Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akizindua zoezi la
upandaji miti katika mji wa Serikali Dodoma. Miti 800 aina ya “midodoma” imepandwa katika eneo hilo
na miti 200 ya aina nyingine pia imepandwa ikiwa ni mkakati wa Serikali wa
kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. Kulia ni Bw. Timothy Mande Afisa Misitu kutoka
Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akipata maelezo ya
maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu
wa Rais katika Mji wa Serikali kutoka kwa Mhandisi Simeo Machibya ambae ni
Meneja Msimamizi wa Mradi kutoka Vikosi vya Ujenzi. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Rais Mhandisi Joseph Malongo na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph
Sokoine.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.
January Makamba hii leo ameongoza watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais
kupanda miti zaidi ya elfu moja (1000) katika eneo la Mji wa Serikali,
inapojengwa Ofisi ya Makamu wa Rais.
Waziri Makamba amesisitiza
kuwa zoezi hilo ni endelevu na takribani miti 1000 ya aina ya mdodoma
inayostahimili ukame imepandwa hii leo. “Sisi ni watu wa Mazingira, ni lazima
tuonyeshe mfano, hapa kila mtumishi atakuwa na wajibu wa kutunza miti
atakayokabidhiwa na kuhakikisha inakua” Makamba alisisitiza.
Waziri Makamba amesema
kuwa Jiji la Dodoma linakabiliwa na changamoto ya mandhari kutokana na ardhi
yake kuwa kame na kupelekea uoto wa asili kupungua kwa kiasi kikubwa. Hivyo,
ametoa wito kwa kila taasisi na Idara kuunga mkono kwa vitendo kampeni
iliyozinduliwa na Mhe. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan Novemba 2017 ya
kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, kwa kupanda miti kwa wingi katika Mji wa
Serikali na Dodoma kwa ujumla ili uwe mji wa mfano kwa kuwa na mandhari yakuvutia.
“Kwa kuwa sisi ndio
wasimamizi wa Mazingira, upandaji na usimamizi wa miti ni sehemu ya Hifadhi ya Mazingira,
hivyo lengo la Ofisi yetu ni kuonyesha mfano, watumishi wote kuanzia Waziri
mpaka Mhudumu kila mmoja atakuwa na miti yake ya kutunza na kuhakikisha inakua”
Makamba alisisitiza.
Awali Waziri Makamba alipata
fursa ya kutembelea eneo inapojengwa Ofisi ya Makamu wa Rais na kuridhishwa na
kasi ya ujenzi katika eneo hilo na kumtaka Mkandarasi wa Mradi kutoka (Vikosi
vya Ujenzi) Mhandisi Simeo Machibya kukamilisha kazi yote kwa wakati. “Ujenzi
huu ufanyike usiku na mchana” Makamba alisisitiza.
Katika zoezi la leo Waziri
Makamba ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph
Malongo, Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine pamoja na Wakuu wa Idara na
Vitengo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment