Ikiwa ni takribani wiki tatu zimesalia kuelekea NBC Dodoma International Marathon itakayofanyika siku ya jumapili Julai 31, wanariadha wameendelea kujifua ili kushiriki mbio hizo za kimataifa.
-
Leo tumeshuhudia klabu za wanariadha ya Kigamboni runners ikishirikiana na klabu ya wanariadha ya NBC Jogging club ambao wamefanya mazoezi ya pamoja kwa kukimbia kilomita 10 na kilomita 5 ikiwa sehemu ya maandalizi ya kuelekea mkoani Dodoma.
-
Akizungumzia maandalizi kwa ujumla, Msemaji wa NBC Jogging Club, Johnson Ngakiziba alisema lengo ni kuhakikisha wanariadha wanapata muda wa kutosha kujiandaa vizuri kuelekea kwenye mbio hizo ambazo pia zitashirikisha wanariadha kutoka nje ya nchi.
“Tumeungana na wenzetu wa Kigamboni Runners ili kufanya maandalizi ya pamoja kwaajili ya NBC Dodoma International Marathon.Lakini pia, wenzetu hawa walikuwa wanaadhimisha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa klabu hii kwahiyo tukaona tuungane kwa pamoja,” alisema.
-
Mbio za NBC Dodoma International Marathon zitahusisha wakimbiaji wa Kilomita 42, 21 na kilomita 10 ambapo benki hiyo imetenga jumla ya Sh65 milioni kama zawadi kwa vinara huku watanzania wakipewa kipaumbele zaidi kupitia nyongeza (Bonus).
-
Hadi kufikia leo Julai 7, mauzo ya tiketi za kilomita 10 yalikuwa yamefikia asilimia 80 ikiwa ni siku chache tu tangu kutangazwa kwa mbio hizo.
“Nawakumbusha watu waendelee kujisajili mapema ili kuepuka changamoto na kujisajili ni rahisi sana, tembelea tovuti ya www.events.nbc.co.tz na utalipia tiketi kwa njia mbalimbali ikiwamo NBC Kiganjani,” alisema.
-
Kwa upande wake, Katibu wa Kigamboni Runners, Edgar Konyani alisema mapokeo yamekuwa mazuri kwa wakimbiaji wa klabu hiyo ambapo wamekuwa wakishiriki kwa mara ya tatu mfululizo.
-
Mbio za Dodoma International Marathon zimelenga katika kuchangia mapambano dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi (cervical cancer) kwa kushirikiana na taasisi ya Ocean Road ambapo fedha zitakazokusanywa zitapelekwa kwenye taasisi hiyo.
No comments:
Post a Comment