NA LUSUNGU HELELA
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii linalojengwa ndani ya mji wa Serikali katika eneo la Ihumwa Jijini Dodoma.
Ameyabainisha hayo wakati alipotembelea eneo hilo kwa ajili ya kukagua maendeleo yaliyofikiwa katika ujenzi wa jengo hilo.
“Kazi hii inafanywa kwa uhodari mkubwa, nawapongeza kwa maendeleo yaliyofikiwa na ninaamini kwamba Jengo hili litakamilika ndani ya muda uliopangwa’’
Aidha, Mhe. Kanyasu wakati alipotembelea eneo hilo ameweza kukutana na timu ya Wakadiliaji Majengo kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao kwa pamoja na Fundi Sanifu Ujenzi, Agastoni Kayugwa ambaye ni Muwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa pamoja wameeleza kuwa wanaridhishwa na spidi inayoendelea katika ujenzi wa jengo hilo.
Kwa upande wake, Mkandarasi wa SUMA JKT, Luteni Mturi amemueleza Naibu waziri huyo kuwa wanatarajia kumaliza ndani ya muda uliopangwa kwa vile kwa sasa kuna upatikanaji wa uhakika wa vifaa vya ujenzi ikiwematofali ya kutosha na yenye ubora wa hali ya juu pamoja na wafanyakazi wa kutosha
‘’Kesho tunategemea kuanza kumwaga zege katika kipande cha kwanza ambapo hadi kesho kutwa tutamalizia kipande cha pili’ ameeleza Mturi.
Hata hivyo, Mkandarasi huyo ameeleza changamoto ya utayari wa wafanyakazi kufanya kazi usiku kuwa wengi wao wamekuwa hawapo tayari kufanya kazi muda huo licha ya kuwa awali SUMA JKT ilipanga kujenga jengo hilo mchana na usiku.
No comments:
Post a Comment