TUVUNJE UKIMYA, TUZUNGUMZE NA WATOTO KUHUSU AFYA YA UZAZI - DKT. NDOSSI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 21 December 2022

TUVUNJE UKIMYA, TUZUNGUMZE NA WATOTO KUHUSU AFYA YA UZAZI - DKT. NDOSSI

Mkufunzi wa kitaifa wa afya ya uzazi kwa vijana Dkt. Taramael Ndossi  katika kikao cha wadau wa afya  kilichofanyika mkoani Morogoro  akitoa maelezo kuhusu umuhimu wa mzazi kumpatia elimu ya afya ya uzazi mtoto.

Na Faustine Gimu, Morogoro

WAZAZI wameaswa kuvunja ukimya na badala yake waweze kuzungumza na vijana  wao kuhusu afya ya uzazi ili kuepusha madhara yanayoweza kuwapata vijana balehe hapo baadae kutokana na kukosa elimu sahihi ya afya ya uzazi.

Hayo yamebainisha mkoani Morogoro na mkufunzi wa kitaifa wa afya ya uzazi kwa vijana Dkt. Taramael Ndossi katika kikao kilichoandaliwa na wizara ya afya cha kujadili mpango wa kusogeza mahusiano na mawasiliano ya afya ya uzazi baina ya mzazi na mtoto kilichokutanisha wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, asasi za kiraia, taasisi zilizochini ya Wizara ya afya pamoja na wizara za kisekta ikiwemo uwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum.

Dkt. Ndossi amesema asilimia kubwa jamii za kiafrika bado haziko karibu sana kuzungumza na watoto kuhusu masuala ya afya ya uzazi hivyo ni muhimu kuja na mikakati ya pamoja itakayowezesha mzazi kuzungumza na mtoto kuhusu afya ya uzazi kwa ukaribu zaidi.

“Mtu wa kwanza anayeweza kumbadilisha mtoto ni mzazi, bado kuna changamoto ya mawasiliano ya afya ya uzazi kwa watoto na wazazi, mawasiliano ni arts(sanaa), mzazi aweze kuongea na kijana wake kuhusu afya ya uzazi," amesema Dkt. Ndossi.

Aidha, Dkt. Ndossi amebainisha changamoto zinazokwamisha mawasiliano baina ya mzazi na mtoto kuzungumzia masuala ya afya ya uzazi ni pamoja na mila na desturi, umasikini, wazazi kuwa majukumu mengi ya maisha [economic issues], baadhi ya miiko ya imani za kidini pamoja na ukuaji wa sayansi na teknolojia hali ambayo hupelekea mtoto hasa kijana wa rika balehe ashindwe kupata elimu sahihi ya afya ya uzazi kutokana na mabadiliko ya kibailojia hali ambayo hupelekea kijana kutafuta vyanzo vingine vya kupata elimu ya afya ya uzazi ikiwemo mitandao kijamii.

“Hivyo, mtoto anapokosa taarifa sahihi ya afya ya uzazi kutoka kwa mzazi, atakutana na vijana wa rika lake na huko kuna mambo mengi anaweza kupotoshwa na kujiingiza kwenye vitendo hatarishi vya vishawishi ikiwemo kuanza masuala ya kujamiiana katika umri mdogo, pia katika jamii inayomzunguka atakutana na kila aina ya takataka kuna walevi, wastaarab, hivyo changamoto  zinazokwamisha mawasiliano baina ya mzazi na mtoto kuhusu afya ya uzazi ikiwemo changamoto za mila na desturi ni muhimu kuweza kuzitatua,” amesema Dkt. Ndossi.

Nao baadhi ya wadau mbalimbali wa malezi ya watoto akiwemo meneja mpango wa shirika linalotetea afua za malezi ya watoto [Investing in Children and Strengthening their Societies-ICS] Sabrina Majikata kutoka mkoani Shinyanga amesema taarifa anazoweza kuzipata mtoto kutoka mitandaoni zinaweza kumpotosha hivyo ni muhimu kutengeneza mpango wa pamoja wa kuimarisha mawasiliano huku Idd Jengo kutoka chuo kikuu cha Kiislam Morogoro akiipongeza Wizara ya Afya kwa kushirikisha makundi  mbalimbali ya kijamii katika uandaaji wa mpango huo.

“Vijana wanahitaji kuongozwa na wazazi ili wawe na uelewa kuhusu afya ya uzazi, hivyo ni jambo la msingi ili kuwatengeneza hawa watoto kwani kwenye mitandao watoto wanaweza kupata taarifa zisizo sahihi, Wizara ya afya imekuja na mpango huu ambao utatuweka pamoja,” amesema Sabrina.

“Sote tunashuhudia jamii zetu zinavyokabiliwa na masuala ya malezi, vijana hupata changamoto kubwa, Wizara ya Afya kwa kuanza kuandaa program maalum ya mawasiliano ya kuunganisha baina ya wazazi na watoto itasaidia kuleta pamoja na ninaipongeza wizara kwa kuleta makundi mbalimbali ya jamii sisi viongozi wa dini tupo tayari kushirikiana na wizara ya afya,” amesema Idd Jengo kutoka chuo Kikuu cha Kiislam Morogoro.

Naye mwakilishi kutoka halmashauri ya Ilala  Dar Es Salaam Gerwalda Mumba amesema asilimia kubwa wazazi wanakaa na kompyuta na kushindwa kukaa karibu na watoto hivyo mpango huo utasaidia wazazi kuzungumza na watoto kuhusu afya ya uzazi.

“Dunia ya sasa ni utandawazi, wazazi muda wote tupo bize na simu zetu, kompyuta, na hatukai karibu sana na watoto hali ambayo husababisha watoto wajiingize kwenye vyanzo vingine vya kupata taarifa hivyo mpango huu ulioandaliwa na wizara ya afya utarahisisha kuwa karibu na watoto wetu kuzungumzia kuhusu afya ya uzazi,” amesema Mumba.

Ikumbukwe kuwa Mpango huu wa mahusiano na mawasiliano baina ya wazazi na watoto kuhusu masuala ya afya ya uzazi malengo yake ni kuwawezesha watoto kuweza kuongea na wazazi anapokutana na changamoto za afya ya uzazi na kurahishisha kuzungumza na kuleta suluhisho la tatizo na kuleta taifa lenye misingi ya afya imara hasa kwa vijana walioko shuleni.

No comments:

Post a Comment