WANAMICHEZO MEI MOSI WATOA MSAADA KWA WAHITAJI WENYE THAMANI ZAIDI YA SH. MILIONI 10 MOROGORO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 27 April 2023

WANAMICHEZO MEI MOSI WATOA MSAADA KWA WAHITAJI WENYE THAMANI ZAIDI YA SH. MILIONI 10 MOROGORO

Makamu Mwenyekiti Kamati ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Masamu akiwakabidhi baadhi ya watoto wanaolelewa katika Kituo cha Raya Islamic Orphanage Centre Morogoro kilichopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro mahitaji yaliyotolewa na wanamichezo wanaoshiriki michezo ya Mei Mosi 2023 kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho Aprili 26, 2023 mkoani Morogoro.

Makamu Mwenyekiti Kamati ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Masamu (kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa Kituo cha Raya Islamic Orphanage Centre Bi Raya Maganga (kulia) mahitaji yaliyotolewa na wanamichezo wanaoshiriki michezo ya Mei Mosi 2023 kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho Aprili 26, 2023 mkoani Morogoro.

Makamu Mwenyekiti Kamati ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Masamu (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa Kituo cha Mwenda Foundation Bi Prakseda Jeremias (kushoto) mahitaji yaliyotolewa na wanamichezo wanaoshiriki michezo ya Mei Mosi 2023 kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho Aprili 26, 2023 mkoani Morogoro.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WANAMICHEZO wanaoshiriki mashindano ya Mei Mosi mkoani Morogoro wametekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutumia Siku ya Maadhimisho ya 59 za Muungano wa Tanzania kwa kutoa misaada yenye thamani ya takriban Shilingi milioni 10 kwa wahitaji mkoani humo.

Akifanya majumuisho baada ya kutembelea vituo vitano vya wahitaji Aprili 26, 2023, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Masamu amesema wametumia siku hiyo ikiwa ni utaratibu wa wanamichezo wakati wa mashindano ya Mei Mosi Kitaifa kila mwaka kutenga siku moja kuwatembelea wahitaji na kuwapatia mahitaji mbalimbali.

“Siku ya leo tumekutanika wanamichezo kutoka taasisi zote zinazoshiriki mashindano ya Mei Mosi kwa kuwashirikisha viongozi wa timu na wanamichezo, tumekusanya kiasi cha takriban Shilingi milioni 10 ambazo zimetumika kununua mahitaji mbalimbali ambayo tumeyapeleka kwa wahitaji katika vituo vitano” Bi. Masamu.

Amesema fedha hizo ambazo wanamichezo hao wametoa kwa kuchangishana zimetumka kununua vyakula, umeme kwa vituo vinne ambavyo majengo yao yanatumia umeme na kituo kimoja cha Raya Islamic Orphanage Centre kimepewa fedha taslimu kiasi cha Shilingi 400,000/= kwa ajili ya kununua mafuta ya jenereta, vifaa tiba ikiwemo basiskeli mbili za kutembelea wenye ulemavu pamoja na mahitaji mengine ya muhimu ikiwemo vifaa vya wanafuzi vya kusomea na kujifunzia.

Makamu Mwenyekiti huyo amesema vituo vilivyotembelewa na wanamichezo hao katika manispaa ya Morogoro ni vine na kimoja kipo wilaya ya Mvomero. Katika eneo la manispaa ya Morogoro vituo vilivyotembelewa ni Amani Centre chenye watoto 48 wakiwemo watoto wa kiume 25 na wakike 23, kituo cha Mission to the Homeless Children (MHC) Morogoro chenye watoto 39, makazi ya wazee cha Fungafunga chenye wazee 22 wakiwemo wa kiume 15 na wa kike 7 na kituo cha Mwenda Foundation chenye watoto 10 wakati katika wilaya ya Mvomero kituo kilichotemebelewa na kupewa mahitaji hayo ni Raya Islamic Orphanage Centre chenye watoto 73 wakiwemo wa kiume 33 na watoto wa kike 40.

Aidha, Makamu Mwenyekiti Bi. Masamu ametoa wito kwa watanzania wakiwemo watu binafsi, watumishi wa umuma na sekta binafsi kutenga muda wao na kuona umuhimu wa kutembelea vituo hivyo na kuwapelekea mahitaji mbalimbali.

“Ukweli unapokuwa nje ya vituo hivi huwezi kugundua, lakini unapovitembelea vituo hivi, unaona kuna uhitaji mkubwa. Sisi kama familia, taasisi na mtu mmoja mmoja nawasihi mtumie muda wenu na rasilimali zenu kuwapatia watu hawa mahitaji ili nao wafurahie maisha kama watu wengine” amesema Bi. Masamu.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro Jesca Kagunila amewashukuru wanamichezo hao kwa kutenga muda na kujitoa kuwasaidia wahitaji katika vituo hivyo kwa kuwaonesha upendo wao kwao na kuwahimiza watu wengine waige mfano wa wanamichezo hao na kuendelea kuwapenda wahitaji.

Kwa upande wake Padre Beatus Sewando, Mkurugenzi wa Kituo cha Amani Centre ambacho kinalea watoto wenye mazingira magumu na wenye mahitaji maalum amesema kituo hicho kinapata watoto hao kwa kuwaibua, wapo waliokuwa wanafungiwa ndani na wazazi/walezi wao, wapo wanaoletwa na Serikali kupitia Idara ya Ustawi wa jamii baada ya kutelekezwa ama kuokotwa.

Padre Sewando ameongeza kuwa kituo hicho kimejikita kuwasaidia watoto wote kituoni hapo bila kuwabagua wakiwemo wenye uhitaji maalum ili kuwaonesha upendo na kuwapatia haki zote ambazo binadamu anastahili kupata.

“Kwa kweli tunamshukuru Mungu, watoto wengi wamepata nafuu kwa kufanya mazoezi, wanajimudu katika maisha na hata wengine wapata nafasi ya kusoma katika shule yetu ya Mvomero ambayo ina mpaka darasa la saba na wengine wameendelea na hatua nyingine za masomo hata kuajiriwa maeneo mbalimbali” amesema Padre Sewando.

Aidha, Padre Sewando amebainisha na kusema zipo changamoto zinazokabili vituo vya kulelea watoto ikiwemo rasilimali fedha, matibabu kwa watoto wanapougua, chakula, vifaa maalum kwa ajili ya watoto kufanyia mazoezi.

Michezo ya Mei Mosi mwaka 2023 ambayo inawahusisha watumishi wa umma na sekta binafsi inapambwa na kaulimbiu “Miaka Miwili ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Imeimarisha Michezo na Kuongeza Ufanisi Kazini, Kazi Iendelee”.


No comments:

Post a Comment