Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akilihutubia Bunge la 12 na kuelezea Muelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita leo tarehe 22 Aprili, 2021 Jijini Dodoma.
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
DODOMA, 22
APRILI 2021 Mheshimiwa Spika; Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Neema na
Rehma zake, niruhusu niseme kuwa ni miaka takriban 6 imepita tangu niondoke
kwenye Jengo hili adhimu – Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nikiwa
Mbunge.
Hivyo basi,
leo ninayo furaha kurudi tena na kupata fursa hii ya kulihutubia Bunge hili
ambalo limenilea, limenijenga, kuninoa na kufanya uwezo wangu uonekane na wote
mpaka kuweza kushika nafasi hii niliyonayo. Nimefarijika kuona baadhi ya
wenzangu niliokuwa nao bado wapo ndani ya Bunge hili.
Lakini, nimepata faraja zaidi baada ya kuziona
sura mpya zenye ari na matumaini ya kuwatumikia Watanzania. 2 Mheshimiwa Spika;
Nashukuru sana kwa ukarimu wako pamoja na Waheshimiwa Wabunge kunikaribisha leo
hii ndani ya Bunge hili.
Nimekuja kulihutubia Bunge hili baada ya nchi
yetu kupita kwenye kipindi kigumu cha historia ya uongozi. Kama
itakavyokumbukwa, tarehe 17 Machi 2021, Taifa letu lilipatwa na msiba mkubwa wa
kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Kwa sababu
hiyo, kabla sijaendelea mbele na hotuba yangu, naomba sote tusimame kwa dakika
moja tumuombee Hayati Rais Magufuli. Mwenyezi Mungu aipumzishe Roho yake mahali
pema peponi. Amina. Hayati Rais Dkt. Magufuli alikuwa Kiongozi hodari, jasiri
na shupavu; mwenye maono, ambaye aliipenda nchi yetu na kuitumikia kwa uaminifu
na uadilifu mkubwa.
Hivyo basi,
3 napenda nitumie fursa hii kurudia tena kutoa pole nyingi sana kwa familia,
hususan Mama Suzan Magufuli, Mama wa Marehemu; Mjane wa Hayati Dkt. Magufuli,
Mama Janet Magufuli; watoto, ndugu pamoja na jamaa. Napenda pia kutoa pole kwa
Bunge hili Tukufu ambalo kabla awe Rais alikuwa mwenzenu kwa miaka 20. Aidha,
kama ivyofahamika, kwa mujibu wa Katiba yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni sehemu ya Bunge hili.
Hivyo basi,
sina budi kulipa pole Bunge hili. Nitumie fursa hii pia kurudia kuwapa pole
nyingi Watanzania wote kwa kumpoteza Kiongozi wetu mpendwa. Kwa hakika, Taifa
letu limeondokewa na mmoja wa viongozi mahiri, mzalendo, mwana mwema wa
Tanzania ambaye tulimpenda na tunathamini mchango wake kwa taifa.
Mapenzi haya
ya Watanzania yalidhihirika wazi kipindi cha maombolezo 4 na mazishi ambapo
sote tulishuhudia idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kumuaga. Mheshimiwa
Spika, Kufuatia kifo cha Hayati Rais Dkt. Magufuli; tarehe 19 Machi, 2021; kwa
kuzingatia Katiba ya nchi yetu, niliapishwa kushika hatamu za uongozi wa Taifa
letu. Hivyo basi, napenda, kwanza kabisa, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kulipitisha salama Taifa letu kwenye kipindi cha mabadiliko ya uongozi wa Nchi.
Mimi
binafsi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kushusha kudra yake kwangu mimi mja
wake, kwani dhamana hii ni kubwa na yenye mitihani mingi. Hivyo, namwomba
Mwenyezi Mungu anisaidie. Napenda pia nikishukuru Chama changu, Chama Cha
Mapinduzi (CCM), ambacho kimenijengea uwezo mkubwa na wakati wote kimeniamini.
Kama
nisingeaminiwa na Chama 5 changu, huenda leo, nisingekuwa mbele ya Bunge hili
kulihutubia. Nawashukuru pia Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, ambao
wamenilea na kunijengea uzoefu na pia kujiamini. Na hapa naomba niwashukuru kwa
moyo wa dhati kabisa, Waheshimiwa Marais Wastaafu wote pamoja na Viongozi wote
Wakuu wa Kitaifa kwa kuwa nami bega kwa bega katika nyadhifa zangu mbalimbali
za utumishi nilizopitia na kushika. Kipekee kabisa, napenda kutambua mchango na
malezi ya Waheshimiwa Marais Hayati Dkt John Magufuli na Marais Wastaafu Amani
Abeid Karume na Jakaya Mrisho Kikwete.
Niseme wazi
kuwa uwezo wangu wa uongozi uliibuliwa na Mhe. Amani Karume aliyenipa nafasi ya
Uwaziri katika kipindi changu cha mwanzo na cha pili nikiwa Mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar. Malezi haya ya uongozi 6 yaliendelezwa na Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete alienipa Uwaziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na baadaye kuniamini kwenye nafasi ya kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge
la Katiba.
Fursa hii
ilinipa nafasi ya kuwajua na kufanya kazi na baadhi yenu humu ndani na ndiyo
fursa iliyonitambulisha kwa Watanzania. Nimshukuru sana, ingawa hatuko naye
duniani, Hayati Rais Dkt. Magufuli kwa kuniamini kuwa Mgombea Mwenza wake
kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na Mwaka 2020; na hatimaye kuniwezesha kuwa
Mwanamke wa Kwanza nchini kushika wadhifa wa Makamu wa Rais na sasa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa
Spika; 7 Nalishukuru Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano mkubwa ambao limenipa
tangu nimechukua dhamana ya kuliongoza Taifa letu. Nalishukuru sana Bunge kwa
kupitisha Azimio la Kunipongeza na kuniahidi ushirikiano; lakini pia kwa
kuridhia pendekezo langu kuhusu jina la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango.
Wabunge wakipiga makofi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipowasili ndani ya ukumbi wa Bunge leo tarehe 22 Aprili, 2021 Jijini Dodoma. |
Namshukuru
kwa kukubali uteuzi huo na kwamba sasa amejipanga kuchapa kazi kweli kweli.
Siwezi kuhitimisha shukran zangu bila kuwashukuru viongozi wengine wa Serikali
kwa ushirikiano mkubwa walionipa tangu nimekabidhiwa dhamana ya kuliongoza
Taifa letu. Namshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Serikali yake, tumeanza
kufanyakazi kwa ukaribu zaidi.
Namshukuru
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa 8 Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa
Majaliwa; Namshukuru Mheshimiwa Jaji Mkuu na kupitia yeye Mhimili wa Mahakama;
nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri; Katibu Mkuu Kiongozi Ndugu Hussein Kattanga;
Wakuu wa Mikoa; Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wengine wote wa Serikali.
Kwa namna ya
pekee, navishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama, ambavyo kwa ari kubwa
vinaendelea kulinda amani na usalama wa nchi yetu na mipaka yake. Napenda pia
niwashukuru Viongozi wetu wa Dini ambao wakati wote wamekuwa wakifanya dua na
sala kuliombea Taifa letu. Nawashukuru viongozi wa Vyama vya Siasa kwa
ushirikiano wanaonipa.
