PAC YARIDHISHWA UJENZI WA BARABARA NJOMBE-MORONGA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 16 March 2023

PAC YARIDHISHWA UJENZI WA BARABARA NJOMBE-MORONGA

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Japhet Hasunga akisisitiza jambo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Balozi, Eng. Aisha Amour wakati kamati hiyo ilipokagua barabara ya Njombe-Moronga KM 53.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.

Muonekano wa barabara ya Njombe-Moronga KM 53.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika mkoani Njombe.

KAMATI  ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeelezea kuridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa barabara mkoani Njombe.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Japhet Hasunga amesema baada ya kupitia na kukagua barabara ya Njombe-Moronga KM 53.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika wameridhika na utekelezaji wa mradi huo.

“Nitoe wito kwa watumiaji wa barabara kuhakikisha wanazingatia alama za barabarani na maelekezo mengine halali ili kuepusha ajali na kuwezesha barabara  kudumu kwa muda uliokusudiwa”, amesema Mhe. Hasunga.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ameishukuru Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kutoa fedha zaidi ya bilioni 5 ili kuwezesha kujengwa kwa barabra kuelekea eneo la Liganga na Mchuchuma na kusema hatua hiyo itawezesha uwekekezaji mkubwa wa chuma na makaa ya mawe na hivyo kukuza uchumi wa mkoa huo.

“ Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa barabara za lami za kimkakati hali itakayovutia wawekezaji wa kilimo, utalii na viwanda mkoani humu”, amesema Mtaka.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Balozi, Eng. Aisha Amour ameishukuru kamati ya PAC na kuahidi Wizara itatekeleza maelekezo yake ili kuboresha miradi inayoendelea na hivyo kuleta tija kwa wakati.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iko mkoani Njombe kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali ambapo pamoja na mambo mengine imekagua barabara ya Njombe-Moronga KM 53.9 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.


No comments:

Post a Comment