MCHUNGAJI ATAKA TUIOMBEE ‘HAKI’ ILI AMANI IPATIKANE…! - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 28 May 2019

MCHUNGAJI ATAKA TUIOMBEE ‘HAKI’ ILI AMANI IPATIKANE…!

Mch. Nuru Aron, akihubiri siku mbili mfululizo.

Na Adam Mwambapa, Tunduru
AKIWA kwenye ziara ya Uinjilisti Jumapili iliyopita, ziara iliyoandaliwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu Teofilo Kisanji (TEKU) Kitivo cha Theologia. Chuo kilichopo jijini Mbeya, kwa kushirikiana na Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (KIUMA).
Kanisa lililopo Kijiji cha Milonde, Kata ya Milonde, Tarafa ya Matemanga, wilayani Tunduru na mkoa wa Ruvuma. Mch. Lawi Afwilile Mwankuga, aliitaka jamii iombee sana ‘haki’ kabla ya kuiombea amani.
Mch. Mwankuga, aliyaongea hayo mara baada ya mkutano wa nje kumalizika, uliofanyika katika Kijiji cha Kalulu wilayani humo wenye lengo la kuwarejeshea watu Uhuru wao uliotekwa na ufalme wa shetani.
Siku mbili za mlipuko wa injili katika viwanja vya Shule ya Ufundi ya KIUMA, zilitosha kabisa kuwarejesha walio wengi kwenye mstari wa kumjua Mungu ambao awali waliporwa haki zao na ibilisi akiwatumikisha.
Akihubiri kwa siku mbili mfululizo kwenye viwanja hivyo, Mchungaji Nuru Aron, alisema mara zote ibilisi amefanya mambo ya kikatili kwa kuwaangusha watu wa Mungu na kupora ‘haki’ zao kinguvu akiwatumikisha kwenye matendo yasiyofaa.
“Kuwa na maisha magumu na kushindwa kujimudu, kukosa hata lishe bora kwa kutopata milo mitatu, yote hiyo ni kazi ya ibilisi. Kwa kuwa, amepora haki za watu bila wao kujua, na amewatumikisha kupitilizana. Kwa njia hiyo wamekosa tunu zao alizowaandalia Mungu, kwa ajili yao na vizazi vyao.”
“Ni wakati wa kila mmoja kujikagua na kuzirekebisha njia zake, ili amgeukie Mungu na maisha yake yapate kuwa salama na yenye heri,”alisema Mch. Aron.

Baadhi ya vijana na watu mbalimbali waliokata shauri kwenye mkutano huo.
Ndipo naye Mchungaji Mwankuga alipoitaka jamii kukazana sana kuiombea ‘haki’ ndani ya nchi, akisema kwa kukazana kuiombea ‘haki’ ndipo amani nayo itapatikana bila shaka.
Akisisitiza na kuweka mkazo kwenye kile anachokiamini, Mwankuga alisema kuiombea amani pasipo kutanguliza kuiombea haki kwanza, bado hatutendi sawasawa.
“Ni vema sasa hivi watu wakazane sana kuiombea haki, ikiwa haki itatendeka kama inavyotakiwa basi amani ni rahisi sana kupatikana kwa kuwa haki itakuwa ipo,” alisema Mch. Mwankuga na kuongeza:
“Mungu anatutaka sana watu wake tuisimamie na kuitenda haki kikamilifu, sawasawa na Neno lake kwetu lisemalo, [Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote. MITHALI 14:34]”
Aidha, kwa kuzidi kufafanua jinsi haki inavyothaminiwa na kuongelewa kwa mapana kwenye Maandiko Mtakatifu…Mchungaji huyo, alinukuu baadhi ya vifungu vifuatavyo:
‘Ataitokeza haki yako kama nuru, Na hukumu yako kama adhuhuri .‘ (ZABURI 37:6).
‘Mungu wa Israeli alisema, Mwamba wa Israeli aliniambia, Atawalaye wanadamu kwa haki, akitawala katika kicho cha Mungu, Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo, asubuhi isiyo na mawingu…’ (2 SAMWELI 23:3-4).

