MAWAKALA wa T PESA sasa watakuwa wakihudumiwa na Benki ya TPB kwa huduma zote za kifedha ikiwemo kununua Floats za T Pesa kutoka katika Matawi yote 76 ya TPB yaliyopo mikoa na wilaya mbalimbali nchini.
Makubaliano hayo kati ya T PESA, kampuni tanzu ya TTCL Corporation na Benki ya TPB yamesainiwa leo jijini Dar es Salaam ambapo Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya TPB, Bw. Sabasaba Moshingi na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Waziri Kindamba wamesaini mikataba ya ushirikiano huo.
Akizungumzia tukio hilo, Bw. Kindamba alisema kupitia makubaliano hayo taasisi zote zitanufaika kila mmoja kwa namna yake huku lengo letu kuu la kutoa huduma bora kwa Wananchi likitimia kwa kiasi kikubwa.
"...Kupitia makubaliano haya, Benki ya TPB itatoa huduma za kifedha kwa Mawakala wa T PESA ambao sasa wataweza kununua Floats za T Pesa kutoka katika Matawi yote 76 ya TPB yaliyopo katika Mikoa na Wilaya za Nchi yetu. Pamoja na fursa hii, Benki ya TPB inaendelea kuhudumiwa na Shirika la TTCL kwa huduma za Data, Simu za mezani, simu za Mkononi na Trust Account.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya TPB, Bw. Sabasaba Moshingi alisema Faida za ushirikiano huu ni nyingi lakini muhimu zaidi ni kuwawezesha Wananchi na hasa Wafanyabiashara wanaotoa huduma za Mawasiliano na Fedha Mtandao kuweza kufanya shughuli zao kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
Benki ya TPB tutaendelea kushirikiana na TTCL ambao ni ndugu zetu kihistoria. Tunafanya mambo mengi kwa pamoja na tunafurahia ushirikiano uliopo kati yetu hasa kwa kuwa taasisi hizi mbili za Umma zina lengo kuu moja la kuwahudumia mwananchi.
Picha ya pamoja mara baada ya kusaini makubaliano hayo ya kibiashara. |
No comments:
Post a Comment