RUVUMA WAADHIMISHA MIAKA 58 YA MUUNGANO KWA KUFANYA USAFI NA MAZOEZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 27 April 2022

RUVUMA WAADHIMISHA MIAKA 58 YA MUUNGANO KWA KUFANYA USAFI NA MAZOEZI

 

KULIA MWAKILISHI WA MKUU WA MKOA WA RUVUMA MHE.POLOLET MGEMA AKIFANYA USAFI NDANI YA SOKO KUU LA SONGEA SIKU YA MAADHIMISHO  YA MIAKA 58 YA MUUNGANO.

MKOA wa Ruvuma umeadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya mazoezi  na  usafi wa mazingira  katika  Wilaya zote.

Akizungumza kwenye viwanja vya Soko Kuu la Songea, baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi Manispaa ya Songea,Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Pololet Mgema  aliwataja waasisi wa Muungano kuwa walipigania Uhuru wa nchi yetu na kufanikiwa kuunganisha nchi mbili kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

”Muungano wetu umedumu kwa miaka 58,na umeendelea kuimarika,amani na umoja tulionao leo watanzania ni matunda ya waasisi wa Taifa letu tunawashukuru sana ’’,Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

 Maadhimisho hayo yaliaanza saa 12:30 Asubuhi kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuanza na mazoezi ya kukimbia kuelekea katika maeneo ya kufanya usafi katika masoko mawili ya Manzese na Soko kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Akizungumzia usafi wa mazingira,Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kuendelea kufuata utamaduni wa kufanya usafi katika maeneo wanayoishi na wanayofanyia biashara na kwamba usafi ni ishara ya tabia njema kuufanya mji wa Songea kupendeza.

“Sisi wanaruvuma tulikwishajiwekea utamaduni wa kufanya usafi siku zote katika maeneo yetu, na maeneo ya umma lakini Ndugu zangu siku za karibuni utamaduni huo umeanza kufifia ndio maana tukasema tutumie siku ya leo kukumbushana wajibu wakufanya usafi”, alisisitiza. 

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa  amewahimiza wananchi kufanya usafi  kila siku ili kuepuka magonjwa yatokanayo na uchafu  na kwamba gharama za matibabu ziko juu hivyo ni vyema kujijengea tabia ya kufanya usafi  maeneo ya kuishi na maeneo ya kazi ili kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya kuambukiza. 

Pia amesisitiza kufanya  mazoezi ya viungo  kila Jumamosi  ili  kuendelea kulinda afya  na kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kila kisukari na shinikizo la damu.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa  wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki akizungumza kwenye maadhimisho hayo alisema kila mwaka Siku ya Muungano imekuwa ikiadhimishwa kwa  kufanya shughuli mbalimbali ambapo mwaka huu katika Mkoa wa Ruvuma siku hiyo imeadhimishwa kwa kufanya usafi wa mazingira na mazoezi.

Amesisitiza wananchi kuendelea kufanya usafi wa mazingira kila siku badala ya kusubiri Siku ya Muungano ambapo amesema katika masoko ya Manispaa ya Songea hali ya usafi hairidhishi hivyo ameagiza wananchi wote kufanya usafi.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Philipo  Beno alisema uzalishaji wa taka katika Manispaa ya Songea umeongezeka  na unakadiriwa kufikia  tani 80 kwa siku wakati uwezo wa Halmashauri kuzoa taka ni tani kati ya 50 hadi 60 kwa siku. 

Hata hivyo amesema Manispaa ya Songea imejipanga na kuweka mikakati ya kuhakikisha taka zote zinazolewa kila siku kwa kuongeza magari ya kuzolea taka na kuanzisha kampuni binafsi ya kuzoa taka.

Maadhimisho ya Muungano yametimiza miaka 58 toka kuunganishwa kwa nchi mbili kati ya Tanganyika na Zanzibar chini ya waasisi  Mwl. Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

No comments:

Post a Comment