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Na kwa kuzidi kuwekea uzito wa namna haki inavyotakiwa itendeke na kuonekana imetendeka, naye Mchungaji Ernest Simpanzye, alisema haki ni suluhisho la matatizo na mitafaruku mingi katika jamii yoyote.
“Katika Biblia Takatifu kitabu cha MITHALI 29:2,7 Mungu anasema, Wenye haki wakiwa na amri watu hufurahi; bali mwovu atawalapo, watu huugua.  Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini; Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue,”alimaliza Mch. Simpanzye.
Imezoeleka hivi sasa kutamkwa na viongozi wengi wa taifa hili, na hata wale wa Madhehebu pamoja na Makanisa mbalimbali…wakiwasihi sana na kuwataka sana wananchi  huku wakiwasisitiza waiombee amani, ili kuipusha nchi yetu kuingia katika machafuko.
Hata kumekuwako na mikesha sehemu tofauti tofauti. Iwe kwenye Makanisa au pengine Misikitini, lengo likiwa ni kuhimiza jamii izidi kuiombea amani nchi.
Akizidi kulisisitiza jambo la kuiombea haki, Mchungaji Veronica Kafwila (Mtheolojia), alisema Haki ndiyo msingi wa mafanikio kwa kila jambo mbele ya Mungu.
“Tumekuja Tunduru kwa lengo la kuinjilisha watu wa Mungu waghairi njia zao mbaya zisizofaa, na wamgeukie Mungu ili maasi, magomvi, magonjwa, njaa na dhiki kuu visipate katika maisha yetu ya kila siku.”
“Lakini pia watu waipate haki yao kikamilifu waliyoahidiwa na Mungu. Ndipo jamii nzima itamuita Mungu naye atasikia na kuitika,”alisema Mchungaji huyo mwanafunzi.
Sambamba na wito huo wa Wachungaji hao wa TEKU, waliokuwa kwenye msafara wa ziara hiyo wapatao 30, wakiomba na kuihubiri haki itendeke hapa nchini.
Kama taifa baada ya miezi michache kuanzia sasa yaani mapema Oktoba mwaka huu, taifa letu litaingia kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa. Pia Oktoba 25 mwakani, utakuwa ni uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni kipindi mujarabu, ambacho jamii inatakiwa kuwapata viongozi waadilifu, wachapakazi, majasiri, wazalendo kwa taifa lao na nchi kiujumla wenye uwezo wa kutenda haki kwa jamii inayowazunguka.
Kwa muktadha huo, ni kipindi muhimu sana na kinachohitaji umakini mkubwa sana kwa wapigakura, na hasa kwa wale waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi na kutangaza matokeo ya washindi.

Wachungaji, Sultan (Mwenye) na wengine wakifuatilia mahubiri,

Ndicho kipindi kinachohitajika sana haki kutendeka, na si tu haki kutendeka ila ionekane imetendeka ili kuichuchumilia amani inayohubiriwa na wengi.
Hasa tukiangalia jinsi matukio ya uvunjifu wa haki na amani yalivyokithiri kila pande hapa nchini kiasi cha kutishia usalama wa wengi; kwa kuliletea taifa sifa mbaya.
Kupotea kwa baadhi ya Watanzania wenzetu na watu wasiojulikana (ikidaiwa wametekwa), matukio ya watoto kufanyiwa vitendo  viovu na vya kikatili vyenye sura ya kinyama yaliyoshamiri kwa imani za kishirikina; kwa lengo la baadhi ya wasio na nia njema kujipatia mali.
Ikiwemo kuwaua na kuwafanyia vitendo viovu walemavu wa ngozi (albinism) na mengineyo. Ni baadhi tu ya matendo yanayohitaji tumwombe sana Mungu, awasaidie wenye mamlaka ya kutoa haki hapa nchini nao waitoe haki bila upendeleo.
Nje na hapo amani haitakuwa na tafsiri nyingine zaidi ya upole tu na si vinginevyo. Na zaidi sana tafsiri yake yaweza kuwa ni ukimya...kwa sababu upole na ukimya si tafsiri ya amani.
Mungu Ibariki Tanzania!
0765 937 378


No comments:

Post a Comment