SEKTA YA UJENZI KUWAJENGEA UWEZO WAKANDARASI WANAWAKE KANDA YA ZIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 2 August 2021

SEKTA YA UJENZI KUWAJENGEA UWEZO WAKANDARASI WANAWAKE KANDA YA ZIWA

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza Eng. Vedastus Maribe akifungua rasmi mafunzo ya Wakandarasi wanawake wanaotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika utengenezaji wa barabara jijini Mwanza.

Sehemu ya Wakandarasi wanawake wanaotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika utengenezaji barabara wakiwa katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mwanza.

Mgeni rasmi Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza Eng. Vedastus Maribe akiwa katika picha ya pamoja na wataalam toka Wizara ya ujenzi na Uchukuzi.



Sehemu ya Wakandarasi wanawake wanaotumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika utengenezaji barabara wakiwa katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mwanza.

Mgeni rasmi Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza Eng. Vedastus Maribe akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.

IMEELEZWA kuwa kampuni nyingi za wakandarasi wanawake wanaotengeneza barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi zitafanikiwa endapo wakandarasi hao watakuwa na nidhamu ya matumizi  ya fedha.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Mwanza Eng. Vedastus Maribe wakati akifungua mafunzo ya wakandarasi wa barabara kwa kutumia teknolojia stahiki jijini Mwanza.

Eng. Maribe amewaasa wakandarasi hao kujielimisha vya kutosha kabla ya kuomba kazi ya  ujenzi na ukarabati wa miradi ili wapate faida na kukuza kampuni zao.

"Jazeni vizuri 'tender' kwa kuzingatia ukubwa wa kazi, imarisheni usimamizi ili kazi zikamilike kwa wakati, malengo yatimie na kujikomboa kiuchumi," amesema Eng. Maribe.

Amehimiza wakandarasi hao kujisajili ili wapewe miradi mingi na hivyo kukua toka wakandarasi wadogo hadi wakubwa.

Naye Mratibu wa Mafunzo hayo Eng. Liberatha Alphonce amewataka wakandarasi hao kuongeza mtandao wa wadau ili kubadilishana uzoefu, ujuzi na fursa.

Amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina imani na kazi zinazofanywa na wanawake hivyo itaendelea kuwajengea uwezo na kuwapa miradi mingi kutokana na bidii zao.

Zaidi ya wakandarasi wanawake 80, toka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Mara, Geita na Kagera wanashiriki mafunzo hayo ambayo pamoja na mambo mengine yatawajengea uwezo katika ujazaji wa zabuni, taratibu za kusajili kampuni, sheria ya manunuzi, namna ya kutumia mfumo wa manunuzi (TANePS) na usimamizi wa mikataba.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment