NA JOSEPHINE MAJULA, LINDI
SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imeombwa kusimamia upatikanaji wa fedha na utoaji wa mikopo ya Halmashauri inayotolewa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wa makundi maalumu ili kuhakikisha inawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.
Ombi hilo limetolewa wilayani Liwale mkoani Lindi na Mwenyekiti wa Kikundi cha Tunaweza, Bi. Diana Venant, baada ya kumalizika kwa semina ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha kupitia Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha ili waweze kuongeza mitaji ya biashara na kujikwamua kiuchumi.
“Serikali ikisimamia vizuri zoezi la utoaji mikopo kwa makundi yaliyokusudiwa itasaidia kupunguza tatizo la mikopo umiza ama kausha damu kwakuwa wananchi wengi wanakimbilia mikopo ya kausha damu kwa kuwa mikopo hiyo inapatikana kwa haraka bila kuwa na masharti mengi,’’ alisema Bi. Venant.
Aliongeza kuwa wananchi wengi hawana vigezo vya kwenda kukopa kwenye Taasisi rasmi za Fedha kwa kuwa wanahitajika kuwa na hati ya nyumba, hati ya kiwanja au kadi ya gari na kufanya wananchi hao kukosa sifa za kupata mikopo yenye riba ndogo ambayo inalipika kwa urahisi.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Vikundi vya Huduma Ndogo za Fedha Wilaya ya Liwale, Bw. Obadia Anania, aliipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali nchini.
“Elimu hii ni nzuri itasaidia kubadilisha maisha ya wananchi kupitia elimu hii tuliyoipata ambayo imegusa maeneo mbalimbali kama vile nidhamu ya matumizi ya fedha, kujiwekea akiba, kufanya uwekezaji na elimu ya mikopo, naamini kupitia elimu hii wananchi watabadilisha mtindo wa maisha”, alisema Bw. Anania.
Naye Afisa Msimamizi Mkuu wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Kimaro alisema kuwa Wizara inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya fedha ili kuhakikisha wananchi wote wanakua na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo kuwa na mazoea ya kujiwekea akiba, kuwa na nidhamu ya matumizi lakini pia kutumia kulingana na bajeti yako.
“Katika utekelezaji wa programu ya utoaji elimu ya masuala ya fedha, Serikali inakusudia ifikapo mwaka 2025, takriban asilimia 80 ya wananchi wawe wamefikiwa na elimu hii na kuwa na uelewa wa masuala ya fedha,” alisema Bw. Kimaro.
Alisema hadi sasa mikoa 10 imefikiwa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha na kupatiwa elimu ya fedha ikiwemo Kagera, Manyara, Singida, Kigoma, Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Mtwara na Lindi.
No comments:
Post a Comment