WAZIRI DKT. GWAJIMA AFUNGUA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA CHA WIZARA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 11 August 2023

WAZIRI DKT. GWAJIMA AFUNGUA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA CHA WIZARA

 

 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akipokea moja ya simu ya mteja katika Kituo cha Huduma kwa Mteja (Jamii Call Center) katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma Agosti 10, 2023.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kituo cha Huduma kwa Mteja (Jamii Call Center) katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma Agosti 10, 2023.

Na WMJJWM, DODOMA

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amefungua rasmi kituo cha huduma kwa wateja kitakachojulikana kama JAMII CALL CENTER ili kuratibu malalamiko na taarifa kuhusu huduma za Maendeleo na Ustawi wa Jamii nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Agosti 10, 2023, Waziri Dkt. Gwajima amesema lengo la kituo hicho kitakachotumia namba 026-2160250 na 0734 986503 ni kuongeza wigo wa kuwahudumia wananchi kwa haraka na ufasaha hasa katika changamoto zinazohitaji Wizara kuingilia kati.

Amesema moja ya changamoto iliyokuwepo kabla ya kituo hicho ni wananchi kutofikia taarifa na huduma za Wizara kwa urahisi pale wanapohitaji ambapo namba inayotumika ni 116 iliyo chini ya wadau kwa ajili ya taarifa za ukatili dhidi ya watoto na wakati mwingine yeye mwenyewe kutumia namba yake binafsi.

"Mpango wa muda mrefu ni kupanua wigo wa utoaji wa huduma hizi kutoka matumizi ya simu pekee na kutumia njia nyingi zaidi za mawasiliano kama vile barua pepe, ujumbe mfupi na mitandao ya kijamii ili kuboresha huduma" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kwamba, pamoja na Taarifa za pongezi, malalamiko, maoni na ushauri kuhusu huduma za maendeleo na ustawi wa jamii ufunguzi wa JAMII CALL CENTER utasaidia kupata taarifa, elimu, huduma na ufumbuzi dhidi ya changamoto mbalimbali zikiwemo Usajili wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii na fursa za maendeleo na mikopo nafuu kwa wanawake wajasiriamali na makundi maalum.

"Wananchi wataelimishwa utaratibu wa kuasili Watoto na Malezi ya Kambo, watapata Mwongozo na utaratibu wa huduma dhidi ya manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na kwa watoto pamoja na Msaada wa kisheria kwa manusura wa ukatili wa kijinsia na kwa watoto na haki za wanawake na wajane" ameongeza Dkt. Gwajima.

Ameongeza pia JAMII CALL CENTER itasaidia kutoa utaratibu wa huduma kwa wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu, utaratibu wa kuokoa watoto wanaoishi mazingira hatarishi na kufanya kazi mitaani, wazee wasiojiweza na familia duni. 

Hali kadhalika ,kituo hicho kitaelimisha Utaratibu wa huduma za msaada wa kisaikolojia, kutoa Miongozo kuhusu huduma za utatuzi wa migogoro ya familia na ndoa, Huduma za marekebisho ya tabia na elimu kwa watoto watukutu na Utaratibu wa kusajili na kulipia huduma mbalimbali zikiwemo za mitihani, usajili wa makao ya watoto, vituo vya kulelea watoto mchana (day care centres) na Asasi zisizo za Kiserikali.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Taarifa zitakazopokelewa na kituo hicho zitafanyiwa kazi kwa haraka na zitakazohitaji ufumbuzi wa nje ya Wizara zitawasilishwa kwenye Wizara za Kisekta zinazohusiana na taarifa iliyopokelewa. 

Amewaomba Wadau mbalimbali wa kisekta kutoa ushirikiano na kuunganisha nguvu za pamoja katika kutatua changamoto zitakazopokelewa na kituo hicho ili kuwasaidia wananchi na kuwaletea maendeleo.

Akitoa maelezo kuhusu kituo hicho Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Jihn Jingu amesema lengo la Kituo hicho ni kupokea maoni, changamoto na malalamiko kutoka kwa wananchi moja kwa moja ili kuwahudumia na kuwaunganisha wananchi na huduma za Wizara mahali popote.

"Kituo hiki kitatusaidia kupata mrejesho wa moja kwa moja huduma ambazo tutazitoa katika Wizara yetu na itasaidia kuchakata taarifa na kufikia kuboresha huduma muhimu tunazozitoa" alisema Dkt. Jingu

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema Jamii imekuwa ikipata changamoto mbalimbali katika mchakato wa kujiletea maendeleo hivyo Kituo hiki kitatoa fursa ya kupata ufafanuzi katika masuala mbalimbali na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Wizara za kisekta itasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinaiwakabili wananchi. 

No comments:

Post a Comment