Navishukuru
Vyombo vya Habari kwa kuendelea kutoa taarifa na kuwaelimisha Watanzania kuhusu
masuala mbalimbali yanayojitokeza nchini. Mwisho, lakini sio 9 kwa umuhimu, nawashukuru
Watanzania wote kwa kuendelea kuniamini na kuiunga mkono Serikali. Mheshimiwa
Spika; Mwaka huu, nchi yetu imetimiza miaka 57 ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar pamoja na Muungano wetu na tutasheherekea miaka 60 ya Uhuru wa
Tanzania Bara.
Katika kipindi
hicho, mafanikio mengi makubwa yamepatikana. Napenda nitumie fursa hii,
kuzishukuru na kuzipongeza Awamu zote za Uongozi wa nchi yetu; kuanzia Awamu ya
Kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere;
Awamu ya Pili ya Mzee Ali Hassan Mwinyi; Awamu ya Tatu ya Hayati Mzee Benjamin
William Mkapa; Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; pamoja na
Awamu ya Tano iliyoongozwa na Mtangulizi wangu, Hayati Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli; 10 kwa mafanikio hayo. Kwa upande wa Zanzibar, nazishukuru awamu zote
nane za uongozi kwa kujenga Ustawi na Maendeleo kwa Wananchi wa Zanzibar mpaka
hatua iliyofikia. Nami nataka, hapa mwanzoni kabisa, nilieleze Bunge hili
Tukufu pamoja na Watanzania kwa ujumla, kuwa, Dira na Mwelekeo wa Serikali ya
Awamu ya Sita itakuwa “Kudumisha mazuri ya Awamu zilizopita, Kuyaendeleza mema
yaliyopo na Kuleta mengine mapya.
Na hii, kimsingi, ndiyo dhana na maana halisi
ya kaulimbiu/salamu yetu ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Kazi Iendelee”.
Tutaenzi na kuendeleza mambo yote mazuri; lakini pia tutafanya mabadiliko pale
itakapobidi kwa lengo la kukuza ufanisi na tija; huku tukiongozwa na Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 –
2025; Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Ajenda ya 11
Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063 na Ajenda ya Dunia ya Malengo ya Maendeleo
Endelevu ya mwaka 2030. Na katika hilo, Mheshimiwa Spika utakumbuka kuwa,
wakati akizindua Bunge hili, tarehe 13 Novemba, 2020; Rais wa Awamu ya Tano,
Hayati Dkt. Magufuli alieleza mambo mengi muhimu ambayo yangepewa kipaumbele na
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwenye miaka hii mitano, kwa kuzingatia Ilani
yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 - 2025. Hivyo basi, kwa kuwa nilishiriki
kikamilifu katika kuinadi Ilani hiyo; na kwa kuwa, kama nilivyowahi kusema, na
leo nataka nirudie tena kuwa, mimi na Hayati Rais Dkt. Magufuli tulikuwa kitu
kimoja.
Kwa sababu
hiyo, mambo mengi ambayo Serikali ninayoingoza imepanga kuyatekeleza ni yale
ambayo yalielezwa na Hayati Rais Dkt. Magufuli wakati akilizindua Bunge hili.
Mheshimiwa Spika; 12 Naomba sasa uniruhusu nitaje baadhi ya masuala muhimu
ambayo Serikali ya Awamu ya Sita itayapa kipaumbele kwenye miaka hii mitano.
Jambo la kwanza na muhimu kabisa tutakalolipa kipaumbele kwenye miaka hii
mitano ni kuendelea kulinda na KUDUMISHA TUNU ZA TAIFA letu, yaani Amani, Umoja
na Mshikamano, Uhuru wa nchi yetu, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na
Muungano wetu. Kama mnavyofahamu, amani na umoja ni msingi mkuu wa maendeleo
katika Taifa lolote. Hivyo basi, nawasihi sana Watanzania wenzangu tushirikiane
kwa pamoja katika kulinda tunu hizi. Tanzania ni yetu sote; kila mmoja wetu
anao wajibu wa kuhakikisha anazilinda na kuzitetea tunu hizi mahali popote
alipo.
Mheshimiwa
Spika; 13 Mbali na kulinda na kuzitunza tunu za Taifa letu, tunakusudia
kuelekeza nguvu kubwa katika KUSIMAMIA UKUZAJI UCHUMI. Kama mnavyofahamu,
kwenye miaka ya hivi karibuni, hususan kwenye miaka mitano iliyopita, Taifa
letu limepata mafanikio makubwa ya kiuchumi. Tumesimamia ukuaji uchumi kwa
wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka; tumedhibiti mfumko wa bei kwa wastani wa
asilimia 4.4; na kupunguza umasikini hadi kufikia asilimia 26.6.
Muhimu
zaidi, mwaka jana, mwezi Julai 2020, Taifa letu lilifanikiwa kuingia kwenye
Kundi la Nchi za Uchumi wa Kati, ambapo Pato la wastani wa kila Mtanzania
limeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani 1,080, zaidi ya kigezo cha Dola za
Marekani 1,036 cha kuingia kwenye Kundi hilo. Haya, bila shaka, ni mafanikio
makubwa. 14 Lakini, pamoja na mafanikio hayo makubwa, ni wazi kuwa jitihada
zaidi zinahitajika ili kukuza uchumi na kupambana na umasikini nchini.
Hii ni kwa
sababu, licha ya mafanikio yaliyopatikana, kasi ya ukuaji uchumi bado ni ndogo.
Wataalam wa Uchumi wanatueleza kwamba, ili kuweza kupambana na umasikini,
uchumi wetu unatakiwa ukuwe angalau kwa asilimia 8 kwa mwaka. Lakini, kutokana
na Dunia kukumbwa na janga la Corona, ki-uhalisia takwimu zinaonesha kwamba
chumi nyingi duniani zimeshuka. Tanzania nayo imeathirika kwa kushuka kwa
kiwango cha uchumi kutoka wastani wa asilimia 6.9 hadi asilimia 4.7. Hii
inamaanisha kwamba katika miaka mitano ijayo kunahitajika uwekezaji mkubwa
katika sekta za uzalishaji na zitazotoa ajira kwa wingi. Hatua mahsusi
zitakazochuliwa katika kukuza Uwekezaji, ni pamoja na kufanya marekebisho
kadhaa katika Sera, Sheria 15 na kanuni zetu na kuondoa vifungu
vitakavyobainika kusababisha vikwazo katika kukuza uwekezaji.
Tutaendelea
kuboresha sera zetu za Uchumi wa Jumla pamoja na sera za fedha, na kuhakikisha
viashiria vyote vya uchumi; ikiwemo thamani ya sarafu yetu, mfumko wa bei
pamoja na viwango vya riba; vinabaki kwenye hali ya utulivu. Sambamba na hilo,
hatutokuwa tayari kuvumilia Uvivu, Uzembe, Wizi na Ubadhirifu wa Mali na Fedha
za Umma. Aidha, tutachukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya biashara
na uwekezaji nchini ili kuivutia sekta binafsi kushiriki vizuri kwenye shughuli
za kiuchumi.
