ASKOFU GWAJIMA, JERRY SLAA NI WAONGO - BUNGE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 31 August 2021

ASKOFU GWAJIMA, JERRY SLAA NI WAONGO - BUNGE

Askofu Josephat Gwajima (MB).

KAMATI ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge la Tanzania imewakuta na hatia wabunge Josephat Gwajima pamoja na Jerry Silaa ya kwamba wamesema uwongo na kulishushia hadhi bunge hivyo wamesimamishwa kuhudhuria mikutano miwili ya bunge na kupendekeza pia hatua zingine zichukuliwe na vyombo vingine.

Mwenyekiti wa Kamati ya haki, maadili na madaraka ya bunge Emmanuel Mwakasaka, amesema kuwa mbunge Josephat Gwajima amekutwa na hatia baada ya Kamati ya maadili kumuhoji juu ya shutuma zinazomkabili na kisha kukiri kuwa maneno aliyoyatoa ni ya kwake mwenyewe na kwamba alikuwa akiwahubiria waumini wake ulimwenguni kote kuhusiana na Janga la Covid-19 na chanjo ambazo zinatolewa.

Aidha Mwakasaka amesema kuwa kauli za mbunge Josephat Gwajima, zimeleta mpasuko ndani ya nchi hasa wakati huu Tanzania ikikabiliana na mapambano dhidi ya COVID-19 na hivyo kusababisha wananchi kuwa na taharuki hasa wakati huu Tanzania ikiwa imepokea chanjo ya Johnson and Johnson kwa ajili ya kuendesha zoezi la chanjo ambayo ni ya hiyari.

Kamati ya maadili, haki na madaraka ya bunge baada ya kumkuta na hatia mbunge Josephat Gwajima imeazimia kumpatia adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya bunge na kupendekeza kuwa Gwajima ashughulikiwe kwa mujibu wa maadili na afikishwe kwenye chama chake ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia kauli zake.

Wakichangia hoja iliyowasilishwa mezani kwa spika kuhusiana na wabunge Josephat Gwajima na Jery Silaa, wabunge mbalimbali wamesema kuwa Wabunge hao wameonyesha dharau na kiburi hasa wakati walipoitwa mbele ya kamati kuweza kutoa ushahidi na hivyo wanasitaili adhabu

Bunge pia kwa kauli moja limemtia hatiani mbunge wa Ukonga kupitia CCM Jery Silaa na kumsimamisha kuhudhuria mikutano miwili ya bunge na kushauri aondolewe kwenye uwakilishi wa bunge la Afrika Mashariki kufuatia kukutwa na hatia.

Mbunge Silaa amekutwa na hatia baada ya kutoa kauli kuwa Mishahara ya wabunge  Tanzania haikatwi kodi huku mbunge wa Josephat Gwajima akinukuliwa katika moja ya kauli zake kuwa baadhi ya viongozi nchini Tanzania wamepewa fedha ili kuruhusu chanjo kwa Watanzania kitu ambacho ni uwongo.

No comments:

Post a Comment