ASA YASISITIZA MATUMIZI YA MBEGU BORA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 24 April 2023

ASA YASISITIZA MATUMIZI YA MBEGU BORA


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

WAKALA wa Mbegu za Kilimo (ASA) umesisitiza wakulima kuendelea kutumia mbegu bora za kilimo ambazo zimefanyiwa utafiti kulingana na mazingira ya sasa ili kuongeza tija katika kilimo na kulinda usalama wa chakula.

Msisitizo huo umetolewa hivi karibuni wilayani Kilosa mkoani Morogoro na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA), Dkt. Sophia Kashenge huku akifafanua kuwa usalama wa nchi yoyote ni usalama wa chakula na haiwezekani kuwa na usalama wa chakula bila kuwa na usalama wa mbegu.

Ameongeza kuwa, miaka ya nyuma asilimia kubwa ya mbegu zilikuwa zikitoka nje, hivyo sio rahisi kwa nchi kujihakikishia usalama wa chakula kama chanzo cha chakula kilitegemewa kutoka nje ya nchi.

“Matumizi ya mbegu bora nchini bado yako chini, tunawasisitiza wananchi kuwa matumizi ya mbegu bora ni muhimu kwa sababu uchumi wowote katika kilimo unaanza na mbegu sahihi na bora, unapokuwa na mbegu bora tayari umeshajihakikishia asilimia 30 ya ongezekezo la kipato hivyo ukiongeza mbolea, mbinu bora za uzalishaji utavuna kwa tija.” Alisema Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA), Dkt. Sophia Kashenge.

Ameeleza kuwa ASA imesimamia usalama wa chakula kwa kuzalisha mbegu bora za mazao mbalimbali pamoja na kuwa na wigo mpana wa kufanya kazi kutegemea na mipango ya Serikali ambapo inaweza kuelekeza tani kadhaa za zao fulani zipelekwe eneo husika na zigawiwe bure ili kuwasaidia wakulima wanaopata majanga yakiwemo ya mafuriko na ukame.

Kwa upande wake, Afisa Tarafa ya Kimamba iliyopo wilayani Kilosa, Sabina Sugwa amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawekea Shamba la ASA katika maeneo hayo kwani uwepo wa shamba hilo unawasaidia wananchi kupata mbinubora za kutumia mbegu bora. Aidha, ametoa rai kwa wakulima kuacha kilimo cha kizamani cha bila kutumia mbegu bora.

Mashamba ya ASA yanayotumika kuzalishia mbegu yapo kwenye ikolojia zote za uzalishaji na yapo katika Mikoa ya Arusha, Tanga, Pwani, Morogoro, Tabora, Kigoma, Songwe, Ruvuma na Iringa. Moja ya shamba la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) lililopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro linalotumika kuzalishia mbegu.

No comments:

Post a Comment