Mwelekeo
utakuwa kurudisha imani kwa wawekezaji na kutoa vivutio kwa wawekezaji mahiri
(Strategic Investors), ikiwa ni pamoja na kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa
haraka. Kutakuwa na Sifa na matakwa maalum yatakayowekwa kwa uwazi katika
kutambua miradi ya kimkakati itakayostahiki 16 vivutio vya kikodi au vivutio
vyenginevyo. Suala la upatikanaji wa mitaji nalo halina budi kuangaliwa kwa
umakini mkubwa.
Kama
mnavyofahamu, ili sekta binafsi iweze kushiriki vizuri, hatuna budi kuboresha
mazingira ya uwekezaji na biashara. Nchi yetu imekuwa ikilalamikiwa kwa
kutokuwa na mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kutokuwa na sera
zinazotabirika, utaratibu wa kodi usio na utulivu, urasimu mwingi katika kutoa
huduma kwa wawekezaji, na matatizo mengine yanayokwamisha ustawi wa biashara na
uwekezaji. Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kufanya maboresho
makubwa kwenye eneo hilo. Kwanza, tutahakikisha tunatekeleza kikakamilifu
Mpango wetu wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini. Zaidi ya hapo, Nimeiweka
Wizara ya Uwekezaji chini ya uangalizi wa Waziri Mkuu ili kurahisisha uratibu
wa pamoja na ukaribu katika kuhakikisha tunaondoa 17 urasimu kwenye masuala ya
Uwekezaji, ikiwemo kutoa vibali na leseni ndani ya muda mfupi na masuala ya
upatikanaji wa ardhi kwa uwekezaji.
Na katika
hilo, narudia wito wangu wa kujenga Dirisha Moja la mfumo wa kutoa Huduma kwa
Mtandao. Tunakusudia kufanya mageuzi ya kiutendaji kwenye mfumo wa utozaji na
ukusanyaji wa kodi, kuweka mfumo utakaorahisisha na kuvutia walipa kodi, na
kutengeneza wigo mpana zaidi wa walipa kodi ikilinganishwa na walipa kodi
waliopo leo.
Tumejitahidi
sana katika awamu ya tano kuongeza makusanyo ya kodi kutoka wastani wa shilingi
bilioni 850 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.9 hivi sasa.
Makusanyo haya yanatokana na Kodi ya Forodha asilimia 40 na Kodi za ndani
asilimia isiyozidi 20. Hii ina maana kwamba ni watanzania wachache ndio
wanaolipa kodi kati ya Watanzania wanaokaribia milioni 60. Hivyo basi, kuna
kila haja 18 ya kutanua wigo wa walipa kodi, na vile vile, kuweka mifumo rafiki
ya ulipaji na ukusanyaji wa kodi.
Ningependa kuona Wafanyabiashara, Wawekezaji
na Wananchi wanalipa kodi bila shuruti na matumizi ya nguvu, wakitambua kwamba
kodi ni maendeleo yao. Tunadhamiria pia kufanya mapitio na uchambuzi wa kina
kwenye uendeshaji wa Mashirika ya Umma, tukiwa na lengo la kuyafanya yaweze
kujiendesha kwa faida. Mashirika yaliyo mengi yanaendeshwa kwa kusuasua kiasi
kwamba unapofika muda wa kutoa gawio la faida Serikalini, uongozi na Bodi za
Mashirika wanahaha kunusuru ajira zao. Vilevile, tutaendelea kufanya kazi kwa
karibu sana na Sekta Binafsi kwa kutambua kuwa wao ndiyo kiini cha ukuaji wa
uchumi. Kwa kudhihirisha hilo, pamoja na mambo mengine, Serikali tunashirikiana
na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kuanzisha mfumo wa kupokea na kushughulikia
changamoto 19 za wawekezaji nchini kwa njia ya mtandao. Lengo la Mfumo huo ni
kurahisisha ushughulikiaji wa changamoto za wawekezaji kwa njia ya haraka na
kuleta ufanisi katika kuwahudumia. Kumekuwa pia na malalamiko mengi kwenye
upatikanaji wa vibali vya kazi kwa wageni.
Kuna msemo
unasema ukimuona mtu mzima analia ujue lipo jambo. Hapa napo kwa kuwa
malalamiko yamezidi hatuna budi kuliangalia upya suala hili, huku tukilinda
maslahi ya Taifa. Ni imani yangu kuwa hatua hizi, pamoja na nyingine ambazo
sikuzitaja, zitavutia wawekezaji na wafanyabiashara wengi ikiwemo wa ndani,
kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nchini na hivyo kusaidia juhudi za Serikali za
kukuza uchumi, kupambana na umasikini na kukabiliana na tatizo la ajira.
Mheshimiwa Spika; 20 Kama unavyofahamu, zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania ni
Wakulima, ambao wanajishughulisha na KILIMO CHA MAZAO, UFUGAJI NA UVUVI.
Hivyo basi,
ni ndoto kwetu kufikiria kwamba tutaongeza kasi ya kukuza uchumi na kukabiliana
na umasikini bila ya kuelekeza nguvu kubwa katika sekta hizo. Ni kweli, kwenye
miaka iliyopita, tumeweza kupata baadhi ya mafanikio kwenye sekta ya kilimo.
Mathalan, sekta hii kwa sasa inachangia asilimia 100 ya chakula nchini,
asilimia 60 ya malighafi za viwandani, asilimia 27.7 ya Pato la Taifa na
asilimia 25 ya fedha za kigeni. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, sekta ya
kilimo bado inakabiliwa na matatizo mengi, lakini kubwa zaidi ni udogo wa tija
au uhaba wa mavuno. Nimeeleza hivi punde kuwa, zaidi ya asilimia 65 ya
Watanzania ni wakulima lakini mchango wao kwenye Pato la Taifa ni asilimia 27
tu.
Hii
inatokana na tija ndogo inayopatikana kwenye kilimo cha 21 mazao mbalimbali
hasa mazao ya biashara. Kwa mfano; kilimo cha mahindi chenye tija kinawezesha
uvunaji wa tani 8 kwa hekta, lakini kwa hapa kwetu wastani wa uzalishaji ni
tani 1.9 tu. Aidha, tunazalisha pamba kilo 250 kwa ekari moja wakati zipo nchi
wanazalisha kati ya kilo 1,000 hadi kilo 1,250 kwa ekari. Na hali hii ipo
kwenye mazao takriban yote. Ukiachilia mbali tija ndogo kwenye kilimo cha
mazao, nchi yetu, licha ya kushika nafasi ya pili kwa mifugo Barani Afrika,
sekta ya mifugo inachangia asilimia 7.4 kwenye Pato la Taifa.
Mwaka
2019/2020 tulizalisha tani 701,679 za nyama na lita bilioni 3 za maziwa. Hii
inatokana na matumizi madogo ya mbinu za kisasa za ufugaji. Mathalan, ng’ombe
wetu kwa wastani wanazalisha lita 3 za maziwa; wakati kwa kutumia mbinu za
kisasa wanaweza kuzalisha lita 20 hadi lita 30 kwa siku. Ng’ombe wetu wengi
wanatoa nyama isiyozidi wastani 22 wa kilo 150; lakini mahali kwingine duniani
ng’ombe wanafikisha kilo 500 – 600 za nyama. Kwa upande uvuvi, nako hali iko
vivyo hivyo.
