TMS YAJIZATITI KUTEKELEZA MFUMO WA TAIFA WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 22 November 2018

TMS YAJIZATITI KUTEKELEZA MFUMO WA TAIFA WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA

Picha ya pamoja ya sehemu ya washiriki Mkutano wa Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa Tanzania (Tanzanian Meteorological Society (TMS).

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) alifungua Mkutano wa Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa Tanzania (Tanzanian Meteorological Society (TMS) kilichofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza na kuhudhuriwa na wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Wakati akifungua mkutano huo, Dk. Kijazi  aliwapongeza TMS kwa nia waliyoionesha ya kuhakikisha wanaweka msisitizo wa utekelezaji wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa uliozinduliwa tarehe 21 Agosti 2018.

"..Napenda kuwapongeza na nimefarijika kusikia kuwa mipango mikakati ya utekelezaji wa majukumu ya TMS imelenga na inaenda sambamba na utekelezaji wa malengo/madhumuni ya Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa, hii ni hatua nzuri kwa fani ya hali ya hewa na TMS pia," alisema Dk. Kijazi.

Katika hatua nyingine, Dk. Buruhani Nyenzi, ambaye ni Rais wa TMS alieleza kuwa mojawapo ya kipaumbele cha TMS ni kuhamasisha utekelezaji wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa, ambao una umuhimu wake katika shughuli mbalimbali zinazohusisha hali ya hewa na  maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Lengo kuu la mkutano ilikuwa kujadili mpango mkakati wa TMS na namna ya kuendeleza jitihada za utekelezaji (matumizi) wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa kwa manufaa ya wanachama na sekta ya hali ya hewa kwa ujumla..

Mkutano huo umedhaminiwa na Programu ya Kidunia ya Huduma za Hali ya Hewa, awamu ya pili (Global Framework for Climate Services Adaption Programme in Africa (GFCS APA)- Phase II)  kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) chini shirika la misaada la Norway (Norwegian Agency for Development Cooperation (NORAD)).
 
Imetolewa:
Monica Mutoni,
Ofisi ya Uhusiano,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)

No comments:

Post a Comment