RUFIJI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 20 March 2023

RUFIJI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, akiwa na Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, wakishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Nyamwage hadi Utete (km 33.7) kwa kiwango cha lami kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mkandarasi kutoka Kampuni ya  China Railway Seventh Group, wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Muonekano wa sehemu ya barabara Nyamwage hadi Utete (km 33.7) ambayo mkataba wa ujenzi wake kwa kiwango cha lami umesainiwa na kushuhudiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wilayani Rufiji mkoani Pwani.

WANANCHI wa Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia fursa ya ujenzi wa barabara za lami ili kukuza biashara. 

Wito huo umetolewa na Naibu  Waziri wa Ujenzi  Eng. Godfrey Kasekenya mara baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Nyamwage hadi Utete (km 33.7) kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa Daraja la  Mbambe (m 81) na barabara unganishi (Km 3) kati ya Wakala wa Brabara (TANROADS), na kampuni za China Railway Seventh Group na Nyanza Road Works ya Tanzania. 

"Ujenzi wa barabara hii na daraja utafungia fursa za usafirishaji wa abiria, mizigo, mazao ya biashara, misitu na kuvuta watalii hivyo hii iwe chachu kwa wakazi kufungua biashara mbalimbali zitakazoinua uchumi wa Wilaya hii", amesema Eng. Kasekenya. 

Amesema ujenzi huu ni mkakati na miapango ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha miundombinj ya barabara na madaraja nchini ili kuondoa kero kwa wananchi na kuunganisha barabara za mikoa na wilaya ya nchi nzima. 

Aidha, ameongeza kuwa ujenzi wa barabara pamoja na daraja hilo utatumia fedha za ndani kwa asilimia mia moja hivyo jukumu la kulinda vifaa vya ujenzi na kuvitunza ni la kila wananchi ili viweze kuleta matokeo chanya kwa Wilaya. 

Ametoa agizo kwa TANROADS kuhakikisha anawasimamia wakandarasi hao ikiwezekana mradi ukamilike kabla ya wakati na kwa thamani halisi ya fedha. 

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Rufiji ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa takriban bilioni 70 kwa ajili ya mradi huo kwani utaifungua Rufiji na kuifanya kuwa kituo cha maendeleo kwa mkoa wa Pwani. 

"Wananchi wameisubiri barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami  tangu mwaka 1970 bila mafanikio na kwa ujenzi huu Rais Samia ameingia mioyoni mwa wana Rufiji", amesema Mchengerwa.

Akitoa taarifa ya mradi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS)  Eng. Rogatus Mativila ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utajengwa na mkandarasi kutoka Kampuni ya China Railway Seventh Group Co., Ltd. ya nchini China kwa gharama ya Shilingi TZS 43,419,537,043.19, bila kujumuisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa muda wa Miezi 24 na huku ujenzi wa Daraja la Mbambe utajengwa na Mkandarasi kutoka Kampuni ya Nyanza Road Works Ltd ya Tanzania kwa gharama ya Shilingi 24,164,904,622.00 kwa muda wa miezi 24. 

Ameongeza kuwa  daraja hilo litakuwa na upana wa mita 10.5 ambapo mita 7.5 zitatumika kwa ajili ya kupita magari na mita 2.5 kwa ajili ya waenda kwa miguu na waendesha baiskeli. 

Akitoa salam za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya miundombinu inayoendelea mkoa wa Pwani na kuwahakikishia wakandarasi kuwa mkoa huo uko salama na watakuwa pamoja nao wakishirikiana.


No comments:

Post a Comment