Shimo
ambalo linatumika kwa sasa kuteketeza taka za Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, mara
baada ya mtambo maalumu wa kutetekeza taka hizo kuwa katika hatua za ukarabati.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Paul
Lawala kuja na Mkakati wa haraka wa kupata mtambo mpya (Incinerator) ya
kuteketeza taka hatarishi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. Mussa Sima (wa pili kutoka kushoto) akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya
Rufaa ya Kanda ya Mbeya Dkt. Paul
Lawala mara baada ya Mhe. Sima kutembelea Hospitali hiyo kukagua namna taka
ngumu na hata hatarishi zinavyo teketezwa.
Katika
ziara yake Mkoani Mbeya yenye lengo la kukagua
maeneo yenye changamoto za kimazingira katika sekta ya afya na namna ya
uteketezaji wa taka pamoja na kuzitafutia ufumbuzi Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa
Sima ameshuhudia kukosekana kwa mtambo
maalumu wa kuteketeza taka Hospitalini hapo na uteketezaji wa taka kufanyika
katika shimo ambalo si salama kiafya na kimazingira.
“Nimeshuhudia Hospitali ya Rufaa ya Mbeya haina Incinerator, taka hatarishi zinachomwa
kwenye shimo bila tahadhari yoyoye, kuna madhara makubwa zaidi ya uchomaji wa
taka katika eneo hilo. Kama hatua za haraka nimeagiza taka hizo ziteketezwe
katika burning chambers na waanze
kuweka mkakati wa kupata incinerator
itakayokidhi mahitaji” Sima alisisitiza.
Waziri Sima amesema uchomaji wa taka hususan taka
hatarishi bila kuzingatia taratibu madhara yake ni makubwa hasa kwa jamii inayozunguka,
ukizingatia hospitali hiyo inapakana na Shule ya Sekondari ya Loleza.
Ameelekeza kusitishwa kwa uchomaji taka wa aina hiyo na badala yake uongozi wa
Hospitali hiyo utumie kiteketezi taka maalumu “burning chambers” kama mkakati
wa haraka ili kunusuru afya za watu na mazingira.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mussa Sima
ameshuhudia kiasi kikubwa cha taka ngumu ambazo hazijazolewa hospitalini hapo
kwa kipindi kirefu na kusababisha hofu ya mlipuko wa magonjwa. Katika kutatua
changamoto hii Naibu Waziri Sima ameagiza Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya na
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kukaa pamoja na kuweka mkakati endelevu
wa kuhakikisha taka zinaondolewa kwa wakati Hospitalini hapo.
Alipoulizwa
juu ya hali hiyo Kaimu
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda – Mbeya Dkt. Paul Lawala amekiri kuwa Hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto
ya uzoaji taka kwa wakati na kuainisha kuwa changamoto hizo zinafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja kuanza kwa ukarabati wa ‘burning chamber’ na
mkakati wa kupata mtambo maalumu wa kuteketeza taka utakaokidhi mahitaji halisi.
No comments:
Post a Comment