Meneja Miradi wa Taasisi ya Social Action Trust Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa (kulia) akizungumza na wajumbe wa kamati za Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne yaliyoanza Septemba 12, 2023 Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kufikia tamati Septemba 15, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Social Action Trust Fund (SATF)
iliyoanzishwa kwa udhamini wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Serikali ya
Marekani (USAID) na kuratibiwa na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kusaidia
juhudi za Serikali katika kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira
magumu waweze kuzifikia ndoto zao limeiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
mkoani Singida kuunda kamati za Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili
dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika kata kumi..
Uundwaji wa kamati hizo katika kata hizo ulienda sanjari na wajumbe walioteuliwa kupata mafunzo ya namna ya kuziendesha
kamati hizo na kujua utekelezaji wa Mpango Kazi huo wa Taifa wa Kutokomeza
Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ambapo wajumbe hao ni ni viongozi kutoka
idara mbalimbali za serikali, Asasi za Kiraia,viongozi wa dini na wawakilishi
wa makundi ya watu wenye ulemavu, wanafunzi na wanawake chini ya mwenyekiti
wake Afisa Mtendaji wa Kata.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo
Meneja Miradi wa taasisi hiyo Nelson Rutabanzibwa alisema taasisi hiyo imekuwa
ikiwawezesha watoto hao kwa kuwapeleka shuleni, ikiwa hilo halitoshi na
kuhakikisha afya zao zinakuwa sawa kwa kuwapatia bima ya afya.
Alisema pamoja na hayo kutokana na watoto hao
kutoka katika kaya zenye utete wana hakikisha wanakuwa katika ulinzi na usalama
na ndio shabaha kubwa ya kukutana katika kikao hicho cha mafunzo ya kamati hizo
za MTAKUWWA zenye lengo la kumlinda mtoto dhidi ya masuala yote ya ukatili.
Alisema kamati hizo zinawasaidia katika miradi
yao kuhakikisha watoto wanabaki shuleni kwa sababu vitendo vya ukatili wa
kijinsia dhidi ya watoto vinawafanya washindwe kutimiza ndoto zao kwa kupewa
mimba, ndoa za utotoni huku wengine wakiingizwa kwenye ajira wakiwa na umri
mdogo na wale wengine ambao -+-+kwa uzembe wao wanaacha tu kwenda shuleni.
Alisema kwa Mkoa wa Singida ipo changamoto kubwa
ya watoto kuacha shule kwani walianza na watoto 80 lakini hadi sasa wamebaki na
watoto 78 baada ya watoto wawili kutoka kwenye mradi kutokana na sababu mbalimbali
kama, mimba, utoro na masuala ya nidhamu.
“Kupitia kamati hizi tunategemea zitaweza
kutusaidia kutokana na wajumbe wake kuwa ni polisi ngazi ya kata, maafisa
maendeleo, waratibu wa elimu, watendaji wa kata na wengine wote wenye majukumu
mbalimbali ngazi ya jamii ambao kwa namna moja yanaweza kusaidia kuwaondolea
vikwazo watoto hao washindwe kuendelea na masomo yao,” alisema Rutabanzibwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo aliwataka washiriki
kuyatendea kazi hasa kutokana na unyeti wa masuala hayo ya ukatili ambayo
yamekuwa ni changamoto kubwa kwenye jamii.
“Niwaombe sana mafunzo mnayopata hapa baada ya
kwenda huko kwenye jamii mkayafanyie kazi kwa kuwafichua wanayotenda na
kuhakikisha yanafikishwa kwenye vyombo vya dola na kuepuka kupokea rushwa
kutoka kwa watuhumiwa kwa lengo la kuwasaidia,” alisema Myula.
Myula alitumia nafasi hiyo kulishukuru shirika
hilo la SATF kwa kuiwezesha halmashauri hiyo kwa kuunda kamati hizo katika
vijiji hivyo 10 ambazo zinakwenda kuongeza mapambano dhidi ya vitendo vya
ukatili kwa watoto na wanawake.
Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable
Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa,
Benard Sungi ambao wanafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi hiyo alisema kwa
ushirika wao wameweza kufanya kazi katika Kata nne za Ihanja, Lighwa, Isunna na
Kituntu ambapo waliwabaini watoto 80 ambao walikuwa katika mazingira magumu
ambao wamepata ufadhili wa masomo kupitia Taasisi hiyo ya SATF.
