MIRADI YA KIMKAKATI KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 20 December 2022

MIRADI YA KIMKAKATI KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI

 

Baadhi ya watalaam wa masuala ya miundombinu nchini wakipatiwa semina ya utekelezaji wa miradi kwa kushirikisha Sekta Binafsi yaliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), kwa kushirikiana na Chama cha Barabara Tanzania (TARA), jijini Arusha.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Ludovick Nduhiye, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), mara baada ya kufungua semina ya utekelezaji wa miradi kwa kushirikisha Sekta Binafsi iliyofanyika jijini Arusha.

SERIKALI imesema itashirikiana na Sekta binafsi, ndani na nje ya nchi ili kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya Taifa, kiuchumi na kijamii.

 

Hayo yamesemwa jijini Arusha, na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Ludovick Nduhiye, wakati akifungua semina ya siku mbili (2) iliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Barabara Tanzania (TARA), katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC.

 

“Kama nchi tuna miradi mingi inayoendelea kutekelezwa hivyo nia yetu ni kuharakisha miradi hiyo kwa kuhusisha pia Sekta Binafsi hususani kwa miradi ya barabara, madaraja, viwanja vya ndege na miradi mingineyo”, amesisitiza Nduhiye.

 

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema Serikali imetangaza kuanza ujenzi wa barabara kwa kupitia ubia na Sekta Binafsi katika mradi wa barabara ya Kibaha – Morogoro (highway) na barabara ya Igawa – Tunduma mkoani Mbeya. 

 

Amesema semina hiyo ina lengo la kuwajengea uelewa na uwezo wa mambo muhimu kuanzia kuandaa makabrasha ya mradi mpaka utekelezaji wake ambapo wadau muhimu waliohusishwa ni pamoja Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi, TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Mipango ili miradi hii inapoanza kutekelezwa isikwame kwa namna yoyote. 

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Hadija Hamisi Rajabu, amesema miongoni mwa tija za ushiriki wa Serikali ya Mapinduzi ni pamoja na kutatua changamoto ya kukwama kwa miradi kwa kukosa utaalam..

 

“Katika utekelezaji wa miradi kama hii kwa upande wa Sera na Sheria ziko vizuri lakini wakati wa utekelezaji ndipo kunapotokea sintofahamu nyingi kwa kuwa hili jambo hatujalielewa vizuri sana na ndo maana tupo hapa ili kuona wapi tulikuwa tunakosea na namna sahihi ya kuepuka changamoto pindi zinapojitokeza”, amesema Katibu Mkuu huyo. 

 

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Barabara Tanzania (TARA), Bw. Joseph Haule, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa kushirikiana na Wizara ili wataalam waweze kujifunza kutoka katika nchi ambazo wametekeleza miradi kama hii na kupata njia sahihi ya kuepuka makosa yanayoweza kujirudia katika utekelezaji wa miradi hiyo.

 

“Nchi mbalimbali za Latini America na nchi nyingine za Africa ambazo ziliweza kuingia katika miradi kama hii kuna makosa mbalimbali waliyafanya, kutokana na makosa hayo tunataka tujifunze ili tuweze kuyaepuka na hivyo kuhakikisha fedha zitakazotumia katika miradi hiyo ziweze kuleta tija kwa nchi yetu”, amesema Bw. Haule.

 

Semina hiyo imewakutanisha wataalam mbalimbali wa masuala ya miundombinu hapa nchini na baadhi ya wataalam kutoka nchi za Afrika Kusini na Brazil.


 Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

No comments:

Post a Comment