KIKOKOTOO KILIVYOLETA KICHEKO KWA WASTAAFU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 6 June 2022

KIKOKOTOO KILIVYOLETA KICHEKO KWA WASTAAFU

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu.

WASTAAFU sasa watacheka kutokana na kukamilika kwa kanuni mpya ya pensheni ya mafao ya wastaafu (kikokotoo) inayoongeza kiwango cha mkupuo kutoka asilimia 25 iliyokataliwa mwaka 2018 hadi 33. Itaanza kutumika kwa Julai Mosi, 2022.

Kikokotoo ni kanuni inayotumika kuwezesha upatikanaji wa mafao ya mkupuo na pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu.

Akitoa taarifa kwa umma kuhusu kanuni mpya mjini Dodoma hivi karibuni, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu, anasema: “Kanuni mpya inaongeza kiwango cha malipo ya mkupuo kutoka asilimia 25 iliyokataliwa mwaka 2018 hadi asilimia 33 kwa wanachama 1,364,050 sawa na asilimia 81 ya wanachama wote (1,690,187) wa mifuko na inaongeza pensheni ya mwezi kwa wanachama.”

Ushuhuda uliotolewa mbele ya wandishi wa habari jijini Dodoma na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya; Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba-Doran na Kaimu Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Dinna Mathamani, unabainisha kuwa, serikali chini ya Rais Samia, ni sikivu maana kanuni hiyo imetokana ushiriki na makubaliano ya wadau wote.

FAIDA KWA WOTE

Katibu Mkuu anasema: “Michango ya mwanachama kwenye mifuko ya pensheni itaendelea kuwa kama ilivyokuwa kabla ya kanuni (kikokotoo) mpya kutolewa.”

Imebainika kuwa, kupitia kanuni mpya, watumishi wa umma wanaotumia mfuko wa PSSSF, michango itaendelea kuwa asilimia 15 kwa mwajiri na asilimia 5 kwa mwanachama; na wanachama wa NSSF michango itaendelea kuwa asilimia 10 kwa mwajiri na asilimia 10 kwa mwanachama.

Mkurugenzi wa Hifadhi ya Jamii katikaWizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Festo Fute, yeye, anasema: “Kanuni mpya itawezesha mifuko kulipa mafao kwa wakati na kwa uendelevu.... Kupitia kanuni mpya, wastaafu watafaidika kwa kuwa na pensheni bora kwa ustawi wao.”

Ifahamike kuwa, malipo ya pensheni yaliyokuwa yakitumika awali, yalitoa nafasi kwa wastaafu kupata mkupuo mkubwa, lakini yakawapa pensheni ndogo ya kila mwezi isiyotosheleza mahitaji ya kila siku kwa kuwa, malipo ya mkupuo waliyatumia katika matumizi ya muda mfupi na uwekezaji usio endelevu.

Kamishina wa Tume ya Haki za Binadamu, Nyanda Shuli anasema: “Pensheni mpya itaondoa utofauti kwa wastaafu ambapo baadhi walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 25 wakati wengine walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 50. Kanuni mpya ya malipo ya pensheni imeondoa tatizo la utofauti lilikuwepo na sasa mifuko ya pensheni yote inazungumza lugha moja.”

                                                                MADHARA YA MKUPUO MKUBWA WA PENSHENI

Nyanda anasema: “Unapoochukua kiasi kikubwa kwa mkupuo mmoja, ndivyo utakavyopata pensheni ndogo ya kila mwezi na kusababisha ugumu katika maisha yako...”

Mkurugenzi wa Uthamini, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Ansgar Mushi, yeye anasema: “Unapopokea mkupuo mkubwa, unaangukia kwenye kundi la wastaafu wanaopokea kiasi kidogo cha pensheni ya kila mwezi huku kile ulichopata kwa mkupuo mkubwa kikiwa kimeisha na mahitaji bado yako palepale…”

Anasema matokeo ya hali hiyo, ni kile kinachodaiwa na baadhi ya watu kuwa, watu wengi hufa baada ya kustaafu.

“Mtu anakuwa amepata pesa nyingi kwa pamoja na zimekwisha ndani ya muda mfupi bila kufanya la maana na endelevu…,” anasema.

Katika mazungumzo na wachechemuzi mkoani Dar es Salaam kuhusu kanuni npya, Mushi anaongeza: “Katika jamii zetu wastaafu wengi bado wana changamoto ya kujilea na hata kusomesha na kutunza watoto na wajukuu, badala ya wao kutunzwa.”

 “Sasa kama fedha zako ulizimaliza katika mkupuo mmoja na zikaisha, unabaki na kipindi kigumu katika maisha yote kwa kuwa hata pensheni unayopata kwa mwezi ni mdogo na hatoshelezi mahitaji maana uliimaliza katika mkupuo mmoja.”

