TAKRIBANI BIL. 30 KUTENGWA KWA AJILI YA UBORESHAJI WA VIWANJA VYA NDEGE NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 3 February 2023

TAKRIBANI BIL. 30 KUTENGWA KWA AJILI YA UBORESHAJI WA VIWANJA VYA NDEGE NCHINI

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akimkabidhi hundi Mtaalam kutoka Kampuni ya Target Technologies, Keneth Urembo, aliyebuni nembo mpya ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), wakati wa uzinduzi wa nembo hiyo, magari 14 na maboresho ya Jengo la Watu Mashuhuri katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dkt. Ally Possi (wa pili kulia), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila (kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja cha Ndege Tanzania (TAA), Mussa Mbura (kushoto) wakikata utepe kuashiria kukamilika kwa maboresho ya Jengo la Watu Mashuhuri katika Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) uznduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam.


SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, imesema inatarajia kutenga takribani bilioni 30 katika mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege nchini ili kuimarisha utoaji huduma bora kulingana na viwango vya shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa wakati akizindua nembo mpya ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Magari 14 na maboresho ya Jengo la Watu Mashuhuri (V.I.P), uliofanyika katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha viwanja vyote nchini vinatoa huduma kwa saa 24.


“Serikali imejipanga kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege hapa nchini kwa kuvikarabati, kuvijenga na kuweka miundombinu yote muhimu inayohitajika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa”, amesema Prof. Mbarawa. 


Ameitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa inaendelea kuboresha huduma kwa wakati kwa wasafiri na watoa huduma wengine katika viwanja vyote nchini.


“Niwapongeze kwa hatua hii muhimu lakini Mkurugenzi Mkuu uzinduzi huu usiishie kuwa na nembo nzuri tu, nina taarifa kuwa wakaguzi wa kimataifa watakuja hapa siku si nyingi kukagua utoaji wa huduma, hivyo hatutarajii alama kushuka zaidi ya 70”, amesisistiza Waziri Prof. Mbarawa.


Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa abiria wote wanaopita viwanja vya ndege kukaguliwa kwa kufuata kanuni na taratibu za ICAO ili kuepusha matabaka na kufanya alama za utoaji huduma kushuka wakati wa ukaguzi.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dkt. Ally Possi, amesisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu vitendea kazi ikiwemo magari ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kusaidia fedha za ununuzi wa mara kwa mara kuelekezwa kwenye maeneo mengine.


Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Mussa Mbura, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Mamlaka imejipanga kuhakikisha mashirika yanayotoa huduma katika viwanja vya ndege nchini yanaongezeka na hivyo kukuza pato la Mamlaka na Taifa kwa Ujumla.


Waziri Prof. Mbarawa amezindua nembo mpya ya TAA, magari 14 ambayo yanahusisha na magari mawili ya wagonjwa yatakayopelekwa katika Kiwanja cha Ndege cha JNIA Dar es Salaam na Dodoma pamoja na maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika Jengo la Watu Mashuhuri (JNIA).


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi


No comments:

Post a Comment