SERIKALI KUBORESHA SEKTA YA USAFIRISHAJI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 16 December 2022

SERIKALI KUBORESHA SEKTA YA USAFIRISHAJI

Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akisisitiza jambo kwa wahitimu wa kozi mbalimbali za Usafirishaji katika mahafali ya 38 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akimtunuku Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Lojistiki na Usafirishaji Farida Salum katika mahafali ya 38 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

SERIKALI imewahakikishia wahitimu wa kozi mbalimbali za Usafirishaji kuwa itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya usafiri na usafirishaji sambamba na kuzingatia ongezeko la wataalam ili  kuhakikisha miundombinu inasimamiwa kwa kuzingatia weledi

Akizungumza katika mahafali ya 38 ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Nchini (NIT) jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema soko la ajira katika sekta ya usafirishaji limeongezeka sanaa kutokana na maboresho mbalimbali yanayofanywa na Serikali kwenye bandari, ujenzi wa meli, viwanja vya ndege, na ununuzi wa ndege.


“Sekta ya usafiri na usafirishaji inakuwa kila siku na uwekezaji unaendelea kufanywa kwenye miundombinu, nyinyi kama wahitimu mtaweza kupata ajira kwenye maeneo ya reli, bandari na viwanja vya ndege kupitia uwekezaji huu,” amesema Naibu Waziri Mwakibete.


Naibu Waziri Mwakibete ametumia fursa hiyo kuwaasa wahitimu kuzingatia misingi ya uadilifu waliyofundishwa kwani usimamizi wa miundombinu unahitaji nidhamu na uadilifu ili kuifanya iweze kudumu kwa muda mrefu.


Aidha Naibu Waziri Mwakibete ameipongeza NIT kwa kuhakikisha inaongeza kozi katika njia tano za usafirishaji na kupunguza gharama kubwa inayotumia Serikali kwa kuwasomesha wataalam wa fani hizo nje ya nchi.


Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha NIT Profesa Zacharia Mganilwa amesema kwa sasa chuo kimeongeza udahili na kufikisha wanafunzi zaidi ya elfu kumi na mbili kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na wanafunzi elfu sita kwa mwaka 2020.


Profesa Mganilwa ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za kununua ndege  mbili zenye injini moja kwa ajili  ya shule ya usafiri wa anga zitakazosaidia wanafunzi wa urubani na uhandisi wa ndege.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Manonga mkoani Tabora Seif Gulamali ambaye ni mwanafunzi aliyewahi kusoma katika chuo hicho ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa bodi ya usafirishaji ili kuendeleza tasnia hiyo kwa kuzingatia weledi.


Katika Mahafali ya 38 wanafunzi zaidi ya elfu mbili mia saba wametunukiwa shahada za uzamili, shahada, stashahada za juu, shahada na astashahada katika maeneo mbalimbali ya Usafirishaji.


(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

No comments:

Post a Comment