Anasema, malipo kidogo ya mkupuo huwahakikishia maisha bora wastaafu baada ya mkupuo wa kwanza kuisha kwa kuwa hutoa mwanya wa pensheni kubwa ya kila mwezi na kwamba tamaa ya kupata malipo makubwa katika mkupuo wa pensheni, huwafurahisha wasiojua kabla ya kupokea, lakini baadaye huwatoa machozi na kuwapa majuto wastaafu wengi.

FAIDA YA MKUPUO MDOGO

“Faida ya kupata mkupuo mdogo ni kwamba, unakuhakikishia mstaafu usalama na uendelevu wa pensheni kubwa ya kila mwezi kuliko anayechukua mkupuio mkubwa maana yeye anabbaki na pensheni ya kila mwezi isiyofua dafu katika mahitaji.

Faida nyingine ya kikokotoo kipya ni kuongeza pensheni ya mwezi kutoka asilimia 50 hadi asilimia 67 kwa waliokuwa wanachama wa mifuko ya PSPF na LAPF ambao ni asilimia 19 ya wanachama wote wa mifuko.

                                                              

Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Suzanne Ndomba- Doran.

  WANAOCHUKUA MKUPUO MKUBWA ANAVYOJUTA

Lusajo Mwakabuku kutoka Idara ya Mawasiliano kwa Umma, Ofisi ya Waziri Mkuu, anasema wastaafu wengi wamepata majuto kwa kupokea malipo makubwa ya pensheni kwa mkupuo kwa kuwa waliingia katika mipango na biashara iliyotokana na msukumo wa pesa, badala ya malengo ya pensheni kuwasaidia kupata mahitaji endelevu katika maisha.

“Fikiria mtu ambaye tangu azaliwe hawajawahi kushika hata Sh milioni 20 zake binafsi, leo anastaafu, anapata Sh milioni 100, 150, au milioni 200 kwa mkupuo; matokeo yake, kwanza anaoa vibinti; anainghia kwenye biashara asiyojua kama kununua daladala na huku akila starehe nyingine, matokeo yake, baada ya miezi takriban sita, pesa hakuna; imekwisha na pensheni ya mwezi ni kidogo maana alichukua mkupuo mkubwa; inakuwa ni tabu katika maisha yake yote…” anasema Lusajo.

FAIDA ZAIDI

Wadau mbalimbali wa hifadhi ya jamii wanasema kupitia kikokotoo kipya, mifuko ya pensheni ya PSSSF na NSSF sasa itaimarika zaidi na kuwa endelevu.

Kwamba, kupitia kikokotoo kipya kitakachoanza kutumika Julai 1, mifuko pia inaweza kuhuishwa na kuongeza pensheni ya kila mwezi kwa kuzingatia thathmini zitakazofanyika kila baada ya miaka mitatu.

Kwa nyakati tofauti, Profesa Katundu na Fute wanabainisha kuwa, kikokotoo kinachotumika sasa hakina uwiano na michango ya 20 ya wanachama na kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa mfuko wa PSSSF kushindwa kulipa mafao ifikapo mwaka 2034.

HATARI KUBWA

“Hii ilikuwa inaleta hatari kwa wanachama kuwa, ili mfuko huu (PSSSF) uendelee kulipa mafao, inabidi sasa michango ya wanachama na waajiori iongezeke kutoka silimia 20 ya sasa hadi 25. Kimsingi, ongezeko hili lingeongeza mzigo wa makato ya mishahara kwa wafanyakazi,” alisema Katibu Mkuu Katundu.

Kuhusu mfuko wa NSSF, ilibainika kuwa sehemu kubwa ya fedha inatumika kulipa mafao ya kukosa ajira ambayo si lengo kuu la mfuko.

“Kwa msingi huo, “ Fute anasema: “Mfuko wa NSSSF ulikuwa hatarini kushindwa kulipa mafao kwa kutumia kiwango cha sasa cha michango ifikapo mwaka 2042.”

Anaongeza: “Sasa ili kuendelea kulipa mafao, michango ya wanachama pamoja na mwajiri ilikuwa inalazimu kuongezwa kutoka asilimia 20 ya sasa hadi asilimia 23.2.”

Kimsingi, serikali kupitia katibu Mkuu, Profesa Katundu, inasema lengo lake kuu kuunda kanuni (kikokotoo) mpya, ni kuhakikisha wastaafu wanakuwa na hali endelevu ya maisha iliyo bora baada ya kustaafu kwa kuwapa uhakika wa mahitaji muhimu

No comments:

Post a Comment