Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa. |
KATIKA kuhakikisha Sekta ya Usafiri kwa njia ya maji unaimarika Serikali Kupitia Kampuni ya huduma za Meli imedhamiria kujenga meli tatu mpya katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika baada ya kukamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ukarabati wa meli ya MV. Liemba.
Meli hizo mpya ambazo zitajumuisha ujenzi wa meli moja ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 na meli moja ya abiria na mizigo yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mabehewa ya mizigo katika Ziwa Tanganyika.
Hayo yamesemwa leo Mei 22,2023 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2023/2024.
Mbali na ujenzi wa meli hizo mpya Prof. Mbarawa aliongeza kuwa MSCL tayari imeshakamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ukarabati wa meli ya MV. Liemba tarehe 5 Machi, 2023.
“Kwa sasa, majadiliano na Mkandarasi kabla yakusaini mkataba yanaendelea. Mkataba huo unatarajiwa kusainiwa Julai, 2023. Aidha, MSCL inakamilisha taratibu za kumwajiri Mhandisi Mshauri kwa ajili kufanya tathmini ya kina na kuishauri Serikali kuhusu ukarabati wa meli ya MV. Mwongozo ambayo ilisimamishwa kutokana na changamoto ya msawazo (stability). Kazi hii inatarajia kuanza mwezi Juni, 2023 na kukamilika mwezi Novemba, 2023.” Alisema.
Aidha, Prof. Mbarawa alielezea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi mitatu mikubwa ya ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo ya MV Mwanza Hapa kazi Tu na ukarabati mkubwa wa Meli ya mizigo ya MV Umoja za Ziwa Victoria pamoja na ukarabati wa meli ya kubeba mafuta ya MT. Sangara ya Ziwa Tanganyika.
“Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo umekamilika kwa asilimia 83, Meli ya MV Umoja yenye uwezo wa kubeba tani 1,200 za mizigo umekamilika kwa asilimia 75.8 na meli ya MT. Sangara yenye uwezo wa kubeba lita 400,000 umekamilika kwa asilimia 90.7.”
Katika mapendekezo hayo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeomba kiasi ya Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa meli mpya na Ukarabati.
No comments:
Post a Comment