Na.Catherine Sungura,Arusha
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imejipanga kujenga madaraja 189 kwa kutumia teknolojia mbadala katika mikoa yote ishirini na sita nchi nzima kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Hayo yameelezwa na Mhandishi Mshauri Pharles Ngeleja wakati Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa alipotembelea banda la TARURA kwenye Kongamano la Kitaifa la 32 la Taasisi ya Wahandisi Tanzania lililofanyika kwa siku mbili katika Kituo cha Kimataifa cha Mkutano Arusha (AICC).
Mhandisi Ngeleja alisema hadi sasa wameweza kujenga madaraja 56 ya mawe ambapo utaratibu wa ujenzi wa madaraja mengine unafanyiwa kazi.
Alisema teknolojia ya ujenzi wa madaraja kwa kutumia mawe na tofari pamoja na ujenzi wa barabara kwa kutumia mawe ilikuja baada ya kuwa na mtandao mkubwa wa barabara na hivyo kuweza kubuni teknolojia hiyo ili kupunguza gharama za ujenzi.
“Ulinganifu wa barabara zetu zenye mtandao wa Km 144,429.77,mtandao huu ni mkubwa sana hivyo tuliona tutumie teknolojia mbadala ili tuweze kuwafungulia njia wananchi kuweza kufika maeneo yao ya huduma za jamii ”.
Ameongeza kuwa tangia mwaka 2017 hadi sasa TARURA imeweza kujenga madaraja 212 yenye gharama ya Bilioni 8.2 na kama wangejenga kwa kutumia zege wangetumia zaidi ya Bilioni 36.“Teknolojia hiyo imeweza kupungunguza gharama mpaka asilimia 80”.
Aidha, amesema mawe pamoja na matofari wanayoyatumia hupimwa maabara na kiwango cha chini cha ugumu wa mawe (MPA) huwa zaidi ya 25 na matofari ‘MPA’8 ndio hujengea madaraja.
Naye, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) Mhandisi Dkt. Gemma Modu alisema Uhandisi una mchango mkubwa wakuleta maendeleo nchini.
Pia ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kasi ya maendeleo nchini na kuongeza wahandisi wazawa na kuwafungulia fursa wahandisi na mafundi na kuahidi kushirikiana bega kwa bega na Serikali.

No comments:
Post a Comment