ELIMU YA AFYA NI MUHIMU KATIKA KUKABILINA NA MAGONJWA YA MLIPUKO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 23 May 2023

ELIMU YA AFYA NI MUHIMU KATIKA KUKABILINA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

IMEELEZWA kuwa elimu ya kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko ina umuhimu mkubwa katika jamii.

Hayo yamebainishwa na Afisa afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Jackline Saulo wakati akizungumza na watumishi katika kituo cha afya cha Kimeya Wilayani Muleba Mkoani Kagera mara baada ya timu ya wataalam wa afya kutoka mkoa wa Kagera na Halmashauri ya Muleba kufika katika kitup hicho lengo ni kujionea kanuni za afya hususan kukabiliana na magonjwa ya mlipuko zinavyozingatiwa katika kituo hicho.

“Sasa hivi tunaendelea kutembelea katika jamii, vituo vya kutolea huduma ya afya, wagonjwa wote wanaotufikia tunatakiwa kuwafikishia elimu ya kutosha namna gani ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko,” amesema.

Aidha,Saulo amesema watumishi wa afya ngazi ya Jamii (CHW)wana umuhimu mkubwa katika kuhakikisha wanafikisha elimu ya afya katika maeneo yao.

Kaimu Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya  cha Kimeya Dkt. Albert Bongo amesema amesema baada ya kuripotiwa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg hatua mbalimbali za afya zilichukuliwa katika kituo hicho ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vifaa vyote vya usafi ikiwemo maji tiririka na sabuni viliwekwa kila lango la kituo hicho pamoja na watalaam wa afya kujengewa uwezo.

Akitoa elimu ya afya kwa watu waliofika katika kituo hicho kupata huduma za matibabu, mratibu wa elimu ya afya kwa umma halmashauri ya Muleba Johanes Mutoka amesema ni muhimu kuacha tabia ya kusalimiana kwa kushikana mikono ili kuepuka magonjwa ya mlipuko huku Baraka Mohammed akiomba elimu iendelee kutolewa mara kwa mara sehemu za vijijini.

Akiwa katika gulio la Kimeya  Kijiji cha Nkomelo kata ya Kasharunga wilayani Muleba Mkoani Kagera mratibu huyo wa Elimu ya Afya kwa Umma amekumbusha dalili za ugonjwa wa Marburg ikiwa ni pamoja na homa, kutapika damu, kutokwa na damu sehemu za wazi za mwili huku akiainisha jinsi unavyoweza kuambukiza ni pamoja na kugusana ambapo pia amehimiza umuhimu wa vyoo bora katika kukabiliana magonjwa ya mlipuko.

Ikumbukwe kuwa katika kituo cha afya Kimeya jumla ya watu 61 wamepatiwa elimu ya afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwa ni wananchi 53 na watumishi 8 ambapo gulio la Kimeya jumla ya wananchi 150 wakipatiwa elimu huku gulio la Mubunda Kijiji cha Kishoju jumla ya watu 98 wakipatiwa elimu hiyo ya namna ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Marburg.

No comments:

Post a Comment