MAUAJI, KUJIUA YAZIDI KUIKERA PROLIFE - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 17 April 2022

MAUAJI, KUJIUA YAZIDI KUIKERA PROLIFE

Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania, Emil Hagamu.

VITENDO vya mauaji na watu wengine kujiua vimezidi kuwa kero kwa jamii hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (PROLIFE) Tanzania, Emil Hagamu, kuwataka Watanzania kukitumia kipindi cha Sikukuu ya Pasaka kujitathmini na kuvikomesha.

Katika mazungumzo yake Dar es Salaam jana kuhusu maadhimisho ya Sikukuu ya Kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka) yanayofanyika leo, Hagamu alisema: “Tutumie kipindi kilichomalizika cha Mfungo wa Kwaresma na kuitumia Pasaka hii kutenda haki kwa kila mtu na kuepuka mambo yote ambayo ni vyanzo vya ukosefu wa haki ya kuishi kwa watu yakiwamo mauaji dhidi ya watoto ambao hawajazaliwa yaani utoaji mimba na vitendpo vya watu kujiua.”

Alisema katika siku za karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya mauaji na watu kujiua yakiwamo yaliyotokea Kigoma na Geita.

Februari 3, 2022, mwanamke mmoja Naomi mkazi wa Katoro, Geita, alikutwa amejinyonga ndani ya choo cha nyumba ya kulala wageni inayomilikiwa na mumewe. Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe.

Katika tukio la hivi karibuni, polisi mkoani Kigoma walimtia mbaroni Lenita Asheri (54) akituhumiwa kumnyonga mjukuu wake baada ya kuzaliwa Aprili 9, 2022 na kisha kutupa mwili wake chooni akilenga kuficha ushahidi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, James Manyama alisema baada ya bibi huyo kuhojiwa, alisema alifanya hivyo ili kuondoa mzigo wa kumtunza mtoto huyo ambao ulikuwa unamkabili yeye kwa kuwa mama wa mtoto hana uwezo na kwamba ana changamoto za afya ya akili.

Kwa mujibu wa Hagamu, baadhi ya vyanzo vya mauaji katika jamii ni pamoja na tamaa ya kupata utajiri wa harakaharaka, imani potofu za ushirikina, kukosekana kwa upendo, mapigano, dhambi ya watu kukata tamaa, pamoja na uzinzi na uasherati mambo yanayochochea zaidi mauaji kupitia utoaji mimba.

“Haya na mengine utaona yanawalenga zaidi wanyonge wakiwamo watoto wasioweza kujitetea, vikongwe na watu maskini… Kipindi cha Pasaka kitusafishe na kutubadili kutoka kwenye utamaduni wa kifo, kwenda kwenye utamaduni wa uhai maana uhai ni zawadi ya Mungu kwa wanadamu; wote tuseme chuki, dhuluma, vita na mauaji hata ya watu kujiua, sasa basi,” alisema.

Alisema kwa namna na sababu yoyote ukatili ukiwamo utoaji mimba na vitendo vya watu kujiua haupaswi kupata nafasi katika jamii kwa kuwa ni kinyume cha mapenzi ya Mungu na sheria za nchi.

Katika miezi ya karibuni, kumekuwapo taarifa za mara kwa mara za mauaji dhidi ya watoto wadogo, mauaji dhidi ya wanandoa, watuhumiwa wa makosa mbalimbali kutokana na watu kujichukulia sheria mikononi, mauaji yanayofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya wanawake baada ya kuwabaka na pia mauaji ya watu kujiua kutokana na sababu mbalimbali.

Akikemea vitendo vyote vinavyochangia kuwapo kwa utoaji mimba, Hagamu alisema hata inapotokea tatizo la kiafya kwa mjamzito, juhudi zote za wataalamu zilenge kuokoa maisha ya mama na mtoto na si kutaka kuua mtoto ili kuokoa maisha ya mama.

No comments:

Post a Comment