Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile (mbele) akiyaangalia mabenchi hayo maraa baada ya kupokelewa. |
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabenchi 52 yenye thamani ya shilingi milioni 10 ambayo yatatumika kukalia kwenye eneo maalum la kupumzikia ndugu waliopeleka wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi mabenchi hayo jana, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Badru Idd alisema benki hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.
Alisema Serikali inafanya mengi na makubwa katika kuboresha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya maeneo mbalimbali nchini, hivyo NMB kwa kutambua umuhimu wa afya itaendelea kuchangia.
Alisema msaada waliokabidhi wameutoa baada ya uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuiomba NMB isaidie mabenchi ili ndugu wanaokuja kupata huduma eneo hilo wapate hifadhi nzuri wanaposubiri kuhudumiwa.
"...NMB tumeamua kushirikiana na Hospitali ya Muhimbili pamoja na jamii yote inayozunguka hospitali hii kwa kuchangia jumla ya mabenchi 52 imara kwa ajili ya kukalia ndugu na wagonjwa wa hospitali hii kubwa ya Muhimbili, yote yakiwa na thamani ya milioni 10," alisema Bw. Idd.
Aidha Idd aliongeza kuwa kwa mwaka 2018, NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia sekta ya afya na Elimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile akipokea msaada huo aliishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kutatua changamoto za afya na kuwaomba waendelee na moyo huo.
Alibainisha ili kuboresha sekta ya afya Serikali ya awamu ya tano, imetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kununua madawa na inajenga hospitali 63 za Wilaya maeneo mbalimbali kwa sasa, hivyo kuwaomba sekta binafsi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa namna anuai.
Sehemu ya msaada uliokabidhiwa. |
No comments:
Post a Comment