Na Abby Nkungu, Dodoma
SERIKALI imesema itaendelea kuweka mifumo rafiki ya uwekezaji kwa watoto kupitia programu mbalimbali;
ikiwemo Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali
ya Mtoto (PJT-MMMAM) ya miaka mitano iliyozinduliwa Desemba mwaka jana.
Ahadi hiyo ilitolewa Jijini hapa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi maalum, Dk Dorothy
Gwajima wakati akizindua mafunzo ya Kitaifa ya Sayansi ya Malezi, Makuzi na
Maendeleo ya Awali ya Mtoto (SECD).
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Children in Crossfire
(CiC), UTPC na Chuo Kikuu cha Aga Khan yanahudhuriwa na Waandishi habari vinara
wa kuandika habari za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM),
Maofisa Maendeleo ya Jamii, Maofisa Ustawi wa Jamii, Mashirika yasiyokuwa ya
Kiserikali (CSOs) na Mtandao wa Makuzi, Malezi
na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania (TECDEN).
Alisema kuwa ili kufanikisha uwekezaji timilifu kwa mtoto nchini Serikali
haina budi kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kuboresha kundi hilo kwa kuweka mifumo rafiki ya
uwekezaji.
Aidha, alisema kuwa Serikali inataraji mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya
habari kitaifa na kimataifa katika kuhakikisha kuwa jamii inapata uelewa mzuri
na taarifa sahihi kuhusu Sayansi ya Malezi na Makuzi ya Mtoto.(SECD) kutokana
na idadi ya Waandishi habari kutoka kila mkoa nchini kushiriki mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Shirika la Children in
Crossfire (CiC), Craig Ferla alisema kuwa Programu Jumuishi ya Taifa kuhusu
Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inachochea kwa kiasi kikubwa
utekelezaji wa mipango mbalimbali kwenye sekta za ECD.
Akitoa salamu za Muungano wa Klabu za Waandishi wa habari Nchini (UTPC) kwa
niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Victor
Maleko alieleza kuwa tangu mwaka 2019 kupitia klabu 28 zilizopo, Waandishi
habari wamekuwa wakihabarisha umma kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambapo
tangu kuzinduliwa kwa programu hiyo miezi 6
iliyopita, zaidi ya habari 400 zimeripotiwa.
Lengo la mafunzo hayo ya siku sita yanayoendelea Ukumbi wa St Gaspar jijini
hapa ni kuongeza uelewa na uwajibikaji kwa wadau wote ili waone umuhimu wa
kuwekeza kwenye huduma bora za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
No comments:
Post a Comment