MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe Jeryy Silaa ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha uwekezaji unaofaywa kupitia maboresho ya njia kwa reli ya Kati, Chuo cha Reli na Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR unakuwa na matokeo chanya kwa Taifa.
Akizungumza wakati alipotembelea Stesheni, Karakana na Chuo cha Reli Mkoani Tabora Mwenyekiti Jerry Silaa amesema Shirika la Reli ni miongoni mwa Mashirika ambayo Serikali imewekeza zaidi ya trilioni 15 lengo kuliwezesha shirika hilo kujitegemea baada ya uwekezaji huo kukamilika.
“Kwa uwekezaji uliowekwa katika Sekta ya Usafiri kupitia TRC tunapaswa kujipanga sawa sawa sababu wananchi hawatawaelewa kama uwekezaji huu utakamilika na tija isionekane” amesisitiza Mwenyekiti Silaa.
Mwenyekiti Silaa ameitaka Wizara kupitia TRC kuongeza nguvu kwenye usimamizi wa reli ya kati kwani imeonekana nguvu kubwa imewekezwa kwenye Reli ya Kisasa na hivyo kupunguza ufanisi kwa reli ya kati.
Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Profesa John Kondoro ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza fedha kwa TRC kwani kukamilika kwa miradi yote ya uboreshaji, ununuzi na ujenzi utarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo na hivyo kupunguza gharama za bidhaa.
P
Aidha, Mwenyekiti Prof. Kondoro ameihakikishia kamati ya Bunge kuwa TRC imejipanga kwa uendeshaji wa reli ya kisasa kwa kuweka mpango madhubuti wa biashara wa muda mfupi na muda mrefu ili kujipima kwa vigezo maalum kulingana na fedha iliyowekezwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Amina Lumuli, amesema mpango unaotekelezwa wa maboresho ya miundombinu ya reli umehusisha ujenzi wa Chuo kikubwa kitakachofundisha kozi mbalimbali za usimamizi na uendeshaji wa reli zote mbili lengo likiwa kuongeza wataalam.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) iko katika ziara mkoani Tabora ambapo imekagua miundombinu ya reli na Chuo cha Reli ili kuona utayari wa shirika hilo katika uaandaaji wa wataalam na uendeshaji wa reli ya SGR baada ya miradi hiyo kukamilika.
No comments:
Post a Comment