KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU KUENDESHA MBIO MTANDAONI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 14 September 2021

KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU KUENDESHA MBIO MTANDAONI

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Bi. Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari kuzungumzia mbio maalum zinazokwenda kwa jina la 'Haki Marathon' ambapo wadau watakimbia kivyao kila mmoja na kuratibiwa kwa kutumia mtandao maalum. Kulia ni Mkurugenzi Mjengaji Uwezo na Uwajibikaji, Bi. Felister Mauya.

Mratibu wa Haki Marathon, Deus Ntukamazina akizungumza na waandishi wa habari kuzungumzia mbio maalum za 'Haki Marathon' ambapo wadau watakimbia kivyao kila mmoja na kuratibiwa kwa kutumia mtandao maalum.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Bi. Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari kuzungumzia mbio maalum zinazokwenda kwa jina la 'Haki Marathon' ambapo wadau watakimbia kivyao kila mmoja na kuratibiwa kwa kutumia mtandao maalum.

Na Mwandishi Wetu

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezinduwa mbio maalum zinazokwenda kwa jina la 'Haki Marathon' ambapo wadau watakimbia kivyao kila mmoja na kuratibiwa kwa kutumia mtandao maalum. Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Bi. Anna Henga amesema mbio hizo zitafanyika kwa njia ya mtandao kuanzia Oktoba 17 hadi Desemba 10, 2021.

Wakili, Bi. Henga amesema mbio za 'Haki Marathon' zinalenga kutafakarisha umma wa Watanzania juu ya jukumu la kila mmoja kulinda na kuheshimu haki za binadamu, hasa tunapojiandaa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ambayo itaadhimishwa ulimwenguni kote Desemba 10, Desemba 2021.

"...Wazo la kufanya Marathon kwa njia ya mtandao limekuja kama sehemu ya mkakati wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wa kujenga uelewa na kuwawezesha Watanzania kutambua wajibu wao wa kulinda haki za binadamu nchini. Na ukizingatia; janga linaloendelea la UVIKO 19 limelazimisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuratibu Marathoni kwa njia tofauti kwa kuzingatia miongozo ya kiafya inayohimiza kuepuka misongamano mikubwa. Alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji wa LHRC, Wakili Bi. Henga.

Aidha akifafanua zaidia amebainisha kuwa mbio zitatoa fursa kwa mtu yeyote aliyepo popote ndani au nje ya nchi kushiriki ili mradi tu awe amejisajili na kulipia kiingilio, huku akichagua kukimbia kwa kasi atakayochagua na kwa wakati watakaochagua mwenyewe.

"Zaidi ya watu 1,000 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizi na baada ya kumaliza mbio, washiriki kutegemeana na eneo waliopo wataelekezwa wapi na wakati gani wa kwenda kupokea medali zao," alisema na kuongeza kuwa; Haki Marathon itakuwa na makundi matatu ya mbio ambayo ni Kilometer 21, Kilometa 10 na kilometer 5 huku mshiriki akipewa fursa ya kuchagua. 

Pamoja na hayo aliongeza kuwa mbio hizo zitaleta chachu kwa jamii kutafakari namna ya kupambana na matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kwani Kwa mujibu wa ripoti ya Haki za Binadam ya mwaka 2020 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania Ukatili dhidi ya wanawake na watoto umeongezeka suala ambalo linahitaji ufumbuzi.

"Kwa mujibu wa taarifa hiyo, matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yaliyotolewa na vituo cha Polisi nchini yalikuwa ni 26,544 ikilinganishwa na mwaka 2019 ambapo matukio yalikuwa ni 23,685. Hili ni ongezeko la asilimia 5.7%. Pia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi viliongezeka. Kwa mujibu wa taarifa ya Haki za Binadamu ya 2020, matukio 36,940 yalifikishwa vituo vya Polisi kwa kipindi cha mwaka 2015 hadi 2019 ikiwa ni sawa na matukio 7,388 kwa mwaka. Alifafanua Bi. Henga.

No comments:

Post a Comment