 |
| Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Tathmini ya Muda wa Kati wa Mzunguko wa 20 wa Benki ya Dunia (IDA20 Mid-Term Review) unaohusisha wakopaji, nchi Wahisani na Menejimenti ya Benki ya Dunia, unaofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip (Airport)- Zanzibar, kuanzia Leo Tarehe 6 hadi 8 Desemba, 2023. |
 |
| Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wapili kushoto), akiaga na Rais wa Benki ya Dunia, Bw. Ajay Banga (wa pili kulia), baada ya kumalizika kwa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Tathmini ya Muda wa Kati wa Mzunguko wa 20 wa Benki ya Dunia (IDA20 Mid-Term Review) unaohusisha wakopaji, nchi Wahisani na Menejimenti ya Benki ya Dunia, uliofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika Hoteli ya Golden Tulip (Airport)- Zanzibar, ambao utaendelea kuanzia Leo Tarehe 6 hadi 8 Desemba, 2023. Wa kwanza Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Wa kwanza Kulia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba. |
Na. Joseph Mahumi, WF,
Zanzibar
Serikali ya Tanzania inalenga kuongeza uwekezaji katika sekta za
kipaumbele ikiwemo sekta ya Elimu, Afya, na Kilimo cha kisasa kinachozingatia
mabadiliko ya Tabia nchi ili kuchochea ukuaji wa Uchumi Endelevu na Kupunguza
Umaskini.
Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua Mkutano
wa Kimataifa wa Tathmini ya Muda wa Kati wa Mzunguko wa 20 wa Benki ya Dunia
(IDA20 Mid-Term Review) unaohusisha wakopaji, nchi Wahisani na Menejimenti ya
Benki ya Dunia, unaofanyika kwa siku tatu, Zanzibar, ambapo pamoja na mambo
mengine utajikita kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa katika nchi zenye
kipato cha chini kupitia fedha za mkopo na msaada zinazotolewa na Mfuko huo
uliopo chini ya Benki ya Dunia.
Rais Mwinyi alisema kuwa, mfuko wa IDA umechangia kwa kiasi
kikubwa utekelezaji wa miradi ya Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwemo Mradi wa
Nishati ya umeme vijijini wenye thamani ya dola za Marekani milioni 200, ambao
umewezesha kufikia zaidi ya watanzania milioni 2.5 kupata nishati ya umeme,
pamoja na dola za Marekani milioni 335, ambazo zimetumika katika uboreshaji na
ujenzi wa vituo vya Afya na Madarasa.
“Tunatambua namna ambavyo mfuko wa IDA, umekua kielelezo kizuri
cha Ufanisi kwa nchi zenye uchumi wa chini” Alisema Mhe. Dkt. Mwinyi.
Aidha, Mhe. Rais Mwinyi, ameiomba Benki ya Dunia kupitia dirisha
la IFC na IDA kuangalia namna ya kukopesha sekta binafsi ili kuwezesha
Ushindani wa Biashara katika eneo huru la biashara Afrika hatua itakayochochea
ongezeko la ajira kupitia ushirikiano wa kikanda na biashara.
Naye Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
(Mb), amesema kuwa Kaulimbiu ya Mkutano huu wa IDA-20 ambayo ni Ukuaji Endelevu
wa Uchumi, Kujenga Uthabiti, na Kusaidia Maendeleo ya Mtaji wa Watu, inalingana
kikamilifu na vipaumbele vya Tanzania.
“Kujitolea kwa Serikali yetu katika kuboresha miundombinu,
kuwekeza katika rasilimali watu, na kukuza utawala bora, kumechangia kwa kiasi
kikubwa mwelekeo wetu wa maendeleo, na pia Uongozi wa Rais. Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, umepiga hatua kubwa katika kukuza ushirikishwaji na kujenga
uthabiti kupitia mipango mbalimbali ya maendeleo” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia, Bw. Ajay Banga, amesema
kuwa Kabla ya kufika mwaka 2030, Benki ya Dunia kupitia Mfuko wa IDA, itatoa
kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 5 kwa ajili ya kufikisha umeme wa uhakika,
nafuu, na mbadala kwa Waafrika zaidi ya milioni 100.
“Katika siku chache zijazo, tutakuwa na fursa ya kutafakari juu
ya manufaa yaliyotokana na IDA na kwa pamoja, na pia tutapata fursa ya kutoa
maoni juu ya utendaji kazi wake ili kuweza kufikia nchi za kipato cha chini kwa
ukamilifu wenye maono ya ukuaji” alisema Bw. Banga.
Mkutano huo wa Siku tatu unawakutanisha zaidi ya wajumbe 300
kutoka nchi zinazonufaika na IDA, Viongozi wa Benki ya Dunia, pamoja na
Wafadhili wanaochangia Fedha katika Mfuko huo wa IDA.
No comments:
Post a Comment