ENG. KASEKENYA AWATAKA TAZARA KUJIPANGA UPYA - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 29 December 2021

ENG. KASEKENYA AWATAKA TAZARA KUJIPANGA UPYA

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia –TAZARA (hawapo pichani), alipokagua karakana Kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa TAZARA, Eng. Christopher Shiganza.

Naibu Mkurugenzi wa TAZARA, Eng. Christopher Shiganza (katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya alipokagua karakana Kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam.

Muonekano wa kichwa cha treni (locomotive) kilichokarabatiwa katika Karakana Kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Karakana Kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam, Bw. Jumanne Mnyawami (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya moja ya behewa lililokarabatiwa kwenye karakana kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Karakana Kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam, Bw. Jumanne Mnyawami (kulia) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya alipokagua karakana Kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia –TAZARA, alipokagua karakana Kuu ya TAZARA jijini Dar es Salaam.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya ameitaka Menejimenti ya Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), kubuni mikakati ya kibiashara inayoweza kutekelezeka na kupimika ili kuliwezesha shirika hilo kutoa huduma bora na kupata faida, kama ilivyokusudiwa awali.

Akizungumza mara baada ya kukagua karakana Kuu za TAZARA jijini Dar es Salaam, Eng. Kasekenya amesema ni wakati sasa kwa kila mwenye dhamana katika TAZARA kufanya kazi kwa kuzingatia maono ya waasisi wa reli hiyo.

“…Tunao mzigo wa kutosha wa kusafirisha kwa reli ya TAZARA hivyo hakikisheni mnakuja na mkakati wa kibiashara utakaowezesha kuwa na vichwa vya treni na mabehewa yanayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa,” amesisitiza Eng. Kasekenya.

Amezungumzia umuhimu wa karakana zote zilizopo kufanya kazi kikamilifu ili kupunguza msongamano wa mabehewa na vichwa vya treni vinavyotakiwa kukarabatiwa.

Aidha ameitaka menejimenti ya TAZARA kushirikiana na wafanyakazi katika hatua zote ili kuongeza ari ya kufanya kazi pamoja na kutoa huduma zenye tija na kuvutia wasafirishaji na abiria.   

Naye Naibu Mkurugenzi wa TAZARA, Eng. Christopher Shiganza amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya, kuwa TAZARA wamejipanga kuhakikisha wanapata vichwa vya treni na mabehewa ya kisasa ili kuongeza tija katika huduma hiyo.

Ameiomba Serikali kuboresha sheria ya TAZARA ili kuimarisha umoja baina ya nchi wanachama na kuleta tija na ufanisi mkubwa katika huduma za uchukuzi. 

Reli ya TAZARA inayoanzia Dar es Salaam, (Tanzania) hadi Kapirimposhi (Zambia), ilijengwa mwaka 1970 hadi 1975 kwa ushirikiano wa mataifa ya Tanzania na Zambia na imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na udugu kati ya mataifa hayo mawili, ikiwa ni juhudi za waasisi wa mataifa hayo Mwl. Julias Nyerere na Mzee Keneth Kaunda.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

No comments:

Post a Comment