Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akizungumza na mamia
ya wakazi wa Mkoa wa Tabora (hawapo pichani) waliojitokeza katika Ukumbi wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kumsikiliza. Waziri Makamba amezindua Kamati ya
Mazingira na kuwataka wananchi hao kuwa mstari wa mbele kusimamia masuala ya
mazingira katika maeneo yao.
JAMII imetakiwa kufahamu
kuwa Kamati za Mazingira katika ngazi zote zipo kwa mujibu wa Sheria, Sheria ya
Mazingira kifungu Na. 38 (1-2) na Kamati hizo zina wajibu wa kusimamia
mazingira kikamilifu yanayohusu maeneo yao.
Akizungumza na Watendaji
wa Mkoa wa Tabora katika hafla ya kuzindua Kamati ya Usimamizi wa mazingira Mkoani
hapo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January
Makamba ameahidi kujenga uwezo kwa watendaji hao kwa kuwapatia mafunzo.
Aidha, Waziri Makamba
amesisitiza unaziswaji kwa Kamati za Mazingira katika ngazi za vitongoji,
vijiji na kata nchi nzima na kuahidi kutuma wataalamu kutoa mafunzo kwa kamati
hizo ili ziweze kujua majumu yao ipasavyo na kusema kuwa shughuli za hifadhi za
mazingira hazitafanikiwa kama Kamati za mazingira hazitatimiza majukumu yake
katika ngazi hizo.
Waziri Makamba amesema
kuwa dunia tunayoishi sasa tumeiazima kwa kizazi kinachokuja hivyo hatuna budi
kuitunza. “Ukiazima kitu kwa mtu yeyote huna budi kukitunza na kukulinda ila
kukirudisha kwa mwenyewe kikiwa katika hali nzuri.” Makamba alibainisha.
Katika wakati mwingine
Waziri Makamba ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Tabora kuteua ama kuajiri Maafisa
wa mazingira wa kutosha ili kusimamia kikamilifu uzingatiaji wa Sheria ya
Mazingira, pamoja na kuandaa mpango tekelezi wa mazingira katika ngazi ya Mkoa.
Kuhusu usimamizi wa taka,
Waziri Makamba ametoa wito kwa uongozi wa Mkoa wa Tabora na Halmashauri zote
kuwa na takwimu sahihi ya kiwango cha taka kinachozalishwa kwa siku ili taka
hizo ziweze kutumia katika uzalishaji wa nishati. “Naagiza kila Halmashauri
kufahamu kiwango cha uzalishaji wa taka, hii itasaidia kuja na miradi ya
kuzalisha nishati mbadala pale fursa zitakapopatikana.” Makamba alisisitiza.
Katika hatua nyingine
Waziri Makamba amesisitiza matumizi ya nishati mmbada kwa taasisi za Serikalini
ili kupunguza kiwango cha ukataji wa miti na matumizi ya mkaa, pia amewataka
wadau na wakulima wa tumbaku kubuni namna bora ya kuchoma tumbaku ili iweze
kupata soko zaidi duniani.
“Sote tunafahamu kuwa miti ni gharama, haiwezekani
mkulima kuteketeza kiasi cha miti yenye thamani ya Shilingi laki mbili
kuzalisha tumbaku ya elfu themanini, hii haikubaliki ni lazima tubadilishe
uchomaji wake”. Waziri Makamba amebainisha.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Bw. Aggrey Mwanri amemueleza Waziri Makamba jinsi Mkoa wake unavyotekeleza
kikamilifu kampeni ya upandaji miti kwa kuwa na kauli mbiu ya ‘Tabora ya
Kijani’ na amemshukuru Waziri Makamba
kwa kufanya ziara katika Mkoa wake na kuahidi kutekeleza agizo la kuteua maafisa
wenye sifa ya kuwa wakaguzi wa Mazingira.
Waziri Makamba
amehitimisha ziara yake Mkoani Tabora kwa kutembelea Bwawa la Igombe na Kazima
ili kuona utashi na utayari wa wananchi katika kuhifadhi maeneo hayo kabla ya
kutangazwa katika gazeti la Serikali kama eneo lindwa. Akiwa Kijijini Igambilo
Mheshimiwa Makamba ameahidi kutoa mifuko 100 ya Saruji kuchangia ujenzi wa
Zahanati kijijini hapo.

No comments:
Post a Comment