TUTAONDOA MATATIZO SUGU KUPITIA MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA VYAMA VYA USHIRIKA-WAZIRI MKENDA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 17 September 2021

TUTAONDOA MATATIZO SUGU KUPITIA MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO YA SHERIA YA VYAMA VYA USHIRIKA-WAZIRI MKENDA

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda.

Na Mathias Canal, Dar es Salaam

SERIKALI imesema kuwa kumekuwa na mitazamo tofauti miongoni mwa wadau kuhusu sababu ya kuwepo kwa changamoto na matatizo sugu ya ushirika na namna ya kushughulikia na kutatua changamoto hizo.

Wadau wengi wa Ushirika nchini wamekuwa na mtazamo wa kwamba changamoto na matatizo sugu ya Ushirika nchini yanatokana na sababu mbalimbali na miongoni mwa sababu hizo ni mapungufu ya sheria inayosimamia sekta ya ushirika nchini, ambapo sheria hiyo ni ile ya Vyama vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa sasa serikali imekuja na muarobaini wa kutatua changamoto hizo.

Ameyasema hayo leo tarehe 17 Septemba 2021 Jijini Dar es salaam wakati akifungua kikao cha wadau wazoefu wa ushirika kujadili mapendekezo na marekebisho ya sheria ya vyama vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013.

Waziri Mkenda amesema kuwa kufuatia mtazamo wa wadau na dhamira ya kutatua changamoto sugu za ushirika zinazotokana na mapungufu ya sheria, Mwaka 2019 serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilielekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuanza mchakato wa kufanya mapitio ya Sheria ya Vyama Vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013.

Katika mkutano huo Waziri Mkenda amempongeza Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson Ndiege kwa kufanikiwa kuwaalika wadau wote wazoefu katika kikao hicho kwa ajili ya kutoa maoni.

Kadhalika, Waziri Mkenda ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na Wizara ya Kilimo kuhakikisha kuwa maoni yatakayotolewa na wadau katika kikao hicho yanazingatiwa katika mchakato wa marekebisho ya sheria ya Vyama vya Ushirika unaoendelea.

No comments:

Post a Comment