Licha ya kuwa na maeneo mengi makubwa yenye
kufaa kwa uvuvi, ikiwemo mwambao wenye urefu wa takriban kilometa 1,400, maziwa
makubwa pamoja na mito mingi, mauzo yetu ya samaki nje ya nchi ni madogo na
wakati mwingine nchi yetu inaendelea kuagiza samaki kutoka nje. Hii
inadhihirisha kuwa tija kwenye sekta ya kilimo bado ni ndogo sana. Hivyo basi,
kwenye miaka hii mitano, tutaelekeza nguvu kubwa katika kujenga misingi imara
wa sekta ya kilimo kwa lengo la kuongeza tija.
Tutajitahidi
kuwekeza katika kilimo cha biashara, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kwa
kuongeza uwekezaji kwa Taasisi za Serikali za TARI na ASA ili zizalishe na
kuhamasisha matumizi ya mbegu bora kwa wakulima. Taasisi hizo tutazipa fedha za
kuanzia kama mtaji na tutazitaka 23 ziendelee kuzalisha kibiashara. Hii
itarahisisha upatikanaji wa mbegu bora na kupunguza gharama za kuagiza mbegu
kutoka nje. Shughuli nyingine kwenye sekta hii ni upatikanaji wa mbolea ya kutosha
na kwa wakati, kuboresha afya ya udongo, kukuza huduma za utafiti na huduma za
ugani, kujenga masoko Imara kwa kujenga miundombinu na mfumo na kuwezesha
uuzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi, pamoja na upatikanaji wa mikopo yenye
riba nafuu.
Tutaongeza
pia eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 561,383 hadi hekta milioni 1.2
ifikapo mwaka 2025 ili kupunguza kilimo cha kutegemea mvua. Tutakamilisha
ujenzi wa skimu za umwagiliaji zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi kwa tija.
Na hapa nataka kueleza kuwa Serikali itaanza kutoza ada kwa wakulima wanaotumia
skimu hizo ili kugharamia gharama za usimamizi na uendeshaji.
Vile vile,
tutaendeleza ujenzi wa vihenge na maghala maeneo 24 mbalimbali nchini ili
kuondoa tatizo la upotevu wa mazao baada ya kuvunwa. Kuhusu ufugaji, kama
nilivyowahi kusema, tunalenga kuachana na uchungaji wa kuhamahama. Katika
kutimiza azma hii, tutaelekeza nguvu kubwa katika kuhamasisha ufugaji wa
kisasa.
Tutajielekeza
kwenye uzalishaji kwa njia ya uhamilishaji kwa lengo la kubadili kosaafu
(breed) ya mifugo yetu, ili kuwawezesha wafugaji kuwa na mifugo michache yenye
sifa za uzalishaji mkubwa uwe wa Nyama au Maziwa na kuongeza tija. Tutaongeza
vituo vya kuzalisha mbegu bora na pia kuongeza uzalishaji wa chakula cha mifugo
viwandani kutoka tani 900,000 hadi tani milioni 8, kama ilivyoelekezwa kwenye
Ilani yetu ya Uchaguzi.
Vilevile,
tunakusudia kuongeza maeneo ya ufugaji kutoka hekta 2,788,901 za sasa hadi
hekta 6,000,000. Lengo ni kupunguza tabia ya sasa ya wafugaji kuhamahama, ambayo
25 inasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kuzusha migogoro kati
yao na wakulima. Kwa upande wa uvuvi, tutaimarisha usimamizi wa uvuvi wa Bahari
Kuu ili Taifa letu linufaike na rasilimali zake. Na katika hilo, tumepanga
kununua Meli 8 za Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la IFAD ili zishiriki
katika uvuvi wa Bahari Kuu, ambapo meli 4 zitafanya kazi upande wa Zanzibar na
4 upande wa Tanzania Bara. Aidha, tunakusudia kujenga bandari kwa ajili ya meli
zitakazofanya uvuvi katika maeneo ya ukanda wa Pwani. Tunajipanga kuanza
utengaji wa vizimba vya kuvua samaki baharini, utoaji wa vibali vya uvuvi
katika bahari kuu na uwekezaji katika zana bora za kuvulia pamoja na uanzishaji
wa viwanda vya uchakataji wa samaki na mazao mengine ya majini.
26 Sambamba
na hayo, tunakusudia kuendelea kuimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili
kuiwezesha kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Zaidi ya hapo, tunakusudia kuliangalia kwa karibu zaidi suala la Bima ya kilimo
na kuliwekea misingi imara. Mheshimiwa Spika; Ili kukuza sekta ya kilimo,
hatuna budi pia kuifungamanisha na SEKTA YA VIWANDA.
Kama
nilivyosema awali kwamba kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa malighafi ya
viwandani, aidha, viwanda vinawahakikishia wakulima soko kwa mazao yao. Kwa
bahati nzuri, kwenye miaka mitano iliyopita, tuliweza kuhamasisha ujenzi wa
viwanda vingi nchini, kati yao vikiwemo vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo
na uvuvi. 27 Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza jitihada za
kuhamasisha ujenzi wa viwanda nchini, hususan vile vinavyotumia malighafi za
ndani.
Tunakusudia
pia kutenga maeneo ya viwanda kulingana na mazao yanayozalishwa. Aidha, njia
nyingine itakayotumika kuongeza kasi ya viwanda nchini ni kutenga na kuendeleza
maeneo huru ya biashara, ambapo kipaumbele kitakuwa kwenye maeneo ya mipakani
au maeneo yenye miundombinu thabiti ya usafiri, kama reli, bandari na barabara
zinazotuunganisha na nchi jirani. Na katika hilo, suala la Kongani (Industrial
Parks) ni muhimu sana katika kuchochea ujenzi wa viwanda na pia kuiwezesha nchi
yetu kunufaika na vyema fursa za kibiashara, ikiwemo kupitia itifaki mbali
mbali kama vile EAC, SADC, Eneo Huru la Biashara la Afrika; n.k. 28 Mheshimiwa
Spika; SEKTA YA MADINI, ambayo kwa sasa imetoa ajira zipatazo milioni 1.5, ina
nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji uchumi nchini. Kwenye miaka mitano iliyopita,
tumepata mafanikio makubwa kwenye sekta hii. Mchango wake kwenye Pato la Taifa
umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka
2019.
Mapato yake
yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni
527 mwaka 2019/2020. Zaidi ya hapo, mwaka 2019, sekta ya madini iliongoza kwa
kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7.
Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kuendeleza mafanikio hayo kwa kusimamia
Sheria yetu ya Madini ya mwaka 2017, kuendelea kuziba mianya ya utoroshaji wa
madini yetu, tutaendelea kuangalia kwa umakini mkubwa na kuondoa 29 vikwazo vya
uwekezaji katika sekta hii, ili kuvutia na kurahisisha mijadala ya Serikali
kuingia ubia na wachimbaji wakubwa Duniani.
