Baadhi ya wanahabari toka vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika warsha hiyo. |
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi amesema mamlaka hiyo inatambua ushirikiano mzuri unaofanywa na vyombo vya habari katika kuripoti habari za utabiri wa hali ya hewa, kwani uelewa wa jamii kufuatilia taarifa za utabiri unaongezeka kila uchao.
Dk. Kijazi ameyasema hayo leo mkoani Pwani, alipokuwa akifungua warsha ya wanahabari kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2022, iliyoandaliwa na TMA kuwajengea uwezo wanahabari juu ya uripoti habari za utabiri.
"Vyombo vya habari vya Tanzania vinafanya vizuri sana katika kuripoti taarifa za utabiri wa hali ya hewa, tunaomba mwendelee kusonga mbele zaidi na hata mfikie namba moja kwa Afrika," alisema Dk. Kijazi.
Alisema TMA itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari na hata kuwajengea uwezo wanahabari juu ya kuripoti kiusahihi na kwa wakati taarifa za utabiri, ili wananchi waweze kunufaika nazo kiusahihi na kwa wakati.
Aidha akizungumzia warsha hiyo ya mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2022 yenye kauli mbiu “matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu”. Aliongeza kuwa warsha hiyo ni juhudi za mamlaka kutaka kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa kwa uhakika, usahihi na kwa wakati.
"...Ni kipindi kirefu sasa tangu tumeanza kutoa warsha kama hizi kwenu wanahabari mara kwa mara kila tunapokaribia kutoa utabiri wa msimu. Kwa hakika matokeo yapo dhahiri kwani kwa kushirikiana nanyi kupitia mafunzo haya, tumeona mwamko na uelewa wa jamii juu ya taarifa za hali ya hewa kuongezeka," alisema.
Alibainisha kuwa kuongezeka kwa mwamko na uelewa kuhusu taarifa za hali ya hewa ni muhimu kwani taarifa hizi zikiifikia jamii kwa wakati, uhakika na usahihi itaisaidia jamii kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
Hata hivyo, inasaidia mamlaka zinazohusika kupanga mipango ya kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa, upatikanaji wa chakula na lishe bora pamoja na afya kwa ustawi wa jamii na hivyo kuchangia katika maendeleo endelevu.
Meneja Miundombinu ya Hali ya Hewa, Samwel Mbuya akifafanua jambo kwenye warsha hiyo kwa wanahabari. |
McSehemu ya wanahabari wakiwa kwenye warsha ya wanahabari kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba 2022. |
No comments:
Post a Comment