Muonekano wa daraja la mto Mara lenye urefu wa mita
94 na barabara ya maungio ambayo ni sehemu ya barabara ya Tarime-Mugumu ambayo
ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea.
|
Sehema ya chini ya daraja la mto Mara lenye urefu
wa mita 94, mto Mara unaoanzia katika kijiji cha Masai Mara nchini Kenya maji
yake huelekea na kuishia Ziwa Victoria upande wa Tanzania.
|
NAIBU Waziri wa Ujenzi
Mheshimiwa Elias John Kwandikwa ameutaka
muungano wa Makampuni mawili ya kizalendo ya M/S Gemen Engineering Construction
Co. Ltd na Mayanga Constractors Co. Ltd yanayojenga daraja la mto Mara kukamilisha
ujenzi huo Januari mwakani.
Amesema Serikali haitawaongezea
muda katika kazi hiyo hivyo wahakikishe daraja hilo pamoja na barabara za
maingilio zinakamilika kwa wakati na ubora unaostahili.
“Hakikisheni mnafanya kazi
kwa bidii na weledi ili Serikali izidi kuwaamini na kuwapa miradi mingi zaidi
wakandarasi wazawa na hivyo kukuza ujuzi na uchumi wa nchi”, amesema Mhe.
Kwandikwa.
Daraja la mto Mara
lenye urefu wa mita 94 ambalo linaunganisha Wilaya za Tarime na Serengeti ujenzi
wake unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 8.5 na ni miongoni mwa madaraja
mawili makubwa yanayopitiwa na mto Mara unaoanzia katika kijiji cha Masai Mara
nchini Kenya kuelekea Ziwa Victoria, daraja jingine ni Kirumi lenye urefu wa
mita 223.3 lililojengwa mwaka 1985.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri Kwandikwa amekagua kiwanja cha ndege cha Musoma na kusisitiza kuwa Serikali
itakijenga kiwanja hicho ili ndege nyingi zaidi ziweze kukitumia na kuhuisha
uchumi wa mkoa wa Mara.
Amesema ujenzi wake
ukikamilika utafungua uchumi wa mji wa Musoma na mkoa wa Mara kwa ujumla kwani
utavutia watalii wengi kufika katika vivutio vya mkoa huo ikiwemo hifadhi ya
Serengeti.
Naye Mkuu wa mkoa wa Mara
Bw, Adam Malima amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa kufunguka kwa
barabara, madaraja na uwanja wa ndege mkoani humo kutahuisha uchumi wa mkoa
huo.
Meneja wa kiwanja cha
ndege cha musoma bwana Shadrack Chilongani amesema kiwanja cha ndege hicho
ambacho kiko daraja la tatu C kina urefu wa mita 1,600 na upana wa mita 30 hivyo
uboreshaji wake utakapokamilika utakipandisha daraja na kukiwezesha kuongeza
miruko ya ndege na abiria na hivyo kukuza utalii wa mkoa wa Mara.
No comments:
Post a Comment