Tutaendelea
pia kuimarisha masoko na minada ya uuzaji madini, kuhamasisha ujenzi wa viwanda
vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji wa bidhaa za madini.
Mkazo utawekwa kwenye ubora na ufanisi wa teknolojia. Tutawaendeleza wachimbaji
wadogo na kuwapatia mafunzo, mikopo pamoja na vifaa.
Vilevile,
Tutaliimarisha zaidi Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) ili lishiriki
kikamilifu kwenye shughuli za madini. Hatua hizi naamini, zitaifanya sekta ya
madini ikuze mchango wake kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka
2025. Mheshimiwa Spika; Sekta nyingine ambayo tutaipa mkazo mkubwa kwenye miaka
hii mitano ni UTALII. Kama mnavyofahamu, nchi yetu 30 imebarikiwa kuwa ni
vivutio vingi vya utalii na sekta hii imeajiri takriban watu milioni 4. Kwenye
miaka mitano iliyopita, mafanikio mengi yamepatikana kwenye sekta ya utalii,
ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watalii waliotembelea nchini kutoka milioni 1.1
mwaka 2015 hadi watalii milioni 1.5 mwaka 2019. Mapato nayo yaliongezeka kutoka
Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni
2.6 mwaka 2019. Hivyo basi, kwenye miaka hii mitano, pamoja na uwepo wa janga
la Corona, tunalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana, kwa kuongeza idadi ya
watalii hadi kufikia milioni 5 mwaka 2025 na mapato kutoka Dola za Marekani
bilioni 2.6 za sasa hadi Dola za Marekani bilioni 6.
Hatua ambazo
tunakusudia kuzichukua ni pamoja na kupanua wigo wa vivutio vya utalii, ikiwemo
kukuza utalii wa mikutano, 31 malikale na fukwe; ambapo tunakusudia kujenga
miundombinu ya kuwezesha meli za utalii kuzuru nchini. Tutahamasisha pia
wawekezaji kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii, ikiwemo hoteli, ili kupunguza
gharama za malazi. Tunajipanga kusomesha vijana wengi katika taaluma ya utalii
ili waweze kuendesha maeneo mbali mbali ya sekta bila kutegemea wataalamu
kutoka nje. Mheshimiwa Spika; Ili kuchochea shughuli za kiuchumi na uzalishaji
nilizozitaja (yaani kilimo, viwanda, madini na utalii) tutaendeleza jitihada za
kuimarisha MIUNDOMBINU YA USAFIRI, ambayo ni moyo wa ukuzaji uchumi.
Kwenye miaka
mitano iliyopita, jitihada kubwa zilifanyika za kuimarisha usafiri wa barabara,
reli, maji na anga. Jumla ya kilometa 3,537 za barabara za lami zilijengwa
pamoja na madaraja makubwa 12. Usafiri wa 32 reli kutoka Dar es Salaam – Tanga
– Moshi – Arusha ulifufuliwa pamoja na kuanza ujenzi wa Reli ya Standard Gauge
kutoka Dar es Salaam hadi Makutopora (Dodoma), ambapo kipande cha Dar es Salaam
– Morogoro kimefikia asilimia 91 na Morogoro – Makutupora zaidi ya asilimia
58.2 hadi kufikia mwezi Aprili 2021.
Kwa upande
wa usafiri wa maji, umefanyika upanuzi mkubwa wa Bandari za Dar es Salaam,
Tanga na Mtwara pamoja na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala Mkoani Pwani. Kwenye
Ziwa Victoria, tumejenga chelezo, tumekarabiti meli mbili (MV. Victoria na MV.
Butiama) pamoja na kujenga meli mpya. Katika Ziwa Tanganyika, umefanyika
upanuzi na ukarabati mkubwa wa Bandari za Kigoma, Kalema, Kasanga na Kabwe; na
kwenye Ziwa Nyasa zimejengwa meli mpya tatu na kufanya upanuzi wa Bandari za
Kiwira na Itungi.
Kuhusu 33
usafiri wa anga, jumla ya viwanja vya ndege 11 vimepanuliwa ama kukurabatiwa na
ndege mpya 11 zimenunuliwa. Kwenye miaka hii mitano, tutatekeleza yaliyoagizwa
kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuendeleza ujenzi wa miundombinu hiyo ya
usafiri. Tutaendelea kukamilisha ujenzi wa Bandari za Dar es Salaam, Tanga,
Mtwara na Kigoma, kujenga barabara, hususan kwenye maeneo ya kimkakati, ambako
shughuli za uzalishaji zinafanyika.
Tukamilisha pia ujenzi wa madaraja makubwa,
likiwemo la Kigongo – Busisi, Wami, Tanzanite na Pangani. Kwa upande wa reli,
tutakamilisha ujenzi wa reli ya Dar es Salaam – Makutupora na kuanza ujenzi wa
vipande vingine, kikiwemo cha Mwanza – Isaka (lot5); Makutupora – Tabora (Lot
3); Tabora – Isaka (Lot 4) na baadaye Tabora – Kaliua – Kigoma na Kaliua –
Mpanda.
Aidha,
tunakusudia kuimarisha usafiri wa TAZARA kwa lengo 34 la kuiongezea ushindani
Bandari yetu ya Dar es Salaam na pia kunufaika na fursa nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wa usafiri wa majini, tutakamilisha ujenzi wa meli mpya na kuanza
ukarabati wa meli ya mabehewa (yaani Ferry Wagon) kwenye Ziwa Victoria na pia
kuikarabati meli ya Mv. Liemba na kuanza ujenzi wa meli mpya kwenye Ziwa
Tanganyika.
Kuhusu
usafiri wa anga tutaendelea na upanuzi wa viwanja vya ndege mikoani, na kujenga
Kiwanja kipya cha Kimataifa cha Msalato hapa Makao Makuu Dodoma. Aidha,
tutaendelea kulilea Shirika letu la Ndege (ATCL) kimkakati ili liweze
kujiendesha kwa ufanisi. Ninaposema kimkakati ni pamoja na kuangalia uwezekano
wa kutoa unafuu wa madeni na baadhi ya kodi na tozo, kama inavyofanyika kwenye
nchi nyingine, ili liweze kukua. Shirika letu linaonekana kupata hasara
kutokana na mzigo mkubwa wa madeni ya nyuma. Sote 35 tunafahamu kuwa biashara
ya ndege ni ngumu.
Tutajitahidi
kusoma mwenendo wa biashara hii ulimwenguni na kuepuka mambo yote yasiyo na
tija kwa shirika letu. Hatutakubali kuona Shirika linaendelea kupata hasara
baada ya uwekezaji mkubwa tulioufanya. Tutafanya uchambuzi wa kina ili watu
watakaoendesha Shirika wawe na weledi na ujuzi wa biashara. Zaidi ya hapo,
tutawekeza kwenye kupata rasilimali watu wenye uwezo na weledi wa kuendesha
shirika kibiashara. Mheshimiwa Spika; Mbali na miundombinu hiyo migumu,
tutaimarisha pia miundombinu laini, hususan miundombinu ya TEKNOLOJIA YA
MAWASILIANO.
