KatibuTawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga akifungua mkutano wa wadau wa Bohari ya Dawa (MSD) uliofanyika Mei 3, 2023 mjini Singida. Kulia ni Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi na kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Victorina Ludovick.
Na Dotto Mwaibale, Singida
BOHARI ya Dawa (MSD) imefanya maboresho katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini.
Hayo
yamesemwa na Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi wakati akimkaribisha mgeni
rasmi KatibuTawala wa Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga kufungua mkutano wa
wadau wa MSD uliofanyika mjini hapa hivi karibuni na kuhudhuriwa na Mganga Mkuu wa mkoa, Waganga Wakuu wa
Wilaya,Wafamasia,Wataalam wa maabara na viongozi wa MSD.
Sipendi alisema ili kufikia dira na kutimiza dhima na malengo yake, MSD inadumisha na kusimamia mfumo wenye tija wa ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vya umma nchini na baadhi ya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Alitaja kazi nyingine ni kutumia ujuzi, weledi, mbinu, taratibu na ushauri wa kitaalamu katika kusimamia na kudhibiti utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya.
Alitaja eneo lingine ni kufuatilia mahitaji ya bidhaa za afya na kusimamia usambazaji wake katika vituo vya kutolea huduma za afya, huduma za afya katika vituo vya umma na kuboresha pale inapobidi na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya zinapatikana kwa wakati.
Sipendi aliongeza kuwa ili kuhakikisha hayo yote yanafanikiwa, MSD imefanya maboresho kwa kukasimu baadhi ya madaraka na majukumu kwa kanda ili
kurahisisha utekelezaji wa majukumu katika eneo hilo.
Aidha, MSD imeanza kusambaza bidhaa za afya mara sita kutoka mara nne ya awali na kuwezesha kuboresha mifumo ya ndani ya utendaji, kuboresha huduma na mawasiliano na wateja.
Alisema kutokana na serikali kutenga na kuleta fedha za
kununulia bidhaa za afya kama ilivyopanga, upatikanaji wa bidhaa za afya
umepanda kutoka asilimia 54 iliyokuwepo mwishoni mwa mwaka jana na kufikia
asilimia 76 sasa, kuongeza wataalamu ili kuweza kuwa na fani mbalimbali
kuendana na majukumu ya MSD.
Pia Sipendi alisema MSD imeweza
kufanikisha kusambaza vifaa vya uzazi pingamizi wa mama na mtoto (CEmONC), vifaa
vya maabara na mashine za kusafisha damu kwa baadhi ya hospitali kama vile Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dk.Mganga alisema mkutano huo umelenga kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kujadili changamoto zinazovikabili vituo vya afya vya kutolea huduma ili ziweze kupangiwa maazimio na mikakati ambayo itamsaidia mteja au mwananchi kupata huduma iliyo bora.
“Mheshimiwa
Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan ametoa kipaumbele kikubwa katika
sekta ya afya kwa kutoa fedha nyingi za kujenga Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati , tumejenga majengo ya wagonjwa mahututi
(ICU) majengo ya kupata huduma ya dharura ambayo ni ya kisasa,” alisema Dk.Mganga.
Alisema Serikali imefanya yote hayo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora na za uhakika.
Aidha, Dk.Mganga alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwa kufanya
kipengele chake na kilichobakia ni kwa wadau, MSD na wafanyakazi kuboresha pale
ambapo amekomea na wanalojukumu la kuhakikisha mgonjwa anapata matibabu bora.
Aliongeza kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wanapoambiwa dawa hakuna na jambo ambalo linatokana na madaktari kukalili dawa aina moja wakati magonjwa yaliyo mengi yanatibiwa zaidi ya dawa moja.
"Dawa inaweza kutolewa kama mbadala na
kuondoa dhana ya wananchi kuichukia Serikali yao pale wanapoambiwa dawa hakuna, madaktari nawaomba kabla ya kumuandikia mgonjwa dawa mjue akiba za dawa zilizopo ili kuondoa malalamiko ya wananchi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Victorina Ludovick alisema maagizo yaliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa yatafaniwa kazi ikiwamo uboreshaji wa huduma za afya pamoja na upatikanaji wa bidhaa za afya.
Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi, akizungumza kwenye mkutano huo.
No comments:
Post a Comment