TPBA NA TLS WAINGIA MAKUBALIANO YA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KISHERIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 13 June 2025

TPBA NA TLS WAINGIA MAKUBALIANO YA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KISHERIA

 CHAMA  cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kimeingia makubaliano rasmi ya ushirikiano na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), yakilenga kuongeza mshikamano, weledi na ufanisi katika utekelezaji wa masuala ya sheria nchini.


Makubaliano hayo yamesainiwa leo jijini Dar es Salaam na viongozi wa vyama hivyo, mbele ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi, ambaye amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa makubaliano hayo kwa vitendo.

"Ni muhimu kuona haya makubaliano yakitekelezwa kwa manufaa ya pande zote mbili. Hili litasaidia kuimarisha mifumo ya sheria na utoaji wa haki nchini," amesema Dkt. Possi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa vyama husika, ushirikiano huo utahusisha maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo ya pamoja, kubadilishana uzoefu, na kufanya kazi kwa pamoja katika masuala ya kitaaluma na ya kitaifa.

Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwambukusi, amesema makubaliano hayo ni fursa adhimu kwa wanasheria wa pande zote kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kushirikiana katika kuijenga Tanzania yenye haki, amani na utulivu.

"Tunaamini kuwa kupitia ushirikiano huu, tutaimarisha taaluma ya sheria na kujenga taifa lenye mfumo wa haki unaoeleweka kwa wote," amesema Mwambukusi.

Naye Makamu wa Rais wa TPBA, Wakili Debora Mcharo, amesema makubaliano hayo yamekuja katika wakati muafaka ambapo kuna haja ya kuwa na jukwaa la pamoja la kushughulikia changamoto za kisheria nchini.

"Tunatambua nafasi ya kila upande katika kukuza misingi ya haki na utawala wa sheria. Ushirikiano huu utatupeleka mbali zaidi," amesema Mcharo.

Makubaliano haya yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya sheria kwa kuimarisha uhusiano kati ya mawakili wa serikali na wale wa upande binafsi, hali itakayosaidia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na matumizi bora ya taaluma ya sheria nchini.   

No comments:

Post a Comment