Kama
inavyofahamika, dunia ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, ambayo
yanaongozwa na sekta ya Teknolojia ya Mawasiliano (TEHAMA), na kwa maana hiyo,
Uchumi wa dunia pamoja na shughuli nyingi 36 duniani, kwa sasa, zinafanyika kwa
kutumia TEHAMA. Hivyo basi, sisi Tanzania nasi hatuna budi kuweka mkazo mkubwa
katika kukuza sekta hii. Kwa msingi huo, tumepanga, kwenye miaka hii mitano,
pamoja na masuala mengine, kuongeza kasi ya kufikisha miundombinu ya Mkongo wa
Taifa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu, hususan katika ngazi za Wilaya, na pia
kuongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi (yaani broadband) kutoka
asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.
Aidha,
kuongeza watumiaji wa internet kutoka asilimia 43 ya sasa hadi asimilia 80
mwaka 2025; na pia, kuboresha upatikanaji wa mawasiliano ya simu nchi nzima.
Tutatoa kipaumbele kwenye masuala ya utafiti na ubunifu kwenye TEHAMA pamoja na
kuimarisha usalama kwenye masuala ya Mawasiliano. 37 Mheshimiwa Spika; Kwenye
miaka mitano iliyopita, tumepata mafanikio makubwa kwenye SEKTA YA NISHATI.
Tumeongeza uzalishaji umeme hadi kufikia Megawati 1602.3; ambapo mahitaji ya
juu ya umeme kwa nchi yetu kwa sasa ni Megawati 1,200. Tumefanikiwa pia
kufikisha umeme kwenye vijiji 10,294, sawa na asilimia 83.3 ya vijiji 12,317
vilivyopo.
Tumeanza pia utekelezaji wa mradi mkubwa wa
umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere utakaozalisha Megawati 2,115. Mradi huu kwa
sasa umefikia asilimia 45. Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza
jitihada za kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini, ikiwemo kukamilisha
ujenzi wa Bwawa la Nyerere, na kufikisha umeme kwenye vijiji 1,974
vilivyobakia.
Tunajipanga
kuanza kutekeleza miradi ya kuzalisha umeme wa maji ya Ruhudji Megawati 358; 38
Rumakali Megawati 222; Kikonge Megawati 300 na pia umeme wa gesi asilia Mtwara
Megawati 300; Somanga Fungu Megawati 330, Kinyerezi III Megawati 600 na
Kinyerezi IV Megawati 300.
Kutokana na
kasi ya mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji kuchanganya vyanzo vya nishati ili
kuwa na uhakika wakati wote. Hivyo basi, tutaangalia uwezekano wa kutekeleza
miradi ya nishati jadidifu (jua, upepo, jotoardhi) kwa kuwa vyanzo hivi ni
endelevu. Tunatarajia katika miaka hii mitano kuzalisha Megawati 1,100
kupitiavyanzo hivyo.
Katika hatua
nyengine, tutaendelea kutekeleza miradi ya kujenga njia za kusafirisha umeme
kutoka Bwawa la Nyerere hadi kituo kikuu Chalinze na njia zinazoelekea kwenye
maeneo ambayo hayajaunganishwa na Gridi ya Taifa ili kupunguza gharama za
kuzalisha umeme wa mafuta na umeme unaopotea. Sambamba na hayo, tunatarajia
kuanza utekelezaji wa Miradi ya 39 kielelezo ya Bomba la Mafuta kutoka Hoima
nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga lenye urefu wa kilometa 1,445 pamoja na
Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) Mkoani Lindi. Mradi huu umechukua muda
mrefu; hivyo, tunakwenda kumaliza majadiliano ili Mradi huu uanze kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika; Mbali na shughuli hizo za kuchochea ukuaji uchumi nilizozitaja,
katika kipindi hiki cha miaka mitano, tutaendelea kuimarisha na kuboresha
HUDUMA ZA JAMII, hususan afya, elimu na maji.
Kuhusu AFYA, kama mnavyofahamu, kwenye miaka
mitano iliyopita tumepata mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga vituo vya kutolea
huduma za afya 1,887 (zikiwemo zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za
wilaya 99, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na Hospitali za Rufaa za Kanda 3). 40
Katika miaka hii mitano mpaka 2025, tutaimarisha upatikanaji wa huduma za afya
kwa kuendelea kujenga miundombinu, kuongeza watumishi, vifaa tiba, dawa na
vitendanishi.
Aidha,
juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito na watoto zitaendelezwa. Nilipokuwa
Makamu wa Rais nilizindua Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ili kutilia
mkazo uwajibikiaji wa wadau wote katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Hivyo, huu ni mradi wangu wa moyoni kabisa. Binafsi, huwa nasikitishwa sana
kusikia mwanamke anapoteza maisha wakati wa kujifungua kwa sababu ambazo
zingeweza kuzuilika.
Tutaelekeza
pia nguvu katika kinga na tiba, ikiwemo kwa magonjwa yasiyoambukiza, ambayo
yanasababisha vifo vingi na kugharimu Serikali fedha nyingi. Tutaimarisha pia
huduma za matibabu ya kibingwa na kuzipeleka huduma hizi kwenye 41 Hospitali za
Rufaa za Mikoa. Tutaimarisha utoaji wa huduma za matibabu kwa wazee; na
kutaweka mipango maalum kuhudumia makundi yenye magonjwa adimu. Tutaimarisha
Mifuko ya Taifa ya Bima ya Afya ili kufikia lengo la Bima ya Afya kwa wote. Kwa
sasa ni watu 8,224,271 sawa na asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wanaotumia
Bima ya Afya. Vilevile tutahamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa,
vitendanishi, vifaa tiba pamoja na chanjo mbali mbali. Kuhusu ugonjwa wa
corona, kama mnavyofahamu, ugonjwa huu umeathiri dunia nzima na ubaya zaidi ni
kwamba janga hili linapungua na kurudi katika mifumo tofauti tofauti. Mpaka
sasa bado hakujawa na dalili za kupatikana kwa tiba ya maradhi haya. Njia pekee
iliyopo ni kujikinga na kuchukua hatua mbali mbali za tahadhari.
Hapa nchini
tumekuwa tukifuata miongozo kadhaa ya kinga inayotolewa na wataalam, 42 na kwa
kutumia njia zetu za tiba asilia tumeweza kwa kiasi kikubwa kushusha kiwango
cha maambukizi. Hapa nchini, tumeamua kuunda Kamati ya Wataalamu ambao kwa
kushirikiana na taasisi za Afya Duniani na zile za Kikanda za EAC na SADC
wataliangalia suala hili kwa undani, kufanya uchambuzi wa kina na kutoa
mapendekezo ya hatua za kuchukua na jinsi ya kuendelea kupambana na maradhi
hayo.
Hivyo,
wakati tukisubiri majibu ya Kamati iliyoundwa, napenda kutumia fursa hii kutoa
wito kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari zote kama zinavyoshauriwa na
wataalam. Nawaomba kila mmoja awajibike kwani ulinzi wa afya yako unaanza na
wewe mwenyewe. Kwenye Sekta ya ELIMU, katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, udahili wa wanafunzi katika ngazi za elimu Msingi na Sekondari
uliongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na Sera 43 ya elimu bila malipo.
