MVUA ZA VULI KUPUNGUA MSIMU HUU, TMA YATOA USHAURI...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 2 September 2021

MVUA ZA VULI KUPUNGUA MSIMU HUU, TMA YATOA USHAURI...!

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa akizungumza na waandishi wa habari akitoa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli za Oktoba hadi Disemba 2021. Kushoto ni Meneja wa Kituo cha Huduma za Utabiri wa TMA, Samuel Mbuya.

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) akitoa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli za Oktoba hadi Disemba 2021. Kushoto ni Meneja wa Kituo cha Huduma za Utabiri wa TMA, Samuel Mbuya akifuatilia.

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa (katikati)  akisisitiza jambo alipokuwa akitoa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli za Oktoba hadi Disemba 2021.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo imetoa utabiri wa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli za Oktoba hadi Disemba 2021, huku ikibainisha kuwa maeneo mengi ya nchi kwa ujumla mvua zitakuwa za chini ya wastani hadi wastani. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akitoa utabiri huo, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa amesema kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, huku mvua hizo zikianza kwa kusua sua. 

Hatahivyo, alisema vipindi vya ongezeko kidogo la mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache kwa kipindi cha mwezi Disemba, 2021 huku vipindi vya joto kali kuliko kawaida vikitarajiwa katika msimu wa mvuli, hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki.

Alisema mikoa inayotarajia kuathiriwa na hali hiyo ni pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki, yaani Arusha, Manyara na Kilimanjaro, pwani ya kaskazini mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani na visiwa vya Mafia, Dar es Salaam na Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Maeneo mengine ni pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Wilaya za Kibondo na Kakonko.  

Aidha Dk. Kabelwa alisema mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa pia katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, magharibi mwa mkoa wa Shinyanga pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, huku maeneo ya mikoa ya Simiyu, Mara na mashariki mwa mkoa wa Shinyanga yakitarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2021 na kuisha katika mwezi Januari, 2022.

"...Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani, ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba; Mvua zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini. Msimu unatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba,2021. Aidha, katika mkoa wa Morogoro kuanza kwa msimu kunatarajiwa kuwa kwa kusuasua kutokana na kuwepo kwa vipindi vingi vya ukavu. Mvua katika ukanda wa pwani ya kaskazini zinatarajiwakuisha katika mwezi Januari, 2022. Alisisitiza Dk. Kabelwa.

Mvua zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki, yaani Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro na pia msimu utaanza kwa kusuasua katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba, 2021 huku ukitawaliwa na vipindi virefu vya ukavu, mtawanyiko na muendelezo usioridhisha katika maeneo mengi.

Akitaja athari zinazoweza kujitokeza, Dk. Kabelwa alisema ni pamoja na upungufu wa unyevunyevu katika udongo kwa maeneo mengi na magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama, na upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza kwa wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Maradha mengine ni pamoja na uwezekano wa kutokea matukio ya moto katika mapori na misitu, hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo alizitaka mamlaka katika sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Uvuvi, Utalii na Wanyamapori, Usafiri na Usafirishaji,  pamoja na sekta ya Nishati, Maji na Madini kujipanga kukabiliana na athari zozote zinazoweza kusababisha changamoto katika sekta zao ili kupunguza madhara kujitokeza.

MWELEKEO WA MSIMUWA MVUA ZAOKTOBA – DISEMBA,2021(VULI)




No comments:

Post a Comment