Alisema kati ya watoto hao wawili waliondoka
kwenye mradi na kuwa hao wengine wanaendelea na masomo katika shule mbalimbali
za sekondari ambazo amezitaja kuwa ni Isuna, Masinde, Lighwa, Utaho, Miandi na
wengine wapo Chuo cha Ufundi Stadi cha FDC kilichopo Manispaa ya Singida.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa
Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Mariam Mwandekile alisema mafunzo hayo yamelenga
kuzifikia kamati za MTAKUWWA katika kata 10 ambazo ni Puma, Kituntu, Ihanja, Issuna, Dung’unyi,
Mtunduru, Sepuka, Makiungu, Mungaa na Lighwa.
Alisema anaamini kabisa kuwa kamati hizo
zitakapoanza kutekeleza majukumu na mikakati yao zinakwenda kumaliza kama sio
kupunguza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.
Alisema baada ya mafunzo hayo watakwenda
kutengeneza mpango kazi na kuanza kuutekeleza ambapo kila baada ya miezi mitatu
watakuwa wakitoa taarifa ambayo itaunganishwa na ya wilaya hiyo na kuwa kila
mmoja wao atakuwa ni balozi wa kutoa elimu ya kupinga vitendo vyote vya ukatili
katika sehemu zao.
Afisa wa Dawati la Jinsia Kituo cha Polisi Wilaya
ya Ikungi, Musa Musa alisema katika wilaya hiyo bado kunachangamoto ya vitendo
vya ukatili wa kijinsia vikiwamo vipigo kwa watoto na wanawake, mimba za
utotoni, ubakaji, ulawiti na kurithiwa wajane baada ya waume zao kufariki na
baadae wakijikuta wakifukuzwa na kunyang’anywa mali walizozichuma na wenza wao.
Alisema kesi nyingi za matukio hayo zimekuwa
hazipati ushindi kutokana na mashahidi kushindwa kufika mahakamani kwa sababu
mbalimbali zikiwamo za wahusika kupatana na watuhumiwa kwa kupewa fedha hivyo jamuhuri
kushindwa kuendelea na kesi hizo kwa kukosa ushahidi.
Alisema desturi ya wajane kurithiwa na ndugu au
mdogo wa mume wake baada ya kufariki bado ipo katika wilaya hiyo na inafanyika
kwa mtindo wa aina yake kwa familia husika kumchagua mmoja wanafamilia kuwa
mwangalizi wa familia ya marehemu ambapo utakuta mjane huyo akiendelea
kuzalishwa na endapo atakataa kufanya hivyo atajikuta akifukuzwa huku
akinyang’anywa mali alizochuma na mume wake.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa
Ustawi wa Jamii wilayani humo, Flora Temba alisema kuna aina nyingi za ukatili
wa kijinsia ambao watu wamekuwa wakifanyiwa hasa watoto na wanawake ambao
ameutaja kuwa ni wa kingono, kiuchumi, kisaikolojia, vipigo, kunyang’anywa
ardhi.
Temba alisema iwapo atatokea mtu kufanyiwa
ukatili huo anaweza kutoa taarifa, kituo cha polisi dawti la, kwa wajumbe wa
kamati ya MTAKUWWA, ofisi za Kata, maafisa wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii na Huduma
ya Mkono kwa Mkono (One Stop Centre) na maeneo mengine ambayo ataona anaweza
kupata msaada.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ya MTAKUWWA, Mwinjilisti
Isaya Jibu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) akiliwakilisha kundi
la viongozi wa dini na mwakilishi wa wanafunzi Salima Juma kutoka Shule ya
Msingi ya Damankia walisema kamati hizo zinakwenda kuwa mwiba kwa wale wote
wanaoendelea kufanya vitendo hivyo.
Mwinjilisti Jibu ametoa mwito kwa wananchi wa maeneo yote ya kata hizo kutoa taarifa za matukio yote ya ukati kwa wajumbe hao ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua na vyombo husika
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja. Aliye chuchumaa ni Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa, Benard Sungi.
No comments:
Post a Comment