Ongezeko
hilo limeilazimu Serikali kuweka nguvu kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu,
kuongeza idadi ya walimu hasa walimu wa sayansi na hisabati, na kusambaza vitendea
kazi mashuleni. Kumekuwa na ongezeko la kiwango cha mfuko wa elimu ya juu ambao
umeongeza pia idadi ya vijana wanaoingia vyuo vikuu. Awamu ya sita itaendeleza
kazi nzuri iliyofanywa miaka mitano iliyopita. Aidha tutajielekeza katika
kufanya mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na kufanya marekebisho kwenye
Mitaala iliyopo ili ielekezwe kwenye kutoa elimu ujuzi kulingana na mazingira
ya nchi na soko la ajira. Kwa upande wa MAJI, licha ya mafanikio yaliyopatikana
kwenye miaka mitano iliyopita; tatizo la maji bado ni kubwa kwenye maeneo mengi
nchini.
Hali hii
inachangiwa na usimamizi usioridhisha wa miradi, na vile vile, matumizi 44
mabaya ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Miradi mingi imekuwa ikitekelezwa kwa kutumia fedha nyingi; lakini baada ya
muda mfupi maji hayapatikani. Hivyo basi, katika miaka hii mitano, tutaweka
mkazo mkubwa katika kuimarisha usimamizi kwenye utekelezaji wa miradi ya maji.
Na katika
hilo, nakusudia kufanya mabadiliko makubwa kwa Wahandisi wa Maji wa Mikoa,
ambao hawafanyi kazi vizuri. Lengo letu ni kufikia azma ya kufikisha maji kwa
wananchi kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijiji ifikapo mwaka 2025.
Lakini, ili kuweza kufikisha maji kwa Watanzania wengi, hatuna budi kuhakikisha
tunalinda na kutunza vyanzo vyetu vya maji. Aidha, kwa maeneo yasiyokuwa na
vyanzo vya maji, tutajielekeza katika ujenzi wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua.
Vilevile, Kamati za Maji za Mitaa na Vijiji zinaimarishwa 45 ziweze kutimiza
majukumu yao ipasavyo.
Zaidi ya
hapo, tutatafuta vyanzo vingine vya kutunisha Mfuko wa Maji. Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Mahusiano na Ushirikiano na Mataifa mengine na Taasisi za Ki
dunia, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kutekeleza shughuli za Kidiplomasia
kuendana na Sera ya Diplomasia ya Uchumi. Hivyo basi, tutaimarisha na kukuza
Uhusiano na Mataifa mengine pamoja na jumuiya za kikanda na Taasisi za
Kimataifa. Ili kutimiza azma hiyo, tunakusudia kuimarisha utendaji kazi wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Balozi zetu
zilizoko nchi mbali mbali duniani, kwa kuajiri watumishi wenye sifa na weledi
wa kazi na kusambaza vitendea kazi, pamoja na kutumia kiuchumi 46 majengo na
viwanja ambavyo ni mali ya Tanzania vilivyoko nje ya nchi. Kwa madhumuni ya
kuwezesha utekelezaji mzuri wa Diplomasia ya Uchumi, tutafungua na kuanzisha
pia Balozi mpya, Konseli pamoja na Vituo vya Biashara kwenye nchi na miji ya
kimkakati ili kutangaza vivutio vyetu vya utalii, kuvutia uwekezaji na kutafuta
masoko ya bidhaa zetu.
Tutafanya
uchambuzi wa kitaalamu utakaobaini nafasi ya kila ofisi ya ubalozi katika
kukuza biashara, uwekezaji na utalii. Uchambuzi huo ndio utatumika kupanga
maafisa kulingana na uwezo wa kila Ubalozi. Zaidi ya hapo, tutaendelea
kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kimataifa, ikiwemo ushiriki wetu kwenye
kulinda amani duniani. Tunakusudia pia kufanya mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje
ya mwaka 2000 ili iendane na mahitaji ya sasa ya dunia. 47 Mheshimiwa Spika;
Maeneo mengine ni pamoja na kuendelea kulinda misingi ya demokrasia na uhuru wa
watu pamoja na vyombo vya habari.
Kama
mnavyofahamu, uhuru na demokrasia ni msingi wa amani katika nchi na pia
vinasaidia kuchochea maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hata hivyo,
naomba niseme kuwa, hakuna uhuru ama demokrasia isiyolindwa na kusimamiwa na
Sheria, Taratibu na Kanuni. Hivyo basi, pamoja na demokrasia na uhuru wa watu,
niwaombe Watanzania tujidhatiti kufanya shughuli zetu tukizingatia masharti ya
sheria za nchi.
Hapa
nakusudia kukutana na Viongozi wa vyama vya Siasa Tanzania ili kwa pamoja
tuweke mwelekeo wa kuendesha shughuli za kisiasa zenye tija na maslahi kwa nchi
yetu. Katika hatua nyingine, Tutashirikiana pia na Mhimili wa Mahakama katika
kuimarisha mifumo ya utoaji haki, ikiwemo 48 kuendelea kujenga miundombinu ya
mahakama, kuongeza idadi ya majaji na mahakimu, na kukuza matumizi ya TEHAMA
ili kuongeza kasi ya usikilizaji wa kesi na uwekaji mzuri wa kumbukumbu. Niombe
Mahakama yetu na vyombo vya utoaji haki kuzielekeza zaidi nafsi zetu katika kutenda
na kuhukumu yaliyo ya haki kwa wananchi. Na katika hilo, tutaendelea
kuziimarisha taasisi nyingine za usimamiaji haki ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu, Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi, TAKUKURU,
Magereza, n.k.
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Sita kama ilivyokuwa awamu ya tano, itaendeleza jitihada
za kuimarisha nidhamu na uwajibikaji kwenye utumishi wa umma. Tunakusudia
kuimarisha taasisi na pia kuweka mifumo ya uwajibikaji, ambayo itahakikisha
kwamba viongozi na watumishi wa umma katika ngazi zote 49 wanawekewa malengo
yanayopimika. Mfumo uliopo sasa ikiwemo mikataba kati ya kiongozi na walio
chini yake pamoja na OPRAS tutaiangalia upya. Tutawapima viongozi na watumishi
kwa namna wanavyotimiza majukumu yao. Hatutawaonea aibu viongozi na watumishi
wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma.
Tutaendeleza
pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma. Wajibu huu wa
wafanyakazi wa umma ni lazima uendane na haki zao. Hivyo basi, tutasimamia
mageuzi katika Utumishi wa Umma na kutazama maslahi ya watumishi, ikiwemo suala
la upandishaji vyeo na mishahara. Tutaendelea pia na jitihada za kuwawezesha
wananchi kiuchumi, hususan wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Na katika
hilo, tutaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kupitia mapato ya ndani ya
Halmashauri (wanawake asilimia 4, vijana 50 asilimia 4 na wenye ulemavu
asilimia 2) pamoja na kuimarisha Mifuko mingine ya Uwezeshaji Wananchi.
