Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Na Dotto Mwaibale, Manyoni
OFISI ya Mkuu wa Mkoa Singida na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) wamekutana wilayani Manyoni mkoani hapa kutatua changamoto ya wakulima ambao walilipa fedha zao miaka mitatu iliyopita kwa ajili ya kilimo cha zao la korosho katika wilaya hiyo lakini hadi leo hii bado hawajapatiwa mashamba yao.
Kikao hicho kinafanyika kufuatia agizo la Waziri wa Kilimo alilolitoa Aprili 9 mwaka huu kutaka wakutane wakulima hao, bodi ya korosho na ofisi ya mkuu wa mkoa ili kumaliza sintofahamu ya jambo hilo
Mashamba waliotakiwa kupewa yapo Itigi-Njilii, Kaminyange, Masigati na Mkwese ambapo kuna makundi manne ya wakulima ambao wapo kwenye mgogoro huo ulianza kutatuliwa na Serikali mkoani hapa kwa kushirikiana na bodi ya korosho.
Makundi hayo ni la wakulima ambao walilipia mashamba hayo na wameanza kulima, wapo wenye mashamba lakini ni mapori, wapo wenye mashamba lakini hawajakabidhiwa rasmi na wale ambao walilipia lakini wapowapo tu na hawajui hatima yao.
Katika kikao hicho baadhi ya wakulima walipewa nafasi ya kujieleza na kutoa masikitiko yao ya kupoteza muda mwingi wakisumbuliwa kwa zaidi ya miaka mitatu bila ya kupewa mashamba hayo licha ya kutoa fedha zao Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge alisema maazimio yaliyofiwa ni ndani ya mwezi mmoja mvutano huo uwe umemalizika na kabla ya Oktoba 1, 2022 wakulima wote waliolipia fedha zao na kukamilisha taratibu zote wakabidhiwa mashamba yao na kuanza kulima.
Alitaja jambo lingine kuwa kutumika kwa akaunti moja ya mradi huo na kuundwa kwa kamati mpya itakayosimamia baada ya zile mbili za awali kuvunjwa na kuomba wahusika wa kamati hizo zilizovunjwa kutoa ushirikiano kwa kamati mpya na watakaoonekana wanashindwa kutoa ushirikiano watachukuliwa hatua.
Alisema suala hilo litasimamiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko kwa kushirikiana na kamati itakayoundwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile aliwashukuru wajumbe wa kikao hicho kwa kuwa wawazi na kueleza kuwa kilikuwa kikao cha kujua changamoto zilizokuwepo.
Alisema jambo lililomtia moyo ni hatua aliyoichukua mkuu wa mkoa na timu yake yakulimaliza jambo hilo ndani ya mwezi mmoja na kuwa kilimo cha zao hilo licha ya kupunguza umasikini wa mtu mmoja mmoja kinakwenda kuongeza pato la taifa hivyo aliwasihi baadhi ya wakulima waliofikia hatua kudai warudishiwe fedha zao kuacha kufanya hivyo na akasema watendaji wote waliohusika kwa namna moja hama nyingine kuchangia changamoto hiyo wamesamehewa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred akizungumza kwenye kikao hicho alisema tayari baadhi ya kazi alizoagizwa kuzitekeleza kama ujenzi wa kisima cha maji baridi kwa ajili ya kumwagilia miche ya korosho watakayokuwa wakiizalisha Naliendele Mtwara mchakato wake umefanyika ukiwepo wa ujenzi wa ghara la kisasa la kuhifadhi korosho litakalo jengwa wilayani Manyoni.
Mkulima Abdallah Mbonde akizungumza kwa niaba ya wenzake ameshauri kamati itakayoundwa ihakikishe haki inatendeka ili wakulima waweze kuendelea na uwekezaji katika kilimo hicho kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
No comments:
Post a Comment