TANZANIA inashiriki mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali ulioanza leo tarehe 8 Agosti, 2024 katika ngazi ya Makatibu Wakuu jijini Harare, Zimbabwe, ambapo moja ya agenda itakayojadiliwa ni suala la gharama za kujumuisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC.
Itakumbukwa kuwa, katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika nchini Tanzania mwezi Agosti 2024 uliitambua Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi za Jumuiya hiyo. Lugha nyingine zinazotumika ni, kiingereza, kifaransa na kireno.
Mkutano huo unatarajiwa kufanya uteuzi wa Mwenyekiti wa SADC ambapo, Mhe. Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa SADC atateuliwa kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha 2024/2025. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti itajulikana kupitia Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2024.
Aidha, hafla ya ufunguzi wa mkutano huo imewezesha makabidhiano ya nafasi ya unyekekiti katika ngazi ya mkutano wa Makatibu Wakuu ambapo Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Balozi Nazaré José Salvador amekabidhi nafasi hiyo kwa mwenyekiti mpya, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbambwe, Balozi Albert Ranganai Chimbindi akisisitiza kumpa ushirikiano katika nafasi hiyo.
Naye Balozi Chimbindi amemshukuru Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Pia ameahidi kuzingatia ushauri aliokuwa akiutoa kwa Sekretariet ya SADC na kufanya kazi pamoja ili kuyafikia malengo ya jumuiya hiyo kwa maslahi jumuishi.
“Tumepiga hatu lakini bado tuna kila sababu ya kuweka bidii kwenye ujenzi wa miundombinu, usafiri na hatimaye tuweze kuifikia SADC tunayoitaka. Niwahakikishie kuwa Zimbabwe ipo tayari kufanya kazi pamoja nanyi kwa kufuata malengo, kanuni na mikataba ya SADC'', Balozi Chimbindi.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utafanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2024 na utatanguliwa na mikutano ya awali kwa ajili ya maandalizi ambayo ni: Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda kwa kipindi cha Agosti 2023 hadi Agosti 2024. Mkutano huu utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).
Mikutano mingine ni: Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Agosti 2024 pamoja; na Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 11 Agosti, 2024.
No comments:
Post a Comment