Tutaendelea pia kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali
wadogo (machinga, mama lishe, baba lishe, waendesha boda, bajaji, n.k.),
ikiwemo kwa kuwatengea maeneo mazuri ya biashara na kuwawekea miundombinu
pamoja na kuviboresha Vitambulisho vyao ili viwe na taarifa muhimu
zitakazowawezesha kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kubughudhiwa; lakini
pia kutambulika kwenye Taasisi mbali mbali wanakofuata huduma. Mheshimiwa
Spika; Sekta ya sanaa, michezo na utamaduni inakua kwa kasi kubwa hivi sasa.
Vijana wetu
wengi wamepata ajira kupitia sekta hii. Hivyo basi, kama ilivyoahidiwa kwenye
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, kwenye miaka hii 51 mitano,
tunakusudia kuikuza zaidi sekta hii, hususan kwa kuimarisha usimamizi wa
masuala ya Hati Miliki ili wasaniii waweze kunufaika na kazi zao; tutahuisha
Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu, ikiwemo kupata mafunzo
na mikopo.
Aidha,
tutaanza kidogo kidogo kuanza kutenga fedha kwa ajili ya kuziandaa Timu zetu za
Taifa, zikiwemo za wanawake. Tumechoka kuwa kichwa cha mwandawazimu kwenye
michezo. Masuala mengine ambayo yatapewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya
Sita ni kuendeleza ujenzi wa Makao Makuu ya Serikali Jijini Dodoma. Aidha, kwa
kuzingatia vigezo na sifa tutakuza usawa wa jinsia kwa kuwateua wanawake wengi
zaidi kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.
Zaidi ya
hapo, tutazidisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya; uendelezaji na uboreshaji
wa makazi wa wananchi, ambapo 52 tutahakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana
kwa gharama nafuu na mikopo ya ujenzi inapatikana kwa riba nafuu; tutaimarisha
taasisi zetu za utafiti na kuendelea kushughulikia kero mbalimbali za wananchi,
ikiwemo migogoro ya ardhi.
Tutaweka mkazo katika kushughulikia masuala ya
Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi ili kupunguza athari zinazotokana na
mabadiliko hayo kwa maisha ya watu na shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Kitaifa, mbali na Sheria yetu ya Mazingira ya mwaka 2004, Bunge liliridhia
Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris. Tutaendelea kushirikiana na
mataifa mbalimbali katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Tayari tumeandaa Mpango wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Paris 2021-2026
unaolenga kujenga uwezo katika kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi
katika sekta za kilimo, mifugo, misitu, nishati, uvuvi, 53 maji, utalii,
makazi, afya, miundombinu na pia kukabiliana na maafa.
Mheshimiwa
Spika; Ili kutimiza masuala hayo yote niliyoeleza, Bunge hili lina umuhimu wa
pekee sana. Kama mnavyofahamu, mbali na kutunga sheria, Bunge lina wajibu wa
kuisimamia Serikali. Aidha, ninyi Wabunge ni wawakilishi wa wananchi na kwa
maana nyingine, ninyi ni sauti ya wananchi. Hivyo, sitegemei kuona Bunge hili
likijieleza kujadili masuala ambayo hayana manufaa kwa Taifa letu.
Na hili
nalisema kwa vile natambua, bila ya ushirikiano wa Bunge hili, itakuwa vigumu
sana kwa Serikali kuweza kutekeleza masuala yote niliyoyaeleza. 54 Hivyo basi,
napenda kutumia fursa hii kuliomba Bunge hili Tukufu kutoa ushirikiano kwa
Serikali. Tukoseeni pale inapobidi. Mawaziri wakileta vitu visivyoeleweka
wakososolewe lakini kwa staha. Nami naahidi kuwa Serikali itakuwa tayari,
wakati wote, kupokea ushauri wenu na pia ushauri wa watu wengine wenye nia ya
kuiletea maendeleo nchi yetu.
Nitumie pia
fursa hii kuwaomba wananchi pia, kuendelee kuiunga mkono Serikali kwa kudumisha
amani, kuchapa kazi kwa bidii na bila kusahau kulipa kodi, ili kwa pamoja
tuweze kutimiza tuliyoyakusudia. Mheshimwa Spika; Kabla sijahitimiza hotuba
yangu, naomba kueleza masuala mawili. Kwanza, naomba kutumia jukwaa hili la
Bunge lako Tukufu kuwaonya wale wote wanaodhani kuwa usimamizi wa mali ya umma
kwa maslahi ya wananchi, kukataa ukwepaji wa 55 kodi, wizi, na kukemea uzembe
vitasimama kwa sababu tu Rais Magufuli hayupo. Napenda kuwaambia kwamba
wanajidanganya. Hatuko tayari kurudi nyuma. Kama mtu ana dhamira ya kuendeleza vitendo
hivyo basi ni kwa gharama yake. Pili, tangu kifo cha mpendwa wetu, Hayati Rais
Dkt. Magufuli kumetokea tabia ya watu kuzusha maneno ya uchonganishi kwenye
mitandao. Mtakumbuka kuwa, Serikali ilikwishatoa taarifa kwamba, Hayati Dkt.
Magufuli alifariki kwa ugonjwa wa udhaifu wa moyo.
Kwa hiyo,
taarifa zinazotolewa kwenye mitandao kwamba kuna watu wamehusika ni uzushi
mtupu. Hivyo basi, natoa onyo kwa watu wanaoeneza uzushi huo kuacha mara moja
kwa vile Serikali itawatafuta kokote walipo. 56 Mheshimiwa Spika; Hii ni mara
ya kwanza kwenye historia ya Taifa letu kupata Rais Mwanamke. Kwa sababu hiyo,
ninajua, watakuwepo baadhi ya watu wachache wenye wasiwasi kwamba kutokana na
jinsia yangu sitoweza kuyatimiza yote niliyoyasema hapa.
Nataka
nitumie jukwaa hili kuwaondoa hofu kwamba kwanza, Mwenyezi Mungu hakuumba
Ubongo hafifu kwa mwanamke na Ubongo wenye uwezo mkubwa kwa mwanaume. Makuzi na
umakini wa akili hutegemea jamii inayokuzunguka na shughuli unazokuwa nazo.
Nataka nikuhakikishieni kuwa nimekuzwa kwenye jamii sahihi na kwamba nina
uzoefu wa kutosha kwenye Serikali na kwenye Chama changu cha Siasa CCM.
Hivyo basi,
ninajiamini kuwa ninao uwezo wa kuliongoza Taifa hili. Pili, kazi hii
sitoifanya peke yangu bali nitashirikiana 57 na Watanzania wote. Wito wangu kwa
Watanzania, tushirikiane, tushikamane na kuwa kitu kimoja katika kulijenga
Taifa letu. Binafsi naamini, tukiwa na upendo, mshikamano na kuheshimiana, na
kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, tutaweza kufika kule ambako sote tunamani
tufikie. Baada ya kusema hayo Mheshimiwa Spika nimalizie kwa kumuomba Mungu
alibariki Bunge hili pamoja na Wabunge wake! Mungu aibariki Tanzania!
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Ahsanteni sana kwa
Kunisikiliza”
No comments:
Post a Comment