na mawakala.

No